Home Kitaifa Zahera afichua siri ya kuvunja rekodi ya Mbao Mwanza

Zahera afichua siri ya kuvunja rekodi ya Mbao Mwanza

3074
0

Kocha wa Yanga Zahera Mwinyi amefichua siri ya ushindi wa kwanza wa timu yake dhidi ya Mbao FC kwenye uwanja wa Kirumba Mwanza. Kabla ya ushindi huo wa 2-1 kwenye mchezo wa ligi, Yanga ilikuwa imepoteza mechi 3 dhidi ya Mbao kwenye uwanja wa Kirumba.

Zahera anasema aliwapa masharti wachezaji wake kabla ya kutoka hotelini kwenda uwanjani kwamba mchezaji ambaye haamini Yanga itashinda dhidi ya Mbao abaki hotelini asiende uwanjani.

“Niliwaambia wachezaji wangu kila kitu kina mwanzo na mwisho. Wakati tunatoka hotelini kwenda uwanjani, niliwaambia wachezaji kama kuna mtu haamini tunaenda kushinda mechi dhidi ya Mbao asiingie kwenye basi.”

“Nikasema, atakayepanda basi ni yule anaeamini tunakwenda kushinda mbele ya Mbao. Wakati wa mapumziko nikawaambia hamjacheza vibaya kipindi cha kwanza, mkiingia kipindi cha pili ongezeni kasi mbele, chezeni mipira mingi pembeni halafu mpige krosi tutapata goli.”

“Niliwaambia wachezaji hakuna haja ya kulalamika, Mbao hakuna chochote walichotuzidi kipindi cha kwanza licha ya kuongoza 1-0.”

“Nikawakumbusha tena kuwa tulikubaliana wanaoingia kwenye basi ni wale wanaoamini tutashinda mechi kwa Mbao, kwa hiyo turudi kipindi cha pili tukashinde mechi.”

Zahera pia amemtetea golikipa wake Ramadhani Kabwili ambaye mashabiki wengi wanambebesha lawama kutokana na aina ya goli alilofungwa na mshambuliaji wa Mbao Robert Ndaki.

“Nadhani golikipa wetu hakupata hata mpira mmoja, Mbao hawakupiga shuti hata moja golini. Wakati mwingine mpira ni bahati, walipiga krosi golikipa wangu akawa anatoka akatereza ambacho ni kitu cha kawaida kinaweza kumkuta mchezaji yeyote.”

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here