Home Kitaifa Tathmini ya mchezo wa watani

Tathmini ya mchezo wa watani

6718
0

Bao la dakika ya 71 la Meddie Kagere, limetosha kuwatenganisha watani wa jadi wa Dar Es Salaam katika mchezo wao wa 102 wa ligi, tangu wakutane mara ya kwanza 1965.

YANGA

Wakicheza kwa sehemu kubwa katika mfumo wa 3-5-2, Yanga hawakuonesha nia ya kutafuta ushindi, zaidi ya sare au kufungwa mabao machache. Hii inathibitishwa na kikosi ambacho mwalimu Zahera, alianza nacho. Kumfanya Feisal acheze chini, badala ya katikati kwenye wale watano, kunadhihirisha ni namna gani kocha hakutaka kushambulia.

Tshishimbi, ambaye angetarajiwa kuunganisha safu ya ushambuliaji na ulinzi, alionekana kushuka chini na kupanda kwa nadra.

Matokeo yake, Ajib ambaye angetumika kama kiunganishi cha Makambo na Tambwe, akawa anashuka kufuata mipira ili kupandisha timu. Hilo likasababisha washambuliaji hao wakose madhara.

Nilitarajia kuona Feisal akipanda juu kidogo halafu Ajib aachwe acheze huru na kuifungua safu ya ulinzi ya Simba, kwa ubunifu wake.

Upande mwepesi kwa Yanga kupita ulikuwa kushoto ambako Zimbwe Jr. hakucheza kwa nidhamu ya ulinzi. Zahera angemtuma Ngassa aongeze presha upande huu na kumlazimisha Zimbwe Jr. kurudi nyuma. Hii ingemlazimisha kufanya makosa zaidi ya aliyokuwa akiyafanya bila presha. Lakini Zahera alikuwa na mipango yake.

YONDANI AMPOTEZEA AJIB

Katika hali ya kushangaza, nahodha mstaafu wa Yanga, Yondani, alikataa kushikana mkono na mrithi wake, Ajib, kabla ya kuanza kwa mchezo. Haijafahamika ni kwanini, lakini yawezekana ni vita ya kitambaa cha unahodha.

NGASSA NAHODHA WA WATANI

Tangu ajiunge na Yanga mwaka 2007, kwa mara ya kwanza Ngassa amevaa kitambaa cha unahodha kwenye mechi ya watani. Ilikuwa baada ya kutoka kwa nahodha Ajib.

NINJA NOMA

Ninja alionesha kwanini Yanga walimuombea kwa TFF, shauri lake lisogezwe mbele. Uwepo wake ulikuwa nguzo kuu katika safu ya ulinzi ya Yanga. Aliokoa mpira uliokuwa ukielekea wavuni.

KABWILI HAKUTESWA

Tofauti na yaliyomtokea Kakolanya kwenye mchezo wa kwanza, Ramadhan Kabwili hakuwa na wakati mgumu sana safari hii.

ZAHERA HAKUJUA

Baada ya mchezo dhidi ya JKT kule Tanga, Zahera alisema hakujua kama mchezo wao ujao ni dhidi ya Simba. Yawezekana angejua mapema, angeshinda!

SIMBA

Akitumia kanuni ya, ‘usibadili kikosi cha ushindi’, kocha Patrick Aussems, alihifadhi kikosi kile kile kilichoanza na kushinda dhidi ya Al Ahly.

Lakini tatizo kubwa la Simba katika siku za hivi karibuni, ni kiwango duni cha Clatous Chama. Mara zote, Aussems amekuwa akimtumia mzambia huyo kama ubongo wa timu lakini katika mchezo wa leo, hakuweza kufanya ubunifu wowote.

Yawezekana ni kutokana na uimara wa Feisal na labda Ninja, au udhaifu wake mwenyewe. Kuna wakati alikuwa akipoteza mipira kirahisi na wakati mwingine akipiga pasi za pembeni au za nyuma.

Kama ilivyokuwa Kongo dhidi ya AS Vita, Simba ilikuwa na umiliki mzuri wa mpira lakini hawakujua waufanyie nini. Utatu wa kiungo wa Mkude, Kotei na Chama, huwa na faida kubwa pale Chama anapokuwa kwenye ubora wake kwa sababu ataweza kushuka kuchukua mipira na kuipandisha timu.

Kuingia kwa Dilunga kukasaidia kuongeza mipira mbele na kuichanganya safu ya ulinzi ya Yanga.

BOCCO NI MAKELELE WA WASHAMBULIAJI

Mara zote Bocco hulaumiwa kwa nafasi anazopoteza lakini ni vema pia kumpongeza kwa kuwasaidia wenzake.

Harakati zake kwenye eneo la hatari la wapinzani, huwafanya washambuliaji wenzake kupata uhuru wa kujipanga. Bao dhidi ya Al Ahly na hili dhidi ya Yanga, ni ushahidi.

NAHODHA ALIPOTEA

Wakati wa kupiga picha ya pamoja kati ya manahodha na waamuzi, nahodha wa Simba, John Bocco hakuonekana. Haikufahamika nini kilitokea.

KAGERE NA FUMBO LA UMRI

Mfungaji wa bao la ushindi, Meddie Kagere, alisema baada ya mchezo, ‘intelligence is better than age’, yaani akili ni bora kuliko umri. Sijui alimaanisha nini!?

©Zaka Zakazi

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here