Home Kimataifa Simba yaandika historia mpya ligi ya mabingwa Afrika

Simba yaandika historia mpya ligi ya mabingwa Afrika

7558
0

Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1994, klabu ya Tanzania inafika hatua ya robo fainali ya Ubingwa wa Afrika (Klabu Bingwa/Ligi ya Mabingwa). Timu ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa Simba, lakini ilitolewa na Nkana FC kwa jumla ya mabao 4-3.

Kuna watu huhesabia mafanikio ya Yanga 1998, na Simba 2003 kama robo fainali. Lakini ukweli hauko hivyo. Katika miaka hiyo, timu hizi zilifuzu kwa hatua ya makundi na wala siyo robo fainali.

KWANINI?

Mashindano haya yalianza mwaka 1965 yakiitwa Klabu Bingwa Afrika na yaliendeshwa kwa mtindo wa mtoano kuanzia raundi ya kwanza hadi fainali.

Mwaka 1997, CAF ilibadilisha mfumo na kuanzisha hatua ya makundi. Hapo ndipo jina la mashindano likabadilika kutoka Klabu Bingwa na kuwa Ligi ya Mabingwa.

Kulikuwa na makundi mawili ya timu nne nne. Mfumo huu mpya ulifuta hatua za robo fainali na nusu fainali na kukawa na makundi mawili ambapo vinara wa kila kundi walitinga moja kwa moja fainali.

MKANGANYIKO

Mfumo huu haukueleweka kwa wengi. Kwa mfano, mwaka 1998, Yanga ilipofuzu hatua ya makundi, Katibu Mkuu wa FAT, Ismail Aden Rage, alinukuliwa akisema kwamba Yanga wametinga nusu fainali. Yawezekana alikuwa hajaulewa vizuri mfumo mpya.

Mwaka 2001, CAF wakairudisha hatua moja ya nusu fainali, iliyofutwa 1996. Timu mbili za juu kutoka kila kundi zilifuzu kwa nusu fainali…na washindi kutinga fainali.

Mwaka 2017, CAF wakaongeza idadi ya timu za kufuzu hatua ya makundi kutoka 8 hadi 16 na kuongeza makundi kutoka mawili hadi manne.

Hapo ndipo hatua ya robo fainali iliporudishwa tena tangu iwepo mara ya mwisho 1996.

Msimu huu, 2018/19, Simba imetinga robo fainali…ni mara ya kwanza kwa timu ya Tanzania tangu 1994!

© Zaka Zakazi

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here