Home Kitaifa SALIM MBONDE: KWA SASA NIPO HURU KUFANYA MAZUNGUMZO NA TIMU YOYOTE

SALIM MBONDE: KWA SASA NIPO HURU KUFANYA MAZUNGUMZO NA TIMU YOYOTE

2155
0
Salim Mbonde-Beki Mtibwa Sugar
Salim Mbonde-Beki Mtibwa Sugar
Salim Mbonde-Beki Mtibwa Sugar

Na Baraka Mbolembole

Siku 50 kuelekea kikomo cha mkataba wake na klabu ya Mtibwa Sugar, mlinzi wa kati na nahodha wa timu hiyo bingwa mara mbili wa zamani wa Tanzania Bara, Salim Mbonde ameweka wazi kuwa anaweza kujiunga na klabu yoyote kubwa nchini baada ya misimu mitatu ya kujijenga na kujiendeleza chini ya kocha Mecky Mexime.

Mbonde alijiunga na Mtibwa kama mchezaji wa timu B misimu mitatu iliyopita akitokea JKT Oljoro ya Arusha tayari ameiwakilisha timu ya Taifa ya Tanzania ( Taifa Stars) katika michezo minne, huku pia akicheza mara mbili katika timu ya bara (Kilimanjaro Stars).

Mchezaji huyo wa nafasi ya beki ya kati hajaitwa katika timu ya taifa ambayo itacheza na Chad katika mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2017.

Nimefanya mahojiano na mlinzi huyu mwenye umbo kubwa, pamoja na kuzungumzia mkataba wake wa sasa na hatma katika timu yake, Mbonde amezungumzia pia namna alivyowatosa Simba SC misimu miwili iliyopita baada ya timu hiyo kutaka kumuhamisha kinyume na utaratibu akiwa na mkataba na Mtibwa.

Zaidi ungana nami katika mahojiano haya…

www.shaffihdauda.co.tz: Mkataba wako bado una muda gani hapo Mtibwa?

Salim Mbonde: Nimebakisha siku 50

www.shaffihdauda.co.tzSiku 50 kabla ya kumalizika kwa mkataba wako na Mtibwa, je, kuna mazungumzo yoyote yanaendelea na waajiri wako wa sasa?

Salim Mbonde: Tulishazungumza isipokuwa nilichowaambia kwa sasa waniache nivumilie jinsi gani ya kuisaidia timu imalize katika nafasi nne za juu baada ya hapo ndiyo tufanye mazungumzo kuhusiana na  mkataba mpya.

www.shaffihdauda.co.tz: Katika vipindi vinne vilivyopita vya usajili, timu za Yanga SC, Simba SC na Azam FC walijaribu kukusaini ukiwa na mkataba hapo Mtibwa, sasa unaelekea kuwa huru, je, ni wakati wako sahihi sasa kujiunga na timu mojawapo? Naimani umekomaa kiushindani kwa sasa

Salim Mbonde: Kweli kipindi cha nyuma timu zote hizo zilinihitaji lakini nilikataa kwa kuwa nilikuwa bado sijawa na uzoefu pia kukomaa kiushindani kama unavyosema ila kwa sasa naamini nina uzoefu na nina ukomavu wa kwenda kushindana ktk timu hizo na ndiyo nia yangu msimu ujao nitoke hapa nilipo niende nikapate changamoto zingine kwingine.

www.shaffihdauda.co.tz: Mimi nafahamu kwamba makamu wa rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ aliwahi kukufuata na kukuomba usaini fomu za kujiunga na Simba wakati una mkataba na Mtibwa. Ulikataa na kutoa taarifa kwa uongozi wa timu yako. Ulipata wapi ujasiri wa kuikataa Simba wakati ule 2014.?

Salim Mbonde: Nisingeweza kufanya vile kwakuwa bado nilikuwa mali ya mtibwa na nisingewashirikisha viongozi wangu lisingekuwa jambo jema kwani walinipokea vizuri nilipoingia.

www.shaffihdauda.co.tz: Hongera kwa uamuzi mzuri, sasa wakija uko tayari kujiunga nao mkifikia makubaliano?

Salim Mbonde: Kwa sasa nipo huru kufanya mazungumzo na timu yoyote ile kutokana na mkataba wangu unavyosema so hilo hailwezi kushindikana kulizungumzia endapo wakija.

www.shaffihdauda.co.tz: Umewahi kucheza na Faustino Lukoo au kumuona akicheza?

Salim Mbonde: Sikuwahi kucheza nae timu moja ila  nishamuona akicheza.

www.shaffihdauda.co.tz: Kumuona tu Lukoo akicheza kwako ni bahati, ungenufaika zaidi kama ungepata bahati ya kucheza naye hata katika mechi ya ‘Ndondo,’ sasa unacheza na Dickson Daudi hapo Mtibwa imani yangu utakuwa umejifunza vingi kutoka kwa Dicky, anavyocheza Dicky si tofauti sana na alivyokuwa Lukoo, umejifunza nini toka kwa Dicky kama mlinzi wa kati?

Salim Mbonde: Nimejifunza mengi sana kwa Dicky kama mlinzi pia kama kaka yangu ukiangalia mimi bado kijana najifunza kila kukicha na ndiyo maana nipo hapa kutokana na michango yao kamwe sitoweza kuwasahau.

www.shaffihdauda.co.tz: Una umbo zuri kama mlinzi wa kati, unacheza vizuri mipira ya juu, una uwezo wa kujipanga na kuwaongoza wenzako katika ngome. Kitu ambacho nakushauri ni wewe kuendelea kujifunza kutoka kwa wachezaji wazuri waliopita na waliopo, mtazame Dicky jinsi anavyokuwa mtulivu na kukaba kwa uwakini mkubwa wakati timu inaposhambuliwa.

Huwa hapotezi uwezo wake wa kawaida kama mlinzi wa kati, wala haoneshi kuchanganyikiwa. Lukoo kama ilivyo kwa Dicky na wewe hakuwa na kasi ya kutisha lakini alikuwa na uwezo wa kukimbia kila katika eneo la hatari na kucheza mpira.

Nimekuona mara mbili ukijifunga ukichezea timu za taifa (Taifa Stars-katika COSAFA, na Kilimanjaro Stars-katika Challenge), mlinzi yeyote anaweza kujifunga lakini nadhani unapaswa kufanya jitahada zaidi ili uwe mwepesi na kuwahi katika matukio. Unafanya jitahada gani kuwa mwepesi zaidi ya ulivyo sasa ukiwa uwanjani?

Salim Mbonde: Wepesi ni mazoezi ya sprints na miruko

www.shaffihdauda.co.tz:  Nini udhaifu wako na unafanya jitihada gani kukabiliana nao?

Salim Mbonde: Huwezi kuwa mkamilifu 100% lakini hauna budi kupunguza mapungufu, mchezaji mzuri ni yule anayefanyia kazi mapungufu yake, hivyo hata mimi yapo mapungufu yangu na kila siku najitahidi kujirekebisha.

www.shaffihdauda.co.tz: Kama yapi?

Salim Mbonde: Siwezi kuyaweka mapungufu yangu hadharani isipokuwa yapo kwani hakuna aliyekamilika

www.shaffihdauda.co.tz: Sifa gani unazo kama mchezaji wa nafasi ya ulinzi?

Salim Mbonde: Nina urefu ambao naitumia vizuri kwenye mipira ya juu pia nina akili na nguvu za kuweza kushindana.

www.shaffihdauda.co.tz: Asante sana kaka kwa mda wako.

Salim Mbonde: Asante pia.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here