Home Kimataifa Monaco vs Nice ni vita ya watoto wa Wenger Ufaransa

Monaco vs Nice ni vita ya watoto wa Wenger Ufaransa

3006
0

Kwa wale waliowahi kuiona Arsenal katika ubora wake miaka ya 1996 mpaka 2004 kwenye kikele cha kikosi kikichopachikwa jina la ‘The invisible’ baada ya kucheza msimu mzima wakichukua ubingwa wa EPL bila kupoteza.

Majina ya Thierry Henry na Patrick Vieira hayawezi kuwa mageni, wawili hawa hawakuishia Arsenal tu bali walikiwasha vilivyo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa ambayo ilikuwa kwenye ubora wake kwenye miaka ya 1998 mpaka 2000 walipotwaa ubingwa wa dunia na Ulaya.

Vieira alikuwa kiungo mwenye kila kitu unaweza kwenda mbali zaidi na kusema alikuwa toleo la awali la huyu Pogba anayeonekana leo.

Henry alianza maisha kama winga kabla ya kubadilishwa kuwa mshambuliaji hatari aliyekuja kuvunja rekodi na kuweka rekodi za ufungaji kwenye historia ya washika bunduki wa Arsenal.

Wawili hawa walikuwa katikati ya Mapinduzi ya kifaransa yaliyoletwa London yakitokea Japan chini ya Le Professor Arsene Wenger ambaye aliwasajili toka Italia. Vieira akisajiliwa toka AC Milan mwaka 1996 na Henry akifatia miaka mitatu baadaye akitokea Juventus ambako hakuwahi kuonesha ubora wake.

Siku, wiki, miezi na miaka imepita, wawili hawa walistaafu kwa nyakai tofauti na kila mmoja kwa nafasi na mazingira yake tofauti na waliamua kuingia kwenye tasnia ya ukocha mahali ambako walilazimika kuanza moja kwa moja katika ulimwengu ambao ulikuwa tofauti na ile sayari ya mafanikio waliyowahi kuishi wakiwa Arsenal na vijogoo wa Ufaransa.

Henry alianza kwenye vikosi vya wachezaji wenye umri chini ya miaka 18 ambako alipewa fursa na mzee Wenger hata hivyo nafasi yake kweye vikosi hivi haukudumu. Henry ambaye pia alikuwa anafanya kazi kama mchambuzi kwenye mechi za EPL kwenye kituo cha television cha Sky alijikuta akimkera mzee wake pale alipoponda mbinu zake katika moja ya mechi ambazo alipangwa studio.

Wenger akiwa amefura kwa hasira na ‘kisununu’ alimtaka Henry achague moja, ukocha wa vikosi vya makinda wa Arsenal au uchambuzi kwenye studio za Sky na Henry aliamua kuachana na Arsenal na baadaye alijiunga na Roberto Martinez kama kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Ubelgiji ‘Mashetani Wekundu’.

Kwa Vieira ambaye alistaafia Manchester City alianza maisha ya ukocha kwenye timu za vijana za mabingwa hao wa England na ulipowadia wasaa alipandishwa kwenda kuifundisha timu ya wakubwa ya New York City FC timu inayomilikiwa kwenye timu za Manchester City.

Huku wakiwa wanaamini wameiva na wako tayari kuingia misituni kupambana, Henry na Vieira kwa mazingira yasiyofanana msimu huu wamejikuta wakiwa kwenye ligi ya Ufaransa na saa chache zijazo wanakutana uso kwa uso katika mechi ambayo kama utatamani kumuona Arsene Wenger akiwa mwamuzi wa kati akisaidiwa na washika vibendera ambao labda wangeweza kuwa Dennis Bergkamp na David Seaman.

Vieira aliamua kuchukua mikoba kwenye klabu ya Nice aliyoanzanayo msimu huku Henry akikabidhiwa kikosi cha Monaco katikati ya msimu baada ya kufukuzwa kwa Leonardo Jardim.

Ugumu wa Henry na Vieira hauko katika uchanga wao katika tasnia ya ukocha pekee bali hata changamoto ya ubaguzi wa rangi inayofichwa kwenye soka kwa tasnia ya ukocha.

Wanafunzi hawa wa Professor Wenger wanakutana katika mazingira ambayo jukumu lao kubwa ni kuepuka kushuka daraja tofauti ya mbingu na ardhi na mataji waliyokuwa wakiwania katika zama za Arsenal na Ufaransa.

Urafiki hautakuwa sehemu ambapo pointi tatu muhimu ndio zawadi kuu, tayari tumeshuhudia wachezaji wa zamani kama Frank Lampard, Steven Gerrard pamoja na John Terry kwenye klabu za Derby County, Rangers na Aston Villa ambapo Terry ni kocha msaidizi.

Vieira na Henry itakuwa filamu nzuri ya kihistoria kwenye soka la Ufaransa na kama wawili hawa watafika mbali haitakuwa ndoto ya kushangaza pale ambapo watakuja kukutana tena kwenye jukwaa kubwa zaidi la ligi ya Ufaransa mathalan EPL, Champions League hata kombe la dunia kama si la Ulaya katika hali itakayompa faraja kubwa kocha aliyewaongoza kupata mafanikio Arsene Wenger.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here