Home Kimataifa Messi anampenda Neymar, Neymar anapenda ufalme

Messi anampenda Neymar, Neymar anapenda ufalme

5760
0

Hii habari ni kama imechanganya wengi. Kwa sababu wakati Neymar anaondoka kuna walioamini kuwa alifuata marashi ya vikoi vya waarabu, lakini pia kuna kundi liliamini alikwepa kivuli cha Lapurga The King.

Wakati Neymar anatoka Santos kuja Barcelona tayari alikuwa staa mkubwa duniani. Alikuwa anafahamika duniani kuliko hata raisi wake akiwa bado kijana mdogo na mbaya zaidi alitokea tu klabu ambayo haina uwanda mkubwa wa mashabiki duniani.

Lakini mambo hayakwenda sawa kwake pale Camp Nou. Sidhani kama unafuatilia mpira halafu hujui tabia za Neymar. Tabia zake zilimfanya ajione mpweke Barca. Alitaka kujiheshimisha kabla hajaheshimiwa.

Ni Messi pekee aliyechagua kuwa rafiki wa nyota huyu mwenye asili ya utukutu wa kujisikia. Messi hakujali maringo ya Neymar wala mienendo yake ya kunata.

Yawezekana Messi nae alikuwa shabiki wa Neymar kutokana na uwezo wake. Mwisho wa siku hata uwe star vipi lazima atatokea bwana mdogo mwenye kipaji au kitu alichokuzidi akukoshe. Labda tuseme Messi alivutiwa na Neymar.

“Wengi hawajui uhusiano wangu na Messi wanaongea tu. Leo nitaweka wazi ukweli wangu kuhusu mchezaji huyu bora kabisa duniani” Neymar.

Kwani Neymar kuna uhusiano gani ambao hatuujui kati yake na Messi?

“Messi ni mtu wa ajabu sana, alinisaidia mno nilipokuwa Barcelona. Wakati nakutana nae mara ya kwanza, alinishika mkono akaniambia usiogope.” Neymar.

Kwanini Messi alimwambia Neymar asiogope? Inaonekana kuna sababu kubwa na ya msingi ambayo Messi aliisoma kutoka kwenye uso wa Neymar

“Aliniambia nitakuwa mchezaji bora kama nilivyokuwa Santos. Alinisihi sana nisiogope chochote niwe na furaha kama hapo awali. Akanihakikishia kuwa atanisaidia kwa namna yeyote ile” Neymar.

Yawezekana kwenye uso wa Neymar Messi aliona uchu wa kuwa mchezaji mkubwa (Mfalme). Messi alitambua kuwa Neymar atamhofia yeye.

Wakati Neymar anatoka Santos tayari alikuwa mchezaji nyota. Labda hofu yake kubwa ilikuwa kupoteza ustaa wake. Yamkini Neymar alitamani kupita viatu vya akina Ronaldinho ili nae awe mfalme Camp Nou.


Neymar 2013:

Alihusika kwenye magoli 65

34 Magoli
30 assists


“Messi aliniambia usiwe na hofu. Nipo kwa ajili yako. Pambana. Wala usitishwe kabisa na mimi. Nipo hapa kwa ajili yako na nitakusadia kufikia malengo yako” Neymar.

Bila shaka Messi alimpa Neymar ahadi kubwa ambayo nyuma ya pazia ilikuwa ngumu kuitimiza kwa wakati. Swali ni je Messi alitaka kumsaidia nini Neymar? Na Neymar alitaka nini?

Mwisho utagundua ahadi ya Messi ilikuwa kumwachia utawala wake hapo baadae. Ndio, hakuna taifa linaloongozwa na wafalme wawili. Lakini Neymar nae saa yake inakwenda kasi huku kipaji cha Messi kikizidi kuwa kikali kama mvinyo uliokaa mda mrefu.

Messi alihakikisha kuwa Neymar ana furaha. Lakini wakati Messi anamfanya Neymar kuwa bora, Messi nae ubora wake hauoneshi kufifia.

Nadhani kwa ujumbe huu wa Neymar tumepata jibu kuwa Neymar alimkimbia Messi kwa sababu ahadi zake zingechukua muda ambao bado Neymar hakuwa na uhakika nao. Kama kweli Neymar hakumkimbia Messi kama baba yake anavyodhania, je kama Messi alimsaidia Neymar kiasi hicho na alimpa ahadi za kumsaidia kilichomfanya akimbilie kukwaruzana na akina Cavani kisa penati nini?

Neymar alitaka ufalme, waarabu wakamuongezea na dinari za kutosha.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here