Home Ligi EPL Hivi Sarri hajui kama Kante ni kiungo mkabaji bora duniani?

Hivi Sarri hajui kama Kante ni kiungo mkabaji bora duniani?

5871
0

Na Patrick Admila


Sina elimu kubwa ya soka kumzidi Sarri, lakini kumweka Fabregas kama kiungo mlinzi halafu Kante asimame nyuma ya mshambuliaji kunanifanya niwe na mashaka na sigara anazovuta Sarri” Priva Abiud (Privaldinho)


Katika soka, kuna baadhi ya makocha wana mawazo na wengine wana mbinu. Inaonekana Kocha wa Chelsea Maurizio Sarri, anaamini wazo lake la kucheza soka la kumiliki mpira na sio mbinu za namna gani niwatumie wachezaji wangu ili waendane na mfumo wangu.

Inaleta ugumu kuamini kwamba Kiungo wake Ngolo Kante ni bora akicheza kama kiungo mchezeshaji kuliko kiungo mzuiaji/mkabaji. Hili lipo wazi Kante ameuthibitisha ulimwengu wa soka kwamba yeye ni bora akipewa majukumu ya kuwalinda mabeki. Hivi kweli miaka ijayo nikimwambia mwanangu kuwa Kante alitumika kama namba 10 si ataniona baba yake sina akili?Atanidharau anaweza kunikebehi kuwa baba sikuwa nafuatilia mpira.

Kila mtu anajua Kante alishinda taji la ligi akiwa kama namba 6 pale Lecester, akiwa anacheza nafasi ile ile akatwaa ubingwa na Chelsea tena akiwa mchezaji bora wa mwaka. Ni Kante huyu huyu aliyekuwa mhimili mkubwa wa Ufaransa iliyobeba Kombe la Duni akiwa na timu ya Taifa ya Ufaransa Dunia kule Urusi.

Deschamps na Ranieri wote hawakuona ubora wa kante dimba la juu ina maana Sarri ameona nini kwa Kante? Kuna wakati nawaza vibaya sana kuhusu zile fegi zake isije ikawa utata unaanzia pale.

Antonio Conte na ujanja wake wote hakuwahi kumuona Kante bora katika eneo la kukata keki.

Wengine wanaamini kwamba, wakati Chelsea haina mpira, Kante anarudi haraka kusaidiana na Jorginho. Kimbinu hapo unafeli. Kwanza unamfanya Kante aonekane mzururaji au mwana riadha. Kimantiki pia ukikutana na timu ambayo inakulazimisha ufanye makosa, unaruhusu magoli ya kizembe hasa kwa Kaunta atak.

Jorginho ni mpigaji wa pasi mzuri sana ila hana ujasiri mkubwa wa kupora mipira kwa adui. Nimekuwa nikiangalia mechi kadhaa za Chelsea, naona bado umuhimu wa Kante kwenye eneo la ukabaji. Sarri anaamini soka la kumiliki mpira ambalo halina mbinu ndani yake. Mwisho wa siku wanasubiri Hazard abadilishe matokeo. Kikichobaki wapige pasi zaidi ya 1000 halafu ubunifu sifuri kwenye robo ya eneo la audi.

Najua katika Klabu ya Chelsea kuna mapungufu madogomadogo kwenye eneo la ulinzi. Nawaona David Luiz, Marcos Alonso wameimarika sana kuipandisha sana timu kuliko kuongeza nguvu kwenye ulinzi.

Kama Sarri ana lengo la kupambana na makocha wengine kimbinu zaidi basi anatakiwa abadilike maana ni rahisi kuelewa soka lake la kumiliki mpira. Kikawaida tunasema mwalimu amekuwa na falsafa ambazo hazina mwelekeo sahihi wa matokeo chanya.

Kante anatakiwa aendelee kuwa kiungo mkabaji ili hata walio mbele yake wasiwe na hofu kurudi nyuma kipindi timu haina mpira.

Naangalia mfano kwa Pep Guardiola. Anajua kabisa ili Silva, Gundogan, Bernado Silva wawe huru zaidi lazima Fernandinho awepo. Pep anajua umuhimu wa Fernandinho kwenye eneo la kiungo mkabaji. Akikosekana basi lazima awe na mbinu mbadala ili timu iendelee kuwa kwenye uwanda mpana wa kujilinda.

Kwa Maurizio Sarri yeye anaamini Jorginho yupo sehemu sahihi na Kante yuko kwenye sehemu sahihi. Ni kipindi kifupi tangu Sarri awasili Chelsea na wengine wanaweza kuona namhukumu mapema lakini naona Ligi inapoelekea. Kama huna mbinu huwezi kushinda taji. Lazima ubadilike kadri mambo yanavyoenda.

Na Patrick Admila

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here