Home Kitaifa Serikali yaahidi kuboresha mashindano ya Golf Utalii Karibu Kusini

Serikali yaahidi kuboresha mashindano ya Golf Utalii Karibu Kusini

6731
0
SHARE
Washiriki kutoka vilabu mbalimbali vya gofu nchini wakiendelea kushindana kwenye mashindano hayo.

WAKATI mashindano ya golf ya Utalii Karibu Kusini Mufindi Golf Challenge 2018 yakihitimishwa leo kwenye Viwanja vya Golf vya Unilever wilayani Mufindi, Mkoani Iringa serikali imeahidi kuendelea kuyaboresha mashindano  hayo ili yatumike kwa ufanisi zaidi kutangaza vivutio vya Utalii katika kanda za Nyanda za Juu Kusini.

Akizungumza kwenye viwanja hivyo, Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Utalii Wizara ya Mali Asili na Utalii, Bw Deogratius Mdamu alisema uamuzi wa Serikali kupitia ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa kutumia mashindano hayo kutangaza Utalii wa Nyanda za Juu Kusini umeonesha mafanikio licha ya kuwa mashindano hayo yanafanyika mara ya kwanza baada ya kupita miongo kadhaa.

Washiriki kutoka vilabu mbalimbali vya gofu nchini wakiendelea kushindana kwenye mashindano hayo.

“Lengo hasa nikuona ndani ya muda mfupi ujao mashindano haya yanakuwa makubwa si tu hapa nchini bali pia nje ya nchi ili tuweze kuvutia washiriki wengi hasa kutoka nje ya nchi tukiamini ujio wao hapa Mufindi utakuwa na tija si kimichezo bali pia kiutalii na kiuchumi,’’ alisema Mdamu.

Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mashindano hayo wamesema uwepo wa mashindano hayo utatumika kikamilifu kutangaza fursa na vivutio vya Utalii vinavyopatikana katika ukanda huo.  Bw Yeckonia Chaula ambaye ni mchezaji mwandamizi wa golf kutoka klabu ya Golf ya Mufindi alisema:

“Naipongeza sana serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa kuamua kutumia mchezo huu kutangaza vivutio vya Utalii katika Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini na kwa kweli dalili za mafanikio zimeanza kuonekana mapema kwa sababu licha ya mashindano haya kufanyika mara ya kwanza baada ya miaka mingi sana lakini yamevutia washiriki kutoka klabu zote za mchezo huu hapa nchini ikiwemo Dar es Salaam, Morogoro, Arusha na Mufindi.’’

Washiriki kutoka vilabu mbalimbali vya gofu nchini wakiendelea kushindana kwenye mashindano hayo.

Naye Mratibu wa Mashindano hayo kutoka kampuni ya Capital Plus International (CPI) Bw Clement Mshana aliwashukuru sana washiriki hao kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mashindano hayo huku akiahidi kutumia maoni ya washiriki katika kuboresha zaidi mashindano hayo mwakani.

“Pamoja na kuwashukuru washiriki hususani Klabu ya Golf ya Lugalo ambao wameshiriki kwa wingi kwenye mashindano haya kipekee niwashukuru kampuni ya Chai ya Unilever kwa mapokezi mazuri pamoja na maandalizi ya uwanja,’’ alisema.

Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Utalii Wizara ya Mali Asili na Utalii, Bw Deogratius Mdamu (katikati) akikagua Uwanja wa Golf wa Unilever uliopo wilayani Mufindi mkoani Iringa ambapo mashindano hayo yanaendelea. Wengine ni pamoja na Afisa Utalii Mkoa wa Iringa Bi Hawa Mwachaga (kushoto) pamoja na Mratibu wa mashindano hayo kutoka kampuni ya Capital Plus International, Bw Clement Mshana.

Mashindano hayo ya siku tatu yameandaliwa na serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na yamehusisha washiriki zaidi ya 80 wakiwemo wachezaji wa kulipwa yaani ‘Professionals’ na washiriki wa kawaida yaani ‘Amateurs’  na yanatarajiwa kuhitimishwa leo ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Tamisemi, Bw Joseph Kakunda.

Waandaaji wa mashindano hayo wakiwa kwenye picha ya pamoja

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here