Home Kimataifa Uchambuzi wa kina wa wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa FIFA 2017/2018

Uchambuzi wa kina wa wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa FIFA 2017/2018

14385
1
SHARE

Shirikisho la soka duniani FIFA limetangaza orodha ya wachezaji 10 walioko katika kinyang’anyiro cha mchezaji bora wa kiume wa Fifa kwa msimu uliopita huku mshambuliaji wa Brazil Neymar akiwa hayupo kwenye orodha ya wachezaji 10 waliotajwa.

Mabingwa wa dunia Ufaransa wanaongoza kuwa na wachezaji wengi katika orodha hii huku katika nyanja ya vilabu mabingwa wa Champions League Real Madrid wakiongoza kutoa wachezaji wengi katika tuzo hizo zitakazofanyika mwezi wa tisa tarehe 24.

Orodha hii inaonekana wazi inatokana na mafanikio yaliyopatikana kupitia Champions League na kombe la dunia lakini pia mafanikio binafsi, sii vibaya tukaona mchezaji mmoja mmoja katika orodha hii kile alichokipata msimu uliopita.

1. Cristiano Ronaldo(Ureno/Real Madrid).

Mchango timu ya taifa, Ronaldo amekuwa na mchango mkubwa katika timu ya taifa ya Ureno alikuwa kinara kuivusha kuelekea kombe la dunia Urusi, lakini kombe la dunia nako akapiga mashuti 21 na kuifungia Ureno mabao 4 lakini wakaondolewa na Uruguay hatua ya 16 bora.

Mchango kwenye klabu, Cr7 alifunga mabao 15 katika michuano iliyopita Champions League akaibuka kinara wa ufungaji na kuisaidia Madrid kutwaa kwa mara ya tatu Champions League, kiujumla Ronaldo amefunga mabao 44 msimu uliopita katika mechi 44 na assists 8.

2. Lionel Messi(Argentina/Barcelona)

Mchango timu ya taifa, kama unakumbuka Messi alifunga hattrick katika mchezo wa kufudhu kombe la dunia dhidi ya Ecuador matokeo yaliyoipeleka Argentina nchini Urusi, lakini Urusi matokeo hayakuwa ya kuridhisha sana na Messi alikuwa na kiwango kibovu akishuhudia wakiondolewa katika michuano hiyo na Ufaransa.

Mchango kwenye klabu, Messi ndiye kinara wa ufungaji La Liga akiwa na magoli 36 na haya ndio yaliifanya Barca kutwaa La Liga na katika msimu uliopita Messi na Cr7 waligawana ngome, Messi akitawala La Liga huku Cr7 akitawala Champions League.

3.Kylian Mbappe (Ufaransa/PSG).

Mchango kombe la dunia, Mchezaji bora chipukizi wa kombe la dunia 2018 na akaisaidia Ufaransa kubeba kombe hilo, akiwa Urusi Mbappe alivunja rekodi ya Pele ya mchezaji mdogo zaidi kufunga mabao mawili kombe la dunia tangu Pele afanye hivyo 1958, lakini goli lake kwenye fainali likamfanya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kufunga katika fainali kombe la dunia, akamaliza kombe la dunia na mabao 4.

Mchango katika klabu, kama ilivyo kwa timu ya taifa Mbappe pia alikuwa na mchango mkubwa kwa PSG kubeba Ligue 1, alicheza michezo 27 na kwa kushirikiana na Neymar na Cavanni, Mbappe alifanikiwa kuifungia PSG magoli 13.

4.Luka Modric (Croatia/Real Madrid).

Mchango timu ya taifa, kama kuna mchezaji ambaye wananchi wanaongea apewe tuzo apewe tuzo ni Luka, ni injini haswa kwa Wacroatia achilia mbali kama kiongozi uwanjani lakini pamoja na kuwa kiungo amefunga mabao 2.

Mchango kwenye klabu, kama alivyo injini kwa Croatia hii ni injini haswa kwa Real Madrid na kila mipango ya mashambulizi inaanzia kwake, kwa mfano katika La Liga pekeake Modric amepiga pasi timilifu kwa wastani wa 90% msimu uliopita, huku Champions League ikiwa 89%.

5.Harry Kane (Uingereza/Tottenham)

Mchango timu ya taifa, Kane aliwabeba Waingereza mabegani mwake nchini Urusi na kila Muingereza alimuangalia yeye kama ngao yao kupeleka kombe nyumbani, japokuwa waliishia nusu fainali lakini Kane alikuwa kinara wa magoli Urusi akimaliza na magoli 6 japo waliishia nusu fainali.

Mchango katika klabu, alimaliza katika nafasi ya pili ya ufungaji Epl akiwa na mabao 30 katika dakika 3083 alizocheza Epl msimu uliopita huku akipiga mashuti 76 yaliyolenga lango na kuifanya Tot kumaliza nafasi ya 3 ya ligi iliyowapa tiketi ya Champions League msimu ujao.

6.Mo Salah(Egypt/Liverpool).

Mchango timu ya taifa, goli lake pekee vs Congo liliwapa ushindi Misri kwenda kombe la dunia Urusi na hii ikiwa mara ya kwanza kwa Misri tangu mwaka 1990, lakini akashindwa kung’ara Urusi kutokana na majeruhi huku Misri wakiondolewa katika hatua ya makundi bila hata alama moja.

Mchango katika klabu, alikuwa kinara wa mabao Epl akimaliza na mabao 32 na kuisaidia Liverpool kumaliza katika nafasi ya nne ya msimamo wa Epl huku pia akiipeleka Liverpool fainali ya Champions League kwa mara ya kwanza tangu 2004/2005 huku akimaliza michuano hiyo na mabao 10 na assists 4.

7.Kelvin De Bruyne(Ubelgiji/Man City).

Mchango timu ya taifa, Ubelgiji waliishia katika hatua ya nusu fainali kombe la dunia wakiondolewa na Ufaransa lakini bado De Bruyne alionesha ubora wake akifunga goli 1 na akitoa assists 2 na kuisaidi Ubelgiji kumaliza nafasi ya tatu.

Mchango katika klabu, katika mechi 38 ambazo aliichezea Manchester City EPL lifanikiwa kufunga mabao 8 na kutoa assists 16 na Man City kubeba kombe la Epl huku akiwa katika Champions League akitoa assists 4 na kwa ujumla ana assists 21 kwa City msimu uliopita na mabao 13.

8.Eden Hazard(Ubelgiji/Chelsea).

Mchango timu ya taifa, katika kombe la dunia alikuwa kati ya wachezaji waliokuwa na kiwango cha hali ya juu sana akicheza dakika 518 akiishia katika hatua ya nusu fainali akafanikiwa kufunga mabao 3 huku akitoa assists 2.

Mchango katika klabu, japokuwa Chelsea hawakufanikiwa kumaliza katika nafasi nne za juu Epl lakini Chelsea walifanikiwa kubeba kombe la FA na uwezo wa Eden Hazard msimu uliopita umemfanya kuwa lulu kubwa sokoni kwa sasa akifunga mabao 12 katika mechi 36 kwa Chelsea msimu uliopita.

9.Antoine Griezman(Ufaransa/Atletico Madrid).

Mchango timu ya taifa, naye alikuwa nguzo kwa Ufaransa kubeba kombe la dunia pale Urusi, katika michezo 7 ambayo Griezman aliichezea Ufaransa alifanikiwa kufunga mabao 4 pamoja na kutoa assist 2 kwa wachezaji wenzake.

Mchango katika klabu, maisha ya Griezman akiwa na Atletico Madrid msimu uliopita yalitawaliwa na habari nyingi nje ya uwanja lakini ndani ya uwanja walifanikiwa kubeba kombe la Europa huku Griezman akifunga mabao 2 katika fainali vs Marseille, akifunga mabao 19 La Liga na assists 9 huku Atl wakimaliza nafasi ya pili katika ligi.

10.Raphael Varane(Ufaransa/Real Madrid)

Mchango timu ya taifa, wengi wameshangazwa na uwepo wa Varane katika orodha hii, alionesha uwezo mkubwa wa ulinzi kwa Ufaransa katika kombe la dunia na bao moja alilofunga dhidi ya Uruguay lilimpa kitu cha ziada.

Mchango katika klabu, katika maeneo ambayo yalikuwa yanatia mashaka Real Madrid ilikuwa eneo lao la ulinzi lakini mchango mkubwa wa Varane ukaifanya kuwa bora na kubeba kombe la Champions League kwa mara ya tatu mfululizo.

Comments

comments

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here