Home Ligi EPL Sarri mabegani ameibeba Chelsea mkononi ana fegi. Sio mbaya!

Sarri mabegani ameibeba Chelsea mkononi ana fegi. Sio mbaya!

11802
0
SHARE

Kila mshabiki wa Chelsea ametulia tuli. Yaani ukiwauliza kuhusu kocha wao mpya hawana cha kujibu utadhani umewauliza swali la siasa kanisani. Mashabiki wa Arsenal wana uhakika wa kuongea juu ya kocha wao. Hata wale wa Simba wamegugo kocha wao wanatusumbua kweli na kocha wao. Wanatuambia kwa rekodi zake hakuna mtu yupo salama.

Tuachane na hayo twende Italia.

Mwaka 2015 raisi wa Empoli Fabrizio Corsi alitangaza kuwa Maurizio Sarri ataondoka klabuni hapo na kwenda klabu yake ya nyumbani Napoli. Alikwenda kuziba nafasi ya Rafael Benitez aliyekimbilia Real Madrid. Raisi wa Napoli bwana Aureilo De Laurentis alimteua Sarri kuwa mkufunzi wa klabu hiyo maarufu kama Partenopei.

Hakuna mtu aliyejua kama kocha wa klabu ndogo kama Empoli atajiunga timu kubwa kama Napoli. Kama ilivyo kwa sasa upande wa Chelsea baadhi ya mashabiki wanaamini kwamba walihitaji kocha mwenye jina kubwa na mafanikio. Ilikuwa riski kubwa sana kwa Napoli kuziba nafasi ya kocha bora kama Benitez na kocha asiye na uzoefu wowote wa michuano mikubwa.

Vivyo hivyo kwa Chelsea wanaziba pengo la Conte aliyewapa Ubingwa msimu wa kwanza na kombe la FA msimu wa pili. Wanamtimua Conte kisha wanamnunua Sarri ambaye hata kombe la kuku hana. Warombo watakwambia hii ni biashara kichaa.

Jarida la Sky Sport Italia, liliripoti kuwa Sarri alisaini mkataba wa mwaka mmoja wenye thamani ya €1.5 million. Mshahara ule ulikuwa mkubwa sana ukilinganisha na kile alichokuwa akikipata Empoli. Msimu wa 2014-15 katika ligi ya Serie A, Sarri alikuwa akishikilia mkia kuwa kocha anayelipwa mshahara mkubwa €300,000 kwa mwaka. Huo ulikuwa mshahara wa Yahya Toure kwa wiki tu. Napoli wakati huo ilikuwa ikimlipa Benitez €3.5 million.

Msimu wake wa mwisho Napoli aliwatoa kijasho sana Juventus licha ya kupoteza ubingwa huo. Walimaliza wapili alama nne nyuma ya Juventus. Hivyo aliwaziba mdomo wale waliomdharau.

AFANANISHWA NA NGULI ARRIGO SACCHI

Arrigo Sacchi ni nani?

Arrigo Sacchi alizaliwa 1 April 1946. Ni mchezaji na kocha wa zamani kutoka Italia. Amewahi kuiongoza Ac Milan (1987–1991, 1996–1997), akafanikiwa kushinda Serie A msimu wake wa kwanza 1987–88. Akatwaa ubingwa wa (UEFA) European Cups mara mbili mfululizo mwaka 1989 na 1990. Kuanzia mwaka 1991 mpaka 1996, alikuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Italy. Akiwa kama kocha mkuu alishiriki kombe la dunia la mwaka 1994 ambapo walipoteza fainali dhidi ya Brazil kwa matuta.

Sacchi mwenye alikiri kwamba Pep Guardiola na Sarri ni makocha wazuri kizazi cha sasa. Mchezo wa Man City dhidi ya Napoli mwaka jana unasemekana ni moja ya mchezo uliovutia zaidi katika michuano yote ya Uefa mwaka jana.

Wakati wa likizo Pep Guardiola alionekana Milano Marittima, akiwa na Maurizio Sarri akiwa na mkongwe huyu wa AC Milan Arrigo Sacchi. Baada ya Sarri kuondoka Napoli nafasi yake imechukuliwa na aliyewahi kuifundisha Chelsea Carlo Ancleotti

NI FUNDI HASWA!

Alipokuwa Empoli alikuwa na aina 33 ya utengenezaji mashambulizi. Tumeona Unai Emery akiwapa depo wachezaji wa Arsenal lakini Sarri ana mawazo tofauti. Yeye mazoezi yake yanachukua dakika 70-75 tu lakini muda mwingi mazoezi yake wachezaji wanachezea mpira tu na mazoezi yote lazima yarekodiwe kwenye kamera ya juu. Mazoezi ya nguvu kwake anaamini ni mazoezi binafsi ya mchezaji

Sarri akiwa Napoli alimfuata Gonzalo Higuain na kumwambia wewe ni mzembe na mvivu. Wakati huo walikuwa wakijiandaa na msimu mpya. Akwamsihi abadilike ili aweze kutambulika kama mshambuliaji.

Higuain alibadilika akaanza mazoezi ya nguvu na kufanikiwa kupunguza kilo 4. Msimu ulipomalizika Higuain alimaliza msimu ndani ya Serie A kwa kutia kimyani mabao 36 msimu mmoja pekee.

Higuain alipotimkia Juventus, watu wengi wakasema Napoli watapoteana. Sarri akawajibu kwa kumbadilisha Dries Mertens kutoka winga na kumfanya mshambuliaji na akamaliza msimu na mabao 30.

Kisha akawang’arissha wachezaji kama Lorenzo Insigne, Jorginho ambaue amejiunga Sarri Chelsea, pamoja Faouzi Ghoulam, Kalidou Koulibaly na kiungo Sergej anayesakwa kwa kitika cha €160 na klabu ya Real Madrid. Sarri baada ya kumaliza msimu wa 2017 kwa mabao 95 ndani ya msimu mmoja wa Serie A.

Mzee Sacchi alisema “Napoli hawana mchezaji mkubwa sana lakini wanacheza kitimu kuzidi hata zile timu ambazo zina wachezaji wakubwa”

Pep Guardiola akasema “Nikiwa nyumbani napenda kuwatazama sana Napoli wakicheza. Wanavutia zaidi kuliko hata baadhi ya timu kubwa barani ulaya.

AFANYE NINI CHELSEA

Sarri kwa sasa ana kazi kadhaa pale Chelsea. Kwanza kupambaana na hofu ya wachezaji muhimu kuondoka. Hazard na Willian wanawindwa na vilabu vyenye nguvu kubwa ya ushawishi.

Hata hivyo Chelsea ina kikosi imara ambacho kwa aina ya ufundishaji wa Sarri hana haja ya kwenda sokoni. Tayari wamemnasa Joriginho, yupo Kante na Fabregas. Drinkwater na Rose Bakrley wameshindwa kuonesha makali yao labda huu ni muda muafaka wa Sarri kuonesha kuwa yeye ni mkali wa kungarisha nyota zilizofifia mwanga.

Shida ipo kwa Morata. Tokea Morata ajiunge na Chelsea amekuwa akicheza kwa presha kubwa sana. Kama aliweza kumbadilisha Mertens na Higuain sioni kama atakosa namna ya kumtumia Morata na kupata makali yake.

CHANGAMOTO NA MADHAIFU YAKE

Kwa mara ya kwanza Sarri anawekwa kwenye tanuru la moto huku Guardiola, kule Jurgen Klopp na pale Jose Mourinho.
Sarri atahitajika kubadilisha mfumo wake mara kadhaa ili kujua ni upi utakaomfaa. Hata Conte alipokuja EPL mechi yake ya kwanza alifumuliwa na Arsenal mabao matatu. Ilibidi abadikishe mfumo wake wa awali wa 4-1-4-1 na kuhamia 3-4-3 na kufanikiwa kutwaa ubinwa. Mfumo huu ulimsaidia kushinda michezo 12 mfululizo.

Sarri ni mvutaji sigara maaurufu huku akiwa shabiki namba moja wa Charles Bukowski na amekuwa na tabia ya kutokupendelea kuvaa suti muda wote yeye na nguo za michezo tu (traki suti)

“Uzuri wa Sarri ni mwelewa, hana majivuno lakini ukimtibua ana matusi sana,” alisema Koulibaly

Ubaya wake ni lugha tu. Ni mtu ambaye hajali chochote sana hasa pale anapokorofishwa. Hachagui matusi.

Vilabu alivyowahi kufundisha.

Timu alizofundisha
1990–1991 Stia
1991–1993 Faellese
1993–1996 Cavriglia
1996–1998 Antella
1998–1999 Valdema
1999–2000 Tegoleto
2000–2003 Sansovino
2003–2005 Sangiovannese
2005–2006 Pescara
2006–2007 Arezzo
2007 Avellino
2008 Hellas Verona
2008–2009 Perugia
2010 Grosseto
2010–2011 Alessandria
2011–2012 Sorrento
2012–2015 Empoli
2015–2018 Napoli
2018– Chelsea

Makala na Privaldinho (Instagram)

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here