Home Kimataifa Dili la Ronaldo kila mtu amejiwekea kitanzi

Dili la Ronaldo kila mtu amejiwekea kitanzi

12879
0
SHARE

Haya ni mawazo tu haimaanishi kwamba kila kitakachosemwa hapa ni sahihi, Hapana! ni mtazamo tu. Kwa upande mkubwa kila mmoja atafaidika sana lakini pia kwenye kila biashara hasara zipo. Kuna baadhi ya mambo nimewaza tu.

Leo mapema nilikuwa maeneo ya Buguruni. Jamaa mmoja akawa anaongea kwa uchungu sana. Akisema Ronaldo amekunywa maji ya bendera ya Madrid hawezi kuondoka. Nadhani yule jamaa ni mpiga debe. Nina wasiwasi na ufuatiliji wake wa habari.

Nimeona kwenye gazeti la Marca. Gazeti maarufu sana Hispania. Linasema hakuna mchezaji mkubwa kuliko Real Madrid. Ningekuwa na namba za Jose Felix Daiz ambaye ndiye aliyeandika waraka huo pia ningemjibu kwamba Madrid haijawahi kuwa na mchezaji mkubwa kuliko Ronaldo.

Diaz na vibaraka wengine wa Madrid wanataka kufanya usajili wa Ronaldo kwenda Juventus ni sawa na kumtorosha mtoto wa kike na mlango wa uwani. Yaani wanataka kutuaminisha kwamba hawajapoteza sana. Diaz anasema kuwa Ronaldo sio mkubwa kuliko Madrid, sawa nakubali, lakini je nani mkubwa kuliko Ronaldo tokea Madrid ianze? Kimsingi sioni na hakuna na sitegemei siku za hivi karibu tumuone. Wapo wajuaji wataniambia De Stefano.

Mbali na yote haya naona kila mmoja kapoteza licha ya kwamba kila mmoja pia amefaidi kwa kiasi chake.

Florentino Perez amempoteza mchezaji tishio duniani. Cristiano Ronaldo ameondoka ligi bora na klabu kubwa duniani, mwisho Andrea Agnelli anatarajia kumlipa mchezaji mkubwa kiumri mamilioni ya pesa kwa miaka minne hadi miaka 38.

Mimi na Juan Ignacio García-Ochoa tuna mawazo sawa tu. Nawaza kwamba faida aliyowapa Ronaldo Madrid nani mwenye ubavu huo! Hata malaika mbinguni wanafahamu kwamba wakati wanamjadili Ronaldo kuja duniani walijua ametumwa kazi gani. Walifahamu fika hayupo mwanaume mwingine zaidi ya Ronaldo atakayeweza kumlaza Messi na viatu.

Tuanze na Real Madrid:

Los Blancos wamepoteza mabao 50 kwa msimu! Tupo sawa hapo? Ni Zlatan pekee alikuwa na ubavu wa kumaliza ligi na zaidi ya mabao 50. Wengine wote wabahatishaji tu. Ameondoka Raul na Iker Casillas na anayefuata ni Ronaldo anayepita na kuondoa historia ya Alfredo Di Stefano. Ameifungia Real mabao 451 ndani ya miaka 9. Kubeba Uefa 4 na Ballon d’Or 4 sio mchezo. Sawa ana miaka 34 lakini haiondoi mantiki kwamba wamepoteza sana.

Madrid watasajili sio chini ya wachezaji wawili kujaribu kumrithi Ronaldo. Najua Man united ni kielelezo tosha. Kupata mabao 50 kwa mwaka unahitaji wachezaji sio chini ya wawili. Mchezaji mmoja sio chini ya Euro milioni 100. Je hizo Euro Milion 100 walizopewa na Juventus zitawatosha nini? Je mauzo ya jezi waliyopata kwa Ronaldo hapo awali si kwa sasa zaidi ya mashabiki milioni 50 wataelekea Juventus kununua hizo jezi za Ronaldo. Huoni kama wamepoteza? Ni kweli ni ajabu mchezaji wa miaka 33 kununuliwa kwa Euro 100m lakini mashujaa hawana bei. Ronaldo hauziki. Hiyo Hela ni ndogo sana kwa shujaa kama Cr7, “legends are priceless”

Vip kwa Upande wa Cristiano Ronaldo:

Unadhani kwenye akili ya Ronaldo anawaza nini? Bila shaka anajisikia vibaya! Kwanini? Ni kama klabu haithamini kazi yake! Wamemuona kama ganda la miwa. Utamu ushaisha. Kwani Ronaldo amechoka? Jibu ni hapana! Kwanini wasimpe mkataba mpya mnono? Kwanini timu haijapambana kumzuia kuondoka? Iweje azidiwe mshahara na Messi tena karibia mara mbili.

Kwani Florentino Perez hajui Ronaldo ameisaidia vipi klabu kiuchumi? Ina maana wanaogopa kweli kumlipa mkataba wa hata laki 5 kwa wiki?

Ronaldo hajaondoka kwa furaha kabisa. Anaelewa kwamba mafanikio yake yamepatikana nyuma ya msaada wa wachezaji wakubwa sana duniania, Ramos, Marcelo, Kroos, Modric na Casemiro. Hana uhakika wa msaada huo pale Juventus

Ronaldo kama angeendelea kubakia Madrid angefunga mabao mengi sana. Lakini kwa pale Juventus nisiwe mnafiki sidhani kama anaweza kufikia mabao 50. Sijui na sina uhakika. Labda anaweza lakini najiuliza, je wachezaji wa Juventus wataweza kumtumia vyema Ronaldo?

Kuna watu wanaamini ataweza kwa sababu ligi ni rahisi. Sidhani. Umri wake umeenda. Anahitaji muda mwingi wa kupumzika nje na ndani ya uwanjani. Magoli mengi ya Ronaldo yanapatikana kwa upambanaji wake uwanjani kwa kuzingatia ufanisi wa wachezaji wenzake. Kimsingi urahisi wa ligi sio tija kama timu nzima ya Juve haitakubali kucheza chini ya kivuli chake.

Ronaldo anaondoka ligi ambayo alikuwa na uhakika wa kivuli hicho cha wachezaji kusumjudu, anaondoka klabu kubwa duniani. Klabu ambayo alikuwa na uhakika wa mamilioni ya mashabiki kote dunia kumfuatilia. Hatocheza tena El Classico inayovutia zaidi ya watu Billioni moja. Ameondoka kwenye ushindani wake na Messi ambao umempa jina kubwa duniani. Anaenda kuanza maisha mapya kabisa. Umri wake sio rafiki kwa yeye kuanza kujifunza maisha mengine. Kinachomkera zaidi Ronaldo ni pale kwenye geti la Estadio Santiago Bernabeu, ambapo kuna mashabiki waliopigania Modric aongezewe mkataba. Je ni kweli wanapaswa kumuabudu Modric kuliko yeye.

Je Juventus

Mwezi July 10th Ronaldo alisanini mkataba wake na Juventus, Kupitia jarida la The Guardian, kwa masaa 24 jezi 520,000 ziliuzwa zikiwa na jina la Ronaldo.

Ripoti za beIN Sports zinasema juventus waliuza jezi 850,000 kwa mwaka mzima 2016/2017. Mauzo hayo ya jezi kwa masaa 24 yaliipatia klabu kiasi cha $60 million. Lakini kumbuka kwamba Juventus wanapata kiasi cha 10-15 kwenye mauzo ya jezi hivyo Adidas ndio watakaifaidi zaidi. Juventus watapokea kitita cha $9. Kumbe mwisho wa siku mauzo ya jezi sio kitu kama wengi wamavyodhania. Klabu haiuzi jezi. Inapata kiasi kidogo tu.
Lakini ndani ya wiki Juventus wameingia kwenye mtego wa kupoteza karibia robo ha pato lake kwa mwaka la Euro Milioni 112 ili kupata Euro 345 million, ambazo inasemekana kwamba Ronaldo kupitia mikataba yake kwa kipindi cha miaka 12 iliyopita. Je ili wapate hizo 345 wanapaswa kuishi na Ronaldo miaka 12 je inawezekana? Kimahesabu hapo Ronaldo ana miaka miwili tu kwenye ubora wake.

Lakini huoni kama wamefanya riski ya kupoteza kiasi hicho cha pesa kwa kuhisi watafanikiwa? Je itakuwaje akifikisha miaka 36 kwenda mbele? Huoni kama watamlipa mchezaji wa miaka 38 Euro milioni 30 kwa mwaka? Unadhani makampuni yataendelea kumdhamini Ronaldo kiasi ? Muda sio mrefu anakwenda miaka 35? Je mchezaji wa umri huo atacheza mechi 50 kwa mwaka kweli? Unadhani kuna mdhamini atakubali kuingia mkataba mnono na mchezaji ambaye hatacheza mechi 50 kwa mwaka? Anataka kugundua nini?

Kumbuka nimesema hayo ni mawazo tu.. Hakuna maana kwamba kila lisemwalo lazima liwe. Chukulia tu kama ilivyo.

Makala na Privaldinho (Instagram)

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here