Home Kitaifa Picha la usajili Fei Toto, Singida, Yanga

Picha la usajili Fei Toto, Singida, Yanga

15379
0
SHARE

Ukizungumzia usajili wa Bongo kwa sasa Feisal Salum ‘Fei Toto’ ndo ana kiki mitandaoni na kwenye vyombo vya habari. Kwa nini? Kwa sababu ametambulishwa na vilabu viwili tofauti.

Singida United walianza kuachia picha na video za kiungo huyo akionekana anasaini mkataba na kutambulishwa rasmi akiwa amevaa jezi ya klabu hiyo.

Baadaye jioni Yanga ilimtambulisha Fei Toto kwamba ni mchezaji wao rasmi baafa ya kumsainisha mkaba wa miaka mitatu.

Picha lilivyoanza

Singida United walikubaliana na klabu ya JKU kumsajali Feisal kwa ada ya Tsh.25m ambapo alitanguliziwa milioni 18 wakakubaliana atamaliziwa kiasi kilichobaki pindi atakapojiunga na timu.

Simba imetajwa

Baada ya game ya nusu fainali ya Kagame Cup jana (Simba vs JKU) inaelezwa viongizi wa Simba walimchukua Feisal kwa ajili ya kumalizana nae lakini mwisho wa siku dili hilo lilikwama kutokana na Simba kuchelewa kulipa pesa walizokuwa wamekubaliana.

Baadae Yanga waliingilia kati dili hilo lakini walipoelezwa kwamba tayari mchezaji huyo ameshachukua fungu kutoka Singida United, viongozi wa Yanga walijibu wanawamudu Singida United.

Festo Sanga (Mkurugenzi Singida United)

Leo mchana wakati anatangaza kuinasa saini ya Feisal alisema: “Kumekuwa na kelele nyingi kuhusu mchezaji Feisal Salum Abdallah, ni mchezaji ambaye vilabu vingi vikubwa vimekuwa vikipambana kumpata lakini mwenyewe amepima maji ametambua Singida United anaweza kucheza mpira bila presha wala kelele nyingi baadae tunaamini Feisal atakuwa msaada kwenye taifa hili.”

 “Ipo siku huyu Feisal tunaemtaja sasa atakuwa kama Mbwana Samatta tunaamini hivyo kwa sababu ni mchezaji mwenye nidhamu na ameonesha ushupavu kwenye mashindano ya Mapinduzi Cup hadi sisi tukamtamani tunaamini kwa nidhamu aliyonayo ataiendeleza ndani ya Singida United kwa miaka mitatu.”

Mchezaji mwenyewe (Fei Toto)

Video zilizotolewa leo zikimuonesha Fei Toto akisaini mkataba na Singida United, alikiri amemalizana na Singida United na msimu ujao ataanza kuitumikia klabu hiyo.

“Msimu ujao nitaitumikia Singida United kwa nguvu zote na kwa hali zote kwa sababu nimeshamalizana nao kila kitu.”

“Nimejiunga na Singida United si niishie hapa tu  ila nifike timu kubwa mbalimbali, hii iwe kama njia kwa sababu kipaji changu nakiamini pia najifahamu.”

Mwenyekiti wa kamati ya usajili Yanga (Hussein Nyika)

Jioni ya leo July 12, 2018 amemtambulisha Feisal mbele ya wanahabari

“Klabu imeingia mkataba wa miaka mitatu na mchezaji Feisal kutoka klabu ya JKU ya Zanzibar.”

“Yanga ni tumu yenye viongozi wanaotumia ueledi mkubwa, tunajua hata usajili wa Raphael Daudi ulikuwa na matatizo mwanzoni mara amekwenda huku mara kule.”

“Huyu mchezaji (Feisal) bado alikuwa na mkataba na JKU kwa hiyo ilibidi tukamalizane na klabu yake lakini kama kuna klabu imemsaini mchezaji kabla haijamalizana na klabu yake inamaana hilo ni kosa. Sisi tumewafuata viongozi wake wameridhia tumchukue mchezaji.”

Meneja JKU

“Hadi kufikia saa 10:30 jioni leo (Alhamisi July 12, 2018) alikuwa ni mchezaji wa JKU lakini baada ya hapo ni mchezaji halali wa Yanga”-Mohamed Kombo Hamad.”

“Taratibu za mpira duniani kote zinaeleweka mchezaji anakuwa na kwao alikolelewa, hauwezi kumchukua mchezaji ‘from no where’ ukasema huyu ni mchezaji wangu.”

“Kwao ilikuwa ni JKU ndipo alipolelewa na alikuwa na mkataba na timu yetu, Singida walichokifanya ni kosa lakini mimi navishangaa vyama vya mpira majukumu vinayajua vinashindwa kuchukua hatua. Naomba iwe fundisho kwa vilabu ambavyo vitachukua mchezaji mwenye mkataba na kumsaini bila kwenda klabuni kwake.”

Sanga baada ya Feisal kutambulishwa Yanga

“Hili ni jambo dogo ambalo linaendelea kwa mchezaji Feisal Salum ambaye tumemsaini kwa mkataba wa miaka mitatu chini ya mwana sheria na wakala wake na sehemu kubwa ya fedha ameshaichukua.”

Amesaini mkataba ambao unatambulika si mkataba wa awali kama watu wanavyodhani. Tunachoamini amesajiliwa na Singida United hayo yanayotokea kwamba amesajiliwa Yanga ni kuwaweka watanzania njia panda wanashindwa kuelewa kipi ni kipi.”

“Vyombo vya kusimamia mpira vipo na ndio vitakavyoamua hatma ya mchezaji wetu Feisal. Tumeshamalizana na JKU.”

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here