Home World Cup RUS 2018: Bega la mkimbizi halichoki! Mkimbizi Modric amebeba mengi!

RUS 2018: Bega la mkimbizi halichoki! Mkimbizi Modric amebeba mengi!

20985
0
SHARE

Makala tunazoziandika kwenye huu ukurasa mara kadhaa tunalenga kuwainua na kuwatia moyo baadhi ya wachezaji wa changa. Huko Ulaya usidhani kwamba kila mchezaji anatokea maisha mazuri. Wapo ambao wana maisha magumu sana kisoka na kimaisha.

Usikate tamaa wala usiyaonee haya mabega yako.

Luka Modric kwenye mchezo wao dhidi ya Denmark alimfuata kocha wake Zlatko Dalic na kumwambia naenda kupiga tuta. Kocha alishtuka kidogo kwani tayari Modric alikwisha kosa penati kwenye mchezo ule. Huo ndio tunaita ujasiri wa kiume. Usiogope kujitetea au kubeba majukumu yalipo mbele yako kisa tu uliwahi kuanguka.

Kiungo huyu wa Croatia ambaye ndiye nahodha wa Croatia, hatuwezi kusema tusimjumuishe kama nguzo imara kwa Lod Blancos (Real Madrid) baada ya kushinda Champions League mara tatu mfululizo.
Tuna kila sababu ya kutambua mchango wake.

Alijunga na Madrid akitokea Tottenham mwaka 2012 na kujitengenezea jina kubwa zaidi duniani kama kiungo bora aliyekamilika. Ferguson alisuasua kumchukua na Real ilimpata kiulaini. Hili ni moja ya dili kubwa la United kulidharau na ambalo Fergie kama hatojutia basi atakuwa anajitoa akili.

Modric amezaliwa Septemba 9, 1985, jijini Zadar, na alikulia kwenye kijiji cha Modrici. Ni kawaida sana kwa mchezaji mwemye kipaji kutengeneza jina kijijini kwao. Modric alikuwa na kipaji lakini alidharaulika kijijini kwao kutokana na umbo lake. Bila shaka Modric ametengeneza jina kubwa zaidi duniani tofauti na matazamio ya wana kijiji wake hapo awali.

Jina Luka, amelichukua kwa babu yake ambaye aliuwawa na jeshi la Serbia Desemba 1991 wakati wa vita.

Wakati ule wa vita Modric na familia yake walikimbilia jijini Zadar katika hoteli ya Iz.

Hivi majuzi katika hoteli hii ya Zadar watu wengi walikuwa wakimtukana sana Modric kwa kitendo cha kumtetea swahiba wake wa zamani bwana Zdravko Mamic, ambaye anajulikana kama mmoja ya mawakala wenye nguvu kubwa kisoka huko nchini kwao. Wakati huo Mamic alikuwa mkurugenzi wa Dinamo Zagreb klabu ya zamani ya Luka Modric.

Inasemekana Mamic alikuwa na kesi ya rushwa na ukwepaji kodi hasa hasa kwenye sakata la usajili wake wa kwenda Tottenham. Kama Modric angesema ukweli basi Mamic angekwenda jela miaka mitano. Modric mwanzoni alikiri kuna figisu ilitokea wakati wa usajili, lakini yeye hakujua kama kauli yake ingeleta shida.

Mwendesha mashtaka bwana Tonči Petković alimuomba Modric ajieleze upya.

Mahakamani pasikie tu. Unaambiwa Modric alitetemeka kiasi chakupewa muda wa kwenda kupumzika dakika kadhaa arudi tena.

Aliporudi mikono bado ilikuwa inatetemeka, alishindwa kutulia vyema kwenye kiti. Akajitahidi kuongea akasema “hilo…si si si sikuwahi ku ku sema hayo maneno”

Jaji alimkemea sana Modric akimhitaji aseme ukweli kwani yeye ni kiongozi mkubwa wa taifa hilo kisoka. Modric bado hakubadilisha kauli yake na akadanganya alikuwa na mkataba na Mamic tokea 2004 kitu ambacho sio chakweli. Kilichomuokoa Modric ni hiki alichokifanya leo.

Jaji alisema
Modric ni msaada mkubwa kwa taifa, amekuwa na maelewano mazuri na kila mchezaji, tunatambua kuwa kila mchezaji anahitaji kumuona akiwa na kitambaa cha unahodha. Hajawahi kuwa na tatizo lolote na mtu. Amekuwa nembo imara na thabiti kwa taifa. Sina shaka nae. Wala sitaki kuamini kwamba kushindwa kujiamini mbele ya mahakama ni kosa. Haya ni masuala ya kibinadamu”

Alipomtetea Mamic watu wengi walimchukia sana Modric. Mabango yalianza kubandikwa hadi kwenye nyumba ya familia yake wakimuonya kwamba ipo siku atakumbuka ubaya wake. Walimtukana sana na kumuita adui namba moja wa Taifa lao.

Modric asingeweza kukubali mtu aliyemwamini na kumpa nafasi maisha leo akaozee gerezani miaka mitano.

Lakini je najiuliza mpaka sasa yale mabanfo bado yapo?

Baada ya hapo nikagundua kwanini Modric aliomba kapige penati licha ya kwamba alikuwa na presha kubwa. Modric alikuwa na deni kubwa ambalo hata mdaiwa wake alikuwa anamuonea huruma kumdai.

Wangapi walitabiri Croatia kufika nafasi hii? Kufikia hadi tarehe 7 julai yalikuwepo majina makubwa mawili tu kule Kazan (Messi na Ronaldo). Haya majina yalificha kipaji cha Modric kama rangi ya mtu inavyomezwa kwenye kivuli. Hatua ya Robo fainali tu ilikuwa ndoto kwao.

Modric amefika mahali ambapo makocha wa Hajduk hawawezi kuamini kama angefika. Modric akiwa na miaka 10 yeye pamoja na rafiki yake Mario Grgurovic walikwenda kwenye majaribio klabu Hajduk Split. Kocha mkuu wa klabu hiyo na maskauti wakamkatalia Modric kwa kuwa na umbo dogo.

Hata sisi mashabiki tuliimkata Modric kwa kuwa Croatia lilikuwa taifa dogo na tukaamini Brazil, Ujerumani na Argentine na wengine Ubelgiji n.k watafika fainali.

Wakati Modric anakwenda kufanya majaribio alikuwa akiishi kama mkimbizi, Grgurovic alikubaliwa, Modric akatemwa. Modric akarudi Zadar kisha akapata nafasi ya kwenda kujiunga na Zagreb.

“Alipokuwa mdogo alikuwa mpole sana, siwezi kusema eti alifeli majaribo, hapana. Sikuwahi kuona mchezaji mwemye kipaji kama chake. Najua tatizo alikuwa na umbo dogo. Na nachukia kusikia wanafiki wanaposema eti walijua kwamba Modric angekuja kuwa mchezaji bora duniani kipindi yupo Zadar. Huo ni uongo mtupu. Kila mtu alimdharau. Alipokwenda Zagreb ndipo watu wakaanza kumfahamu” Haya ni Maneno ya Grigurovic.

Nikiangalia maneno haya ya huyu swahiba wake nagundua mengi sana. Ni kweli hata hawa Croatia wakati wanaingia kwenye makundi wapo watu tuliamini kwamba hata kwenye kundi atapita kwa tabu. Hakuna mtu aliyetarajia kwamba eti leo Modric ataiduwaza dunia.

Akina Issa Masoud walikuwa kwa Kane wengine mara ooh Neymar noma, sisi wengine ndio kwanza tulikuwa kwa Hazard, akina Msuva, Samatta na Kaseja waliamini Neymar na Jesus watafika mbali. Kwanini tuwe wanafiki. Kama uliamini kwamba Modric atafika steji hii basi ndugu yangu hongera. Una roho ngumu hata ya kuwa mchungaji wa kilokole Somalia.

Anayejua Modric alianzia wapi ni Tomislav Basic, aliyempeleka Modric kwa Mamic na kumpeleka Dinamo mwaka 2002. Mamic namuona kama yule Jaji aliyemsamehe Modric. Mamic hakutishwa sana na umbo la Modric ila aliangalia kipaji chake. Hata yule jaji hakutishwa sana na woga wa Modric wala hakuangalia makosa yake ila aliangalia taifa lao linahitaji nini kwa sasa.”

Modric ni mtoto wa mtaani. Amecheza kila aina ya soka. Liwe la kihuni la kibabe yeye amecheza. Hakujali sana umbo lake. Leo amewaonesha waingereza kwamba shule za soka zina umuhimu lakini soka la mtaani lina faida kubwa. Asilimia 90 ya wachezaji wa Croatia wengi wao hawajatoka kwenye akademi ila ni watoto wa mtaani tu.

Kwanini nasema Modric analijua soka la kibabe. Modric pia amecheza Bosnia kwa mkopo kwenye klabu ya Zrinkski, chini ya kocha Stjepan Deveric. Kocha huyo anasema “Nilipokuwa na Modric katikati, hata nicheze na timu ngumu vipi nilikuwa sina wasiwasi. Modric alicheza kila aina ya mazingira. Mpira wa Bosnia ni wa vurugu. Wachezaji wengi wameathirika na vita vya Balkan lakini Modric alikuwa kivutio cha ziada uwanjani. Hata wapinzani waliona aibu kumchezea rafu.

Alipokuwa Dinamo, alikutana na mwalimu Slaven Bilic. Modric anasema huyo ndiye kocha bora maishani mwake. Alimpa nafasi kubwa sana kwenye kikosi cha U21 kisha baadae kumpa nafasi timu ya wakubwa.

Modric alicheza mchezo wake wa kwanza kwa taifa lake mwezi Machi 2006 dhidi ya Argentina. Alicheza kwa dakika 90 na kumfunika Messi kwa ushindi wa mabao 3-2. Kumbe kipigo cha juzi cha mabao matatu kwa nunge ni marudio tu.

Hao hapo wapo fainali. Davor Sucker mwaka 1998 aliwaduwaza wengi wakati walipoipuekea Croatia hadi nafasi ya nusu fainali ya kombe la dunia kule Ufaransa, baada ya kuifumua Ujerumani mabao matatu kwa nunge. Wakati ule Davo Sucker nae alikuwa akiichezea Real Madrid.

Modric ana mabega madogo lakini kwenye mafanikio makubwa ya Real tusipomtaja Luka Modric tutatenda dhambi kubwa mno.

Usikate tamaa na unachokifanya. Hata kama wachache wanakuelewa. Piga kazi. Wewe fanya kazi. Onesha bidii. Pambanaa

Naitwa Privaldinho pia unaweza kunifollow Instagram

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here