Home Kimataifa CR7 to Juventus: Ni siasa za Mendes kutaka malipo makubwa au kweli...

CR7 to Juventus: Ni siasa za Mendes kutaka malipo makubwa au kweli anaondoka Real Madrid?

15347
1
SHARE

Kila unapofika wakati wa usajili suala la Cristiano Ronaldo kuhusishwa na kuondoka Real Madrid huwa linatawala vichwa vya habari. Kwa muda wa miaka 9 aliyokaa Madrid siku zote amekuwa akihusishwa na kurejea Old Trafford – lakini safari hii kwa mara ya kwanza tetesi za kurejea United hazina nguvu sana, sasa hivi inatajwa Juventus.

Wakala wa Ronaldo, Jorge Mendes amekuwa na tabia ya kutengeneza story za hatma ya mteja wake kila wakati wa usajili unapofika ili kutengeneza nguvu upande wao katika majadiliano ya kuomba mkataba wenye manufaa zaidi kwa CR7 na mara kadhaa amekuwa akitumia watu wake waliopo kwenye vyombo vya habari kuihusisha Manchester United kwa kiasi kikubwa na hufanikiwa kuitikisa Real Madrid na hatimaye lengo lake hutimia kwa Ronaldo kuboreshewa mkataba wake na Los Blancos.

CR7 ana mkataba ambao unamuweka Madrid mpaka 2021 na amekuwa akilipwa mshahara wa £365,000 sawa na zaidi ya billioni 1 kwa kila wiki, lakini baada ya wapinzani wake Neymar kupata mikataba mikubwa ya kulipwa zaidi ya £500,000 kwa kila wiki kwenye vilabu vyao vya PSG na Barca – kulimfanya CR7 na Mendes kuona na wao wanahitaji kuboreshewa mkataba – kutokana na mchango wa Ronaldo katika timu ndani ya uwanja na nje ya uwanja kwenye masuala ya biashara.

Suala hili limekuwepo tangu mwanzoni mwa msimu uliopita, lakini kilio chao kimekuwa kikikutana na masikio mabovu ya Florentino Perez. Jambo lilopelekea CR7 kutoa kauli kadhaa zilionyesha kwamba hana furaha Bernabeu kwa kuona kwamba anadharauliwa. May 2017 baada ya mchezo wa fainali ya UCL alisema kwamba ‘nimekuwa na wakati mzuri na Madrid lakini baada ya muda nitasema nitacheza wapi msimu ujao.’ – Kauli ilipelekea mpaka nahodha Sergio Ramos kusema kwamba CR7 bado muhimu na hawezi kuondoka Bernabeu.

Hata hivyo pamoja na majaribio kadhaa ya kumtikisa Perez aongeze mpunga hayakuzaa matunda kiasi walichotegemea – inaelezwa Ronaldo ana ofa ya maboresho ya mkataba wa Madrid lakini sio kama ambayo yeye na timu yake walivyotaka.

Wiki hii sasa Mendes kupitia mahusiano yake na media tofauti wamekuja na kampeni ya kumpeleka CR7 Juventus – El Chiringuito TV ilianza kuripoti kwamba Ronaldo anaondoka Madrid – anaelekea Juventus ambao kuna kipengele kwenye mkataba wa Ronaldo ambacho kinaziruhusu vilabu vya Serie A tu kupunguziwa bei ya kumnunua kutoka $1 billion mpaka €120m. Wakaendelea kusema kwamba tayari Ronaldo na Mendes wameanza mazungumzo na Juventus kuhakikisha uhamisho huo unafanikiwa. Kituo hiki cha TV kina mahusiano mazuri sana na Mendes pamoja na Rais Florentino Perez.

Marca – gazeti pendwa la Madrid nalo leo limeibeba story hiyo na kuripoti kwamba tayari Juve wamekubali kumpa Cristiano Ronaldo mkataba wa miaka 4 na kumlipa €30m kwa mwaka – €5m zaidi ya anayolipwa kwa sasa Madrid.

Taarifa kutoka Italia

Vyombo vya habari vikubwa nchini Italia kama Gazzetta Dello Sport, Tuttusport na waandishi wakubwa wa michezo wamekaririwa wakisema wamejaribu kuwasiliana na CEO wa Juventus Beppe Marrotta kuhusiana na jambo hili – wamepewa jibu moja ‘No Comment’ – majibu haya yametolewa na kiongozi ambaye mara zote amekuwa mwepesi kukanusha taarifa za tetesi za usajili.

Chombo kingine cha habari nchini humo Premium Media wanaripoti kwamba ni kweli kuna mazungumzo ya dili hilo baada ya Jorge Mendes kuwapa Juventus ofa ya kumsaini Ronaldo na kuwahakikishia kwamba uhamisho huo unawezekana kabla ya klabu hiyo kuanza majadiliano na Madrid.

Kwa wanaomfahamu vizuri Mendes bado wanashindwa kuamini kama ni kweli anataka kumpeleka Ronaldo Juventus na hizi zote ni sarakasi za kupata nguvu kwenye kujadiliana upya na Madrid ambao bado wanamhitaji Ronaldo na kwamba anaitumia tu Juventus kumtikisa Florentino Perez.

Upande mwingine inaelezwa Je Ronaldo ana utayari kuiondoa familia yake jijini Madrid? – mtoto wake Cristiano Jr tayari anasoma, mchumba wake ni mwenyeji wa mji huo na tayari ana CR7 ameshaanzisha makazi katika mji huo – Je atakuwa tayari kuyaacha haya na kwenda Turin kuanzisha kila kitu upya? Je sarakasi za Mendes zitafanikiwa na Perez ataongeza mtonyo? MUDA UTAONGEA

Comments

comments

1 COMMENT

  1. Duuuuh this time Ronaldo ataondoka kwa mimi ninavoona kwa maana. Perez amekuwa akipanga kununua wachezaji kama Neymar, Kane na Hazard kila Ronaldo anapopata ukame kitu ambacho Co kizuri Kwa Ronaldo kama mchezaji hivo ngoja tusubirie muda utaongea

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here