Home Kimataifa Shaffih Dauda, Geoff Lea, waibuka na mchawi wa Afrika kombe la dunia

Shaffih Dauda, Geoff Lea, waibuka na mchawi wa Afrika kombe la dunia

10033
0
SHARE

Timu zote tano zilizokuwa zinaiwakilisha Afrika kwenye fainali za kombe la dunia 2018 zimetupwa nje ya mashindano hayo katika hatua ya makundi ikiwa ni mara ya kwanza tangu jambo hilo lilipotokea mara ya mwisho 1982 (miaka 36 iliyopita.)

Wachambuzi Shaffih Dauda na Geoff Lea kila mmoja ametoa maoni yake kwa nini timu za Afrika zimefanya vibaya lakini wamesema nini kifanyike ili kuhakikisha Afrika inarudi kwenye zama zake.

Shaffih Dauda

Mara zote huwa nasema ukweli lakini mara nyingi huwa naonekana kama nina chuki. Huwa sikurupuki, nafanya uchunguzi wangu na kujiridhisha kabla ya kutoka na kuzungumza jambo fulani.

Bahati nzuri huwa nakutana sana na watu kutoka mataifa tofauti na wakati mwingine huwa napata habari za ndani za timu zetu za Afrika namna ambavyo zinafanya maandalizi yao kuelekea michuano mikubwa ya kimataifa.

Tatizo ambalo lazima lifanyiwe kazi na timu za Afrika ni ‘kujiona’ hapa namaanisha wachezaji ambao wanakuwa wamepata nafasi ya kucheza Ulaya huwa na tabia ya kujiona wana kitu cha ziada. Wanapokutana kwa ajili ya majukumu ya kimataifa kunakuwa na hali ya kukosekana kwa umoja miongoni mwa wachezaji jambo ambalo wanaingia nalo hadi uwanjani.

Kitu kingine ambacho tunasahau ni namna ambavyo timu zetu zinafuzu kwenda kwenye haya mashindano. Mechi zetu zimejaa magumashi mengi, sisi wenyewe ni mashahidi mwaka huu tumeshuhudia kesi kadhaa zinazohusisha waamuzi kupanga matokeo.

Kuna mwamuzi kutoka Kenya ambaye ilibidi akachezeshe kombe la dunia lakini hayupo kwa sababu aligundulika kujihusisha na upangaji matokeo.

Mechi ya kufuzu kombe la dunia kati ya Afrika Kusini dhidi ya Senegal iliyochezwa Afrika Kusini na baadaye kurudiwa kutokana na mwamuzi wa mchezo huo kuhusika kuuharibu kutokana na upangaji wa matokeo. Kutokana na mambo haya kiuhalisia inakuwa vigumu kushindana na timu ambazo zimefuzu bila mizengwe nje ya uwanja.

Kwa hiyo timu zetu za Afrika kuanzia ngazi ya shirikisho la soka Afrika Caf, wanachama wa Caf wajaribu kutengeneza ushindani mkubwa na weledi. Lazima ifike wakati tuwe serious katika level zote kuanzia wachezaji, viongozi, wadau wote pamoja na mashabiki.

Geoff Lea

Mpira wa Afrika unahitaji mageuzi makubwa kwa sababu tumeachwa mbali sana, ukianza kupiga hesabu kuanzia 1970 hadi sasa hivi kuna mataifa kama Sweden, Denmark, Switszalernd tayari yameendelea sisi bado tupo palepale.

Tunahitaji mageuzi kuanzia kwenye falsafa za mpira, standards za ukocha, ligi, kwa mfano mataifa ya Afrika Mashariki kitu kinachoyaokoa  siyo mipango ila ni wachezaji ambao wameshafanikiwa ndio wanazipa uhai timu za taifa.

Hispania walishinda ubingwa wa kombe la dunia 2010 kwa sababu ya faida ya La Masia  (Barcelona), Ujerumani walibeba kombe la dunia 2014 kwa faida ya mipango iliyokuwepo Borussia Dortmund na Bayern Munich lakini huku kwetu kuna tofauti kubwa kati ya vilabu na shirikisho.

Ninaposema soka letu linahitaji mageuzi ni mjadala mkubwa, mpira wetu unaenda kama kipofu aliyetupwa msituni huku kukiwa na giza nene hata Mungu akimbariki macho yakafunguka bado atakuwa haoni.

Tumebarikiwa vipaji pengine kuliko hata watu wa Ulaya lakini kama vipaji hapigigwi hata polish tangu mwanzo haviwezi kufika sehemu.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here