Home World Cup RUS 2018: Kwanini Mwana FA anataka VAR iletwe VPL?

RUS 2018: Kwanini Mwana FA anataka VAR iletwe VPL?

9887
0
SHARE

Hivi VAR unaichukuliaje kwa mawazo yako? Unadhani ni njia sahihi ya kuondoa matatizo? Je Ungetamani iletwe katika ligi pendwa ya EPL au VPL.

Kimsingi VAR imesaidia kwa kiasi chake hasa ukilitizama suala la Neymar kujiangusha. Kila kizuri kina mapungufu yake. Hakuna jema la wanadamu lisilo na kasoro. Hakuna ubaya wa VAR. VAR haidanganyi. Shida ipo kwa upande wa waamuzi. VAR sio suluhisho la mwisho kama tulivyodhania.

Naungana mkono na Mwana FA. Mwana FA anasema “VAR huwa inatuonesha kilichotokea ni nini, na inatupa uhakika zaidi. Lakini kuna matukio tumeona kama ila ya Ronaldo, imeonekana wazi kuwa Ronaldo katumia kiwiko kwa makusudi na ilikuwa na kadi nyekundu lakini tumeona mwamuzi akaamua kutoa kadi ya njano. Wasiwasi wangu ni kwamba, pamoja na VAR ipo lakini bado waamuzi watatumia utashi wao kufanya maamuzi ya mwisho”

Huenda usikubaliane kabisa na msimamo wa Mwana FA. Binafsi yangu nipo upande wake. Kuna wasaa huwa unajiuliza je VAR inawaogopa watu au timu? Mwisho wa siku itabidi ukubaliane na mimi kwamba VAR sio chombo cha mwisho cha usuluhishi. Kama nilivyosema hatuwezi kukataa kwamba VAR inasaidia sana. Ina faida kubwa tu, lakini haitoi mwanga kama itamaliza malalamiko. Wapo watakaosema mwanzo ni mgumu. Kisha watajipiga vifua na kusema “Aaah hakuna teknolojia inayokuja kirahisi”

Juzi tumeona mchezo wa Iran na Ureno mtu alinawa. Nimeona Geoff Lea akijaribu kuelezea mawazo yake kwamba tukio la Mchezaji wa Ureno kunawa ni sawa tu na lile na Marcus Rojo katika mchezo wao dhidi ya Nigeria.

Edo Kumwembe nae akajaribu kwenda tofauti na Lea na wale wengine waliojificha nyuma ya uhuzuni ya Nigeria wakiamini akina Messi wamebebwa.

Edo anasema “Kwanini haikuwa penati? Kwa sababu Rojo alianza kuupiga mpira kwa kichwa halafu ukamgona mkono wake. Hivyo haikuwa dhamira yake. Kama angeenza kuupiga kwa mkono kisha kichwani bila shaka ingekuwa tuta halali. Pale taifa kila mpira unaomgonga mchezaji mkononi “tunataka tuta”. Ile haikuwa penati, Wakati mwingine hauwezi kufafanua haya ukaeleweka kwa sababu sisi tuna unazi. Huwa inapotokea suala kama hilo pale taifa wakiniuliza huwa nayeyusha nawaambia Zari na Diamond watarudiana kweli? Hiyo ndo fani yetu zaidi kuliko soka” Mwisho wa kunukuu Kisha akaweza kiashirio cha kucheka

Mwana FA hapingani sana na VAR lakini yeye anawaza upande wa kushoto wa VAR ” VAR sio kitu kibaya sana. Ni kitu kizuri. Kitaondoa yale makandokando ya malalamishi. Lakini pia kuna wakati nawaza kuhusu sisi mashabiki. Furaha ya mashabiki ni majadaliano ya hapa na pale hasa baada ya mchezo kuisha. Ni kweli mpira ni mchezo wa kibiashara lakini pia yale malalamiko yanaleta utamu wake. Mashabiki wanakaa siku tatu wakibishana hapa na pale kuhusu makosa ya uwanjani n.k. Mpira una figisu zake na ndivyo ilivyo. Ndio mpira huo”

Wakati FA analiongelea hili nimekumbuka tukio la Salah na Ramos.

Kosa la refa uwanjani linajenga historia na huvuruga historia kwa upande wa pili. Huenda Ramos angepewa kadi nyekundu alipoonekana anacheka Salah kwenda nje au kile kiwiko alichompiga Karius. Real Madrid iliweka historia na Liverpool walishindwa. Ile ni rekodi itakayodumu milele. Miaka nenda rudi tukio la Ramos litaimbwa. Ndio. Hata leo Maradona anajivunia bao lake la Mkono.

Lakini hatuwezi kusema soka limeporomoka kwa sababu ya marefa! la hasha! Sidhani. Binafsi bado soka letu lilikuwa salama mikononi mwa wanadamu wenzetu. Tuna wanadamu watano wanasimamia soka. Hii VAR ni mtu wa sita tena nyuma ikiwa na watu watatu lakini bado wanayumba.

Mwisho nikamuuliza Mwana FA ni kweli VAR ni kwa ajili ya rangi fulani? akajibu
“Huo mtazamo wa kusema VAR ni kwa ajili ya wazungu ni mtazamo wa kitoto sana. Kuleta masuala ya ubaguzi wa rangi kwenye soka ni hoja za kipuuzi. Tumeona jana Rojo anataka kuucheza mpira Iheanacho anaparazwa na mguu wakati Rojo anarudisha mguu. Hakuna namna ingeweza kuwa penati, ni utoto kuaminisha watu huo ujinga”

Kwa hili pia Naweza kuamini Vivyo hivyo sawa na FA. Irani sio wazungu walipewa penati ambayo Wanaigeria walinyimwa. Di maria alinyimwa penati ambayo Nigeria walipewa. Mechi ya Iceland na Argentina zilikataliwa penati mbili. VAR hiyo hiyo ilimzawadia Ronaldo penati nyepesi kwenye mchezo wao dhidi ya Hispania. VAR hiyo hiyo imewapa Nigeria penati.

Mwana Fa akaenda mbali kidogo. Akazungumzia suala la ligi yetu. Akasema “Kuna mpira kufuata mkono na mkono kufuata mpira. Mpira uliopigwa na mpinzani unapokwenda moja kwa moja kwenye mkono wa anayezuia mara nyingi ni tuta ikiwa tu mchezaji hakuonesha jitihada za kuuficha mkono. Lakini Mlinzi anapojaribu kuucheza mpira na kiungo kingine cha mwili wake lakini mpira ukaelekea mkononi hatuwezi kusema amedhamiria kuushika. Na ile ya Rojo ni sisi tu kwenye kariakoo Derby usipotoa penati kama ile utashikwa mashati”

Nadhani FA ameelezea tatizo sugu ambalo lilimtoa povu Abdi Banda na kuingia kwenye mgogoro wa chini kwa chini na Haji Manara. Ligi yetu kumekuwa na kasumba kwamba kila mtu anaponawa mpira basi ni penati. Kidogo nikataka kumchimba FA nikamuuliza je VAR inafaa kutumiwa kwenye ligi yetu. Akacheka sana. Kisha akanijibu
“Kama tungekuwa na VAR Tanzania lile tatizo la kung’oa viti taifa lisingetokea. Waamuzi wengi wamekuwa wakijficha kwenye kivuli cha makosa ya kibinadamu au SIKUONA”.

Mwisho mwana Fa akamaliza wa kusema ” VAR bado ina utata, hasa tukio la Ronaldo. Kama mwamuzi aliona Ronaldo kweli katumia kiwiko sehemu ambayo mahusiano ya kiwiko na aina ya ukabaji havikuhusiana kwanini alitoa kadi ya njano badala ya nyekundu? Kwa sababu aliona na alikiri kuwa kiwiko kimetumika? Sasa sijui Refa alitumia busara zipi au kwakuwa Ronaldo ni faza basi akaamu kufukia juu kwa juu”

Makala na Privaldinho unaweza kunifollow Instagram kwa jina hilo hilo. Credit kwa Mwana Fa kwa kukubali kufanya nae Mazungumzo. Tupe mtazamo wako.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here