Home World Cup URUSINI: Misri wamepata nafasi za kizungu wakazitumia kiafrika.

URUSINI: Misri wamepata nafasi za kizungu wakazitumia kiafrika.

10867
0
SHARE

Bila shaka ukizungumzia moja ya safu ya ulinzi bora na imara Misri wanaweza kuwekwa kundi hilo. Hawajufungwa zaidi ya bao moja katika michuano ya kufuzu kombe la dunia. Safu yao ya ulinzi chini ya Fathy imecheza vizuri sana kuhakikisha kwamba sio Suarez au Cavan wanafanya kitu.

Mchezo umekamilika kwa Ushindi wa bao moja kutoka kwa Gimminez kufunga bao la kichwa baada ya kupokea krosi kutoka kwa Sanchez

Walichokuwa wanakosa Misri ni kimoja. Walikuwa wanatengeneza nafasi kizungu lakini wanazitumia kiafrika. Wanashambuliaji bila kujua tageti yao kumalizia ni nani. Ndio maana kila walipofika katika eneo la hatari la Uruguay waliishia kutetemeka miguu kama mwanaume anayetaka kumuomba mrembo namba.

Uruguay walionekana kugundua kwamba uzuri wao ndio uzuri wa Misri. Yaani mipira ya juu. Utagundua walifanya mabadiliko na kumleta Sanchez ili apige krosi kwa sababu hawakuwa na uhakika kwamba Suarez na Cavan watacheza mipira ya chini.

Suarez na Cavan walijaribu mipira ya chini ambayo kwa asilimia 100 walifeli.

Misri walishindwa kugundua kwamba kuwekeza sana kwenye mfumo mmoja wa uchezaji kuna madhara. Kumtegemea Karhaba pekee yake kama mshambuliaji. Inawezekana Mo Salah hajapona na hilo lipo wazi. Mwalimu aliona kabisa kuna ubutu hasa kwenye umaliziaji wa nafasi kitu ambacho Mo Salah ni tiba lakini bado mwalimu hakuwa na uhakika wa Mo Salah.

Kama Misri wataendelea na mfumo huu hu hata Mo Sallah akiingia mechi za hapo baadae msishangae kuona wanatoka kapa bila kupata bao lolote.

Mahesabu ya haraka haraka katika kundi A kuhusu Mechi zilizobaki,ili Egypt afuzu…

-Mechi mbili zijazo za Egypt inabidi ashinde. (Russia na Saudi Arabia)

-Mechi mbili za Russia,apoteze na Uruguay alafu aje kupotea na Egypt.

-Mwisho Saudi Arabia wapoteze zote.

Kwa mahesabu haya, Egypt ataiwakilisha Afrika katika hatua ya 16 bora.

Mechi zilizobaki ni rahisi mno kwa Misri kushinda kama mwalimu atabadili mfumo na wachezaji kuwa huru. Kila mchezaji wa Misri alicheza kama mfungwa. Hawana kitu cha Ziada wakiwa na mpira. Ni mara chache sana kuona krosi zinapigwa au wakijaribu mashuti hakuna pasi za mwisho za kuchomekea utaona tu wakikimbilia pembeni na mwisho wa siku wanaupoteza. Hawana mshambuliaji ambaye anaweza kutengeneza nafasi yake binafsi.

Hawana uwezo wa kufungua nafasi na zikazaa matunda. Wanakimbilia maeneo ambayo hayana tija kwenye kutengeneza nafasi za hatari. Nimejiuliza sana kwanini Ramadhan Sorby hakucheza tokea mwanzo. Misri wamekuwa na ubutu sana hata kwenye mechi za kufuzu. Ni timu inamtegenea zaidi Salah. Lakini hii ni michuano ya kidunia na ni hatari sana kumtegemea mchezaji mmoja.

Sio mbaya sana kwenye ulinzi ni kosa dogo na kwa mzungu hata nukta yeye ana amini ina umuhimu kwenye sentensi.

makala hii imeandaliwa na Privadinho (Instagram)

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here