Home Ligi LA LIGA Alichokosa Gaddafi ni kipara cha Zidane Saladin

Alichokosa Gaddafi ni kipara cha Zidane Saladin

12476
0
SHARE

Zidane ametuachia maswali mengi sana. Lakini unadhani maswali yake yana majibu mepesi kweli? Bila shaka majibu yake ni marahisi mno lakini ukiona moshi unafuka ujue kuna moto chini.
Makocha wengi sana wametumia hii mbinu aliyotuduwaza nayo Zidane. Jose Mourinho na Pep Guardiola ni makocha walioacha vibarua vyao licha ya kwamba walipata mafanikio makubwa. Tofauti kidogo na hili la Zidane ni FUNUNU.

Zidane amefanya maamuzi haya ghafla bila fununu zozote. Hakuwahi kuelezea kuwa ataondoka Madrid wakati gani. Akina Guardiola na Mou walitangaza kuwa wataondoka aidha mwisho wa msimu au mkataba ukiisha. Zidane bado alikuwa na miaka miwili kabatini.

Hamis Jamal ananikumbusha kwamba mafanikio sio uwezo tu ni fursa na nafasi unazotumia kila zinapotoke. Zidane alitumia nafasi zake vyema.

Nimewaza sana kuhusu Ronaldo kutokuonekana kwenye video ya utambulisho wa jezi mpya za Madrid.
Je ni kweli kwamba Ronaldo anaweza kuondoka? Jibu ni ndio. Ameshaipatia Madrid kila kitu. Umri wake utaondoka na kila kitu chake. Je Perez anahitaji nini cha zaida kwa Ronaldo? Hakuna. Kwahiyo? Miaka kadhaa ijayo Ronaldo ni kama ganda la ndizi ukiliacha ndani litaangusha watoto.

Je Zidane alimhitaji Ronaldo? naweza kusema ndio. Kwanini? kwa sababu ninaamini siri kubwa ya mafanikio ya Madrid ni ndoa ya Ronaldo na Zidane. Je Zidane yupo tayari kubaki mjane pale Madrid endapo Ronaldo ataondoka? Jibu ametoa leo kwamba hayupo tayari
Rafiki yangu Aidani Mlimbila anasema hivi, Zidane amefanya uamuzi sahihi kabisa. Ameondoka na heshima isiyo na doa. Heshima ambayo haitochafuliwa kamwe na itakumbukwa milele.

je unakubaliana na Aidan Mlimbila? Mimi namuunga mkono asilimia zote.

Kwa Mawazo ya Mlimbila ni wazi kwamba Zidane hajaondoka ili kutafuta changamoto mpya ila ameondoka mapema kabla maji hayafika shingoni hapo baadae. Ni kama Zidane ameona unabii.

Duniani kila kocha anaiwaza UEFA, hakuna ligi bora na ya kujivunia kama La Liga hasa ukiwa kocha wa Madrid na Barcelona. Kila mchezaji na kila kocha anaiwaza Madrid au Barcelona.

Hivi mnadhani Mou aliondoka Madrid kwa kupenda? Unadhani Guardiola hatamani kurudi Barcelona?

Gaurdiola alisema hivi “kwa hali hii nikiendekea kubaki hapa, ipo siku mtakwazika na mtanikwaza na wote tutaumia na heshima zetu zitashuka”

Kwani ni kombe lipi kubwa zaidi ya UEFA na La Liga ambalo Zidane anataka kwenda kushindana nalo? Au ana ndoto na kombe la dunia? Bila shaka Hili Swali Zidane mwenyewe hawezi kukujibu

Zidane ana akili sana. Amenikumbusha hadithi za Kanali Muammar Gaddafi.
Gaddarf alikuwa mtawala wa kiimla wa Libya. Nadhani unamkumbuka vyema. Heshima aliyokuwa nayo Gaddafi ni sawa na hii ya Zidane Madrid. Alifanikiwa katika nyanja zote za kiuchumi na kiulinzi ndani ya taifa lake. Alichokosea ni kimoja tu. Hakujua wakati gani aondoke na heshima yake. Aliamua kuwa Arsene Wenger.

Tukubali tu kwamba Wenger ameondoka kama mkimbizi, aliikuta Arsenal nafasi ya 6 leo kaiacha ya tano, Zidane aondoka watu wanalia, Wenger watu wanashangilia.
Wenger ameondoka kama kocha aliyefeli na ni wachache sana wanaotambua heshima yake. Kocha mkubwa kama Wenger unaondoka watu wanashangilia?. Miaka 22 yenye kila aina ya tusi kwa kila aina ya mshabiki wa Arsenal. Gaddafi aliyeishi kwenye makasri ya kifalme safari yake ya mwisho ilikuwa kwenye mtaro wa Maji machafu. Je mlitaka Zidane nae aelekee huko?

Hii sio kwa Mara ya kwanza Zidane anafanya uamuzi wa busara unaoacha fedheha kubwa kwa mashabiki nyuma yake.
Baada ya kombe la dunia nchini Ujerumani Zidane alistaafu huku akituachia kumbukumbu murua akiwapiga kanzu na matobo De lima na Dinho. Je Madrid ilikuwa haimhitaji zidane kwa wakati huo? Je ni kweli Zidane alifulia? Jibu ni hapana. Aliondoka na utamu wake. Wadogo zetu wa kike wajifunze kitu kutoka kwa Zidane. Yaani wasijiachie sana mpaka wakachokwa.

Bila shaka hakuna kocha ambaye angeweza kutwaa nafasi ya Zidane Madrid kwa sasa. Zidane ameondoka lakini ameacha kilio. Nimejaribu kuuva uhusika wa Perez kwa sasa.

Labda nikukumbushe kitu
Walio wengi hasa waislamu nadhani wanamfahamu Sultan Saladini. Saladin alikuwa jemedari wa kwanza na mwenye heshima kubwa kwa waislamu na waarabu hasa hasa wa Misri. Jemedari alifanikiwa kupigana kwenye vita vya msalaba mara tatu na kushinda mbili za mwanzo isipokuwa vita ya tatu ambayo vita iliisha kwa makubaliano.

Ni Jemedari wa kiarabu aliyefanikiwa kuiweka Yerusalem chini ya himaya yake.
Mwaka 1187 Saladin alifanya maajabu makubwa hapa duniani. Aliivamia Palestina na kuiteka Hattin na kumfanya mateka Mfalme Guy. Mwezi Julai Akaifanyia kufuru Yerusalem kwa kumteka mfalme wao na kumuua Reignald Chattilon mmoja wa maadui zake wakubwa. Alimuua Chattilon kwa mkono wake mwenyewe.

Saladin huyu huyu aliingia kwe vita na Mfalme Richard wa I wa Uingereza. Katika vita hii Saladin na jeshi lake lijukikanalo kama Salah al-Din lilipoteza baadhi ya maeneo muhimu. Sehemu kubwa iliyobakiwa nayo ilikuwa Yerusalemu lakini miji mingine ilikwenda kwa Richard.

Alipoona hali ni mbaya ilibidi akubaliane na mfalme Richard kwamba aendelee kuwa mtawala halali wa Yerusalemu lakini wakristu waliruhusiwa kuingia Yerusalem bila kubughudhiwa na jeshi.

Kwanza Saladin atakumbukwa kwa heshima kubwa. Hasa pale alipoiteka Yerusalem lakini hakutaka kuua mtu awae yeyote. Aliweka malipo kwa mtu akitaka kuishi ndani ya Yerusalemu lazima alipe kodi ambayo ilikuwa dola 50 kwa sasa. Yeyote aliyejisikia kuondoka aliondoka bure na mali zake na kula kitu. Hakumfanya mtu yeyote kuwa mtumwa.

Hata alipopigana Vita na Mfalme Richard baada ya kugundua farasi wa mfalme Richard aliiumizwa alimpa farasi wake arudi nae nyumbani. Yaani alimsaidia adui yake arudi nyumbani salama. Saladin ni mfalme wa kukumbukwa zaidi kwa dini zote.

Ipo filamu moja hivi maarufu sana inamhussu huyu mfalme ijulikanayo kama Kingdom Heaven kama sijakosea

Zidane namuona kama Saladin.

Mwanzoni mwa Misimu yake ya kwanza alianza vyema. Msimu huu wa tatu mambo yamemkataa hasa hasa kwenye ligi na hata baadhi ya mapambano muhimu pale Bernabeu amepoteza ikiwemo na Buyern, Barcelona na Juventus.

kwenye msururu wa matokeo mabovu ya ligi ulitia shaka sana maisha ya Zidane klabuni hapo. Gari lilipata moto dakika za Mwisho na hata kutwaa ubingwa wa UEFA. Wakati huu Ronaldo alikuwa amerudi uwanjani baada ya kupigwa marufuku.

Michezo ya mwanzo ilikuwa na matokeo mabovu sana. Hili lilikuwa sawa na pambano la Saladin na mfalme Richard. Zidane amegundua kama ataendeleza sakata hili atapoteza Yerusalem (Heshima yake). Saladin alikubali yaishe maana vita ya tatu alipoteza wanajeshi zaidi ya 7000.

Vita ya UEFA ya Zidane ya Mwisho hii ni kama atapoteza mwanajeshi wake muhimu sana (Ronaldo) na baadhi ya wachezaji wa muhimu umri unakwenda. Hivyo kama akiendeleza pambano atapoteza heshima yake, utawala wake na angebaki kuwa mtumwa. Akili hii Gaddafi aliikosa.

Hayo ndiyo mawazo yangu. Ni heri zidane akapoteze heshima kwingineko lakini sio Madrid.

Utamwambia nini Zidane? hasa kwa Dunia hii ambayo kumpata mrithi wa Ronaldo mchezaji wa hadhi ya Juu kama Hazard ni Paundi milion 200 ? Unadhani pengo la Ronaldo litazibwa na mchezaji mmoja tu? Madrid itahitaji kuwekeza zaidi ya Milion 400 je Zidane yupo tayari kutoa hela hiyo? Je wakitoa hiyo hela na mambo yakabuma? Si ndo ataanza kudharauliwa?

Asante Zidane kwa Rekodi Asante Zidane kwa kutukumbusha kuwa kila kitu ni kiasi.
Makala hii imeandaliwa na Privaldinho unaweza pia kunifollow instagram kwa jina hilo hilo.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here