Home Kimataifa Arsene Wenger vs Unai Emery, adui mmoja, mbinu, mafanikio na matumizi tofauti

Arsene Wenger vs Unai Emery, adui mmoja, mbinu, mafanikio na matumizi tofauti

7804
0
SHARE

Arsene Wenger ameondoka Arsenal, na taarifa za hivi karibuni zinadai kwamba kocha waliyepita wa PSG Unai Emery atarithi mikoba ya Arsene Wenger. Hii ni kwa mara ya kwanza kwa Arsenal kuwa na kocha mpya katika miaka 22 na wengi tunasubiri kuona nini kipya Emery ataleta Arsenal.

Katika kuthibitisha kwamba Emery ni kocha mpya wa Arsenal, hapo jana katika website yake binafsi walipandisha kimakosa picha ambayo ilikuwa na ujumbe wa kuonesha furaha yake kujiunga na Arsenal ujumbe ambao baadae uliondolewa.


Tuanze kuwaangalia makocha hawa, kwanza kabisa kama ulikuwa hujui tu kwa kuanzia wote hawa wawili Wenger na Emery ni maadui na Jose Mourinho, wakati Wenger na Mou wameshakwaruzana mara nyingi achilia mbali unafiki wa kuchekeana wakati Wenger alipotamgaza kustaafu lakini Unai Emery naye alishawahi kumfananisha Mourinho na mtoto anayelialia”Cry Baby” mwaka 2010 akiwa Sevilla wakati huo Mou akiwa Real Madrid na kuanzia hapo uhusiano kati ya wawili hawa ukawa mbovu.

MBINU.

Arsene Wenger. Amekuwa muumini mkubwa wa 4-4-2 kutokana na imani ya mbinu hii kumpa kile atakacho, mzee Wenger mara nyingi amekuwa akiamini 4-4-2 kwamba pamoja na kutopata matokeo lakini mfumo huu ulikuwa ukiwafanya Arsenal kucheza mchezo wa kuvutia.

Mwaka 2005-2006 Wenger alikuwa akitumia 4-5-1 kwa kujaza viungo wengi katikati ya uwanja na hii iliwasaidia Gunners kufika fainali za CL, wakati wakiwa na Fabregas mzee Wenger aliichezesha Gunners 4-3-3 kutokana na ubora wa Cesc na kumfanya aonekane kinara, msimu wa 2016-2017 Arsene Wenger akaanza kuichezesha Arsenal 3-4-3.

Unai Emery. Waandishi wengi Ufaransa wanamtaja Emery kama mtu wa kazi ambaye huwa anasisitiza kufanya kazi mazoezini. Lakini kimbinu Emery anaweza kuibadili Arsenal kabisa na Arsenal wanaweza kuanza kucheza 4-2-3-1 mfumo alioutumia Valencia na Sevilla.

Uwepo wa Lacazette, Aubameyang na Mkhitaryan katika kikosi cha Gunners unaweza pia kumpa nafasi Emery kuichezesha Arsenal 4-3-3 kama ilivyokuwa PSG alipokuwa na Neymar, Edison Cavani na Mbappe lakini wengi wanaamini 4-2-3-1 inaweza ikaendeleza soka zuri la Arsenal pamoja na kuanza kutengeneza Counters.

MAFANIKIO

Arsene Wenger. Katika kipindi cha miaka 22 ya Wenger ndani ya Arsenal unaweza kuigawa katika vipindi viwili, kipindi cha kwanza ni miaka 11 ya Wenger ndani ya Arsenal na hiki ndicho kipindi ambacho mzee Wenger alikuwa na mafanikio Gunners.

Kipindi hiki cha miaka 11 ya kwanza ya Wenger ilikuwa cha kibabe kwani msimu wake ambao aliongoza Arsenal msimu mzima ilikuwa 1997-1998 akawapa Gunners EPL tena alama 12 juu ya wapinzani wao wakubwa Manchester United na kubeba FA.

2001-2002 akawapa tena EPL wakiwa alama 7 juu ya wapili Liverpool na alama 12 juu ya United, wakawapiga Chelsea na kubeba FA. 2003-2004 ndio Wenger akabeba kombe la EPL kitemi zaidi kwa kumaliza bila kufungwa. Wenger pia alibeba FA 1998, 2002, 2003, 2005, 2014, 2015 na 2017 huku wakicheza fainali ya CL 2006.

Unai Emery. Jambo kubwa ambalo Ulaya haitamsahau Unai Emery ni makombe 3 mfululizo ya Europa aliyobeba akiwa na Sevilla. 2014 waliifunga Benfica kwa penati, 2015 wakaifunga Ukrainians Dnipro kisha wakaipiga Liverpool 2016.

Alipohamia PSG msimu wake tu wa kwanza kombe la ligi likaenda kwa Monaco lakini msimu uliofuata wakalitetea, baadae Emery akashinda French Cup na French league Cup akiwa na PSG kabla ya kibarua chake kumalizika.

MATUMIZI YA PESA.

Arsene Wenger. Katika rekodi inaonekana Wenger amenunua kwa £827.1m katika miaka yake 22 na kuuza wachezaji kwa £577.28m. Hii inaonesha ni sawa na £249m tu ndio kiasi ambacho Arsenal wametoa kwa wachezaji wapya katika miaka hiyo 22.

Pamoja na imani kwamba Wenger sio mtumiaji mkubwa lakini siku za usoni hali ilibadilika na Arsenal walianza kufanya usajili kwa pesa kubwa, Pierre Aubameyang alinunuliwa kwa £57.38m, Alexandre Lacazette akanunuliwa kwa £47.70m, Arsenal ilikuwa timu inayotoa pesa nyingi za usajili tangu mwanzo lakini Wenger hakuwa tu akipenda kutumia pesa nyingi.

Emery. Tofauti na makocha wengi wa kisasa Unai Emery anaonekana ni kocha ambaye amezoea maisha ya bajeti finyu. Akiwa Valencia mwaka 2008 na 2012 Emery hakuwahi kusajili mchezaji kwa bei zaidi ya £9m.

Pamoja na kutosajili alishuhudia nyota wengi wa kikosi chake wakiondoka, wachezaji kama David Silva, David Villa na Raul Albiol waliondoka Valencia lakini bado Valencia ilibaki kuwa timu bora La Liga.

Msimu wa kwanza wa Emery ndani ya Valencia walimaliza nafasi ya sita, kisha Emery akaiongoza Valencia kuwa top 3 ya La Liga kwa mismu mitatu mfululizo, baadae alikwenda Sevilla ambako usajili wake mkubwa ulikuwa wa Ciro Immobile kutoka Dortmund kwa £9m.

Wakati akimnunua Ciro Imobille ilishuhudia Sevilla ikiwapoteza Alberto Moreno aliyekwenda Liverpool, Ractic akaenda Barcelona, Carlos Baca akaenda Ac Milan, huku Aleix Vidal akienda Barca na bado Sevilla wakabeba Europa mara 3 mfululizo.

Akiwa PSG sera na mabadiliko ya haraka aliyokuwa akiyataka mmiliki wa klabu hiyo Nasser El Khelaifi yalimlazimu Emery kutumia pesa, msimu wa kwanza tu akatumia £124.65m kusajili nyota watatu tu Julian Draxler, Goncalo Guedes, Grzegorz Krychowiak na Jesse.

Habari kubwa ikawa msimu uliofuata wa Emery ndani ya PSG ilikuwa kufuru, rekodi ya usajili ya dunia ikavunjwa kwa kumnunua Neymar kwa £198m, kisha Kylian Mbappe akaja kwa mkopo na makubaliano ya kumnunua kutoka Monaco kwa £166m.

Kikazi Gunners wajiandae kupata kocha ambaye halali na Emery mwenyewe amekiri kutumia masaa 5/24 kulala na muda wote uliobaki anawaza mbinu za soka tu, lakini lugha inaweza kuwa mtihani mkubwa kwake japo ni kocha ambaye huwa anatumia video mara nyingi kufundisha.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here