Home Kitaifa Dar es Salaam-Pacha: Endelea kuiogopa Yanga, hatari ya Simba ni Kwasi na...

Dar es Salaam-Pacha: Endelea kuiogopa Yanga, hatari ya Simba ni Kwasi na Gyan

17120
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

LICHA ya kuachwa pointi 11 na viongozi wa ligi-mahasimu wao Simba SC, mabingwa watetezi Yanga SC wataendelea kuwa tishio kwa kikosi cha Pierre  Lechantre wakati timu hizo zitakapombana Jumapili hii katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo unaotazamwa na wengi kama ‘utakaoamua bingwa wa VPL’ msimu huu.

Kuachwa alama 14 mechi nne-sita kabla ya kumalizika kwa msimu

Wakati Simba walipoangusha alama mbili katika uwanja wa Samora, Iringa dhidi ya Lipuli FC weekend iliyopita ilionekana kama Yanga wangetumia ‘mwanya’ huo ‘kubalansi mbio za ubingwa’. Baada ya sare ya kufungana 1-1 na Lipuli Jumamosi iliyopita, hesabu zilikuwa zinaenda-alama pacha, kama Yanga ingeshinda michezo yake yote mitatu ya mkononi (Mbeya City FC 1-1 Yanga, Mtibwa Sugar FC vs Yanga, Tanzania Prisons vs Yanga, ukiwemo huu dhidi ya Simba).

Lakini, Idd Selemani alitibua kila kitu wakati alipoifungia City goli la kusawazisha katika dakika ya mwisho ya nyongeza (90+5) Jumapili iliyopita na kufanya Yanga kushindwa kupunguza gepu la pointi baada ya washindani wao Simba kuvutwa shati. Ilikuwa sare ya kufadhaisha mno kwa maana City walicheza pungufu mchezaji mmoja na bado waliweza kuwarudisha nyuma Yanga na kufanikiwa kusawazisha.

Kuelekea mchezo  wa Jumapili hii, Simba wana alama 59, na watakuwa wamebakisha michezo minne tu kabla ya kumaliza msimu. Hawajapoteza mchezo hadi sasa. Yanga wanafuatia wakiwa na alama 48-pointi 11 nyuma ya viongozi, na wanaingia katika mchezo huu wakiwa na michezo  23-mechi 7 kabla ya kumaliza msimu.

Kupoteza dhidi ya Simba ni jambo litakalo waondoa rasmi mabingwa hao mara tatu mfululizo katika mbio  za ubingwa-kwani watakuwa nyuma kwa alama 14, Yanga ikiwa imebakiwa na alama 18 tu tena kama watashinda michezo yao yote sita baada ya Dar-Pacha. Ili kuzuia hili lisitokee ni lazima ‘wachezaji wafie uwanjani’ na kuhakikisha wanaifunga Simba jambo ambalo litawarudisha katika mbio za ubingwa.

Ushindi utawafanya Yanga kufikisha alama 51-na watakuwa nyuma kwa alama nane tu, na michezo miwili ya viporo ambayo wakishinda itawafanya wawe nyuma kwa alama mbili. Simba wataenda, Songea kucheza na Majimaji FC inayopigana kutoshuka daraja, wataenda Singida kucheza na timu iliyopoteza mwelekeo-Singida United.

Lakini pia Simba bado wana mchezo dhidi ya Kagera Sugar FC katika uwanja wa Taifa, hivyo uwezekano wa mbio za ligi kuendelea hadi siku ya mwisho ya msimu ni mkubwa-na Yanga ndio wenye uwezo wa kuonyesha hilo na lazima wahakikishe wanaifunga Simba Jumapili hii kabla ya kufikiria kuhusu safari nyingine ngumu za Morogoro na Mbeya kumaliza viporo vyao.

Endelea kuiogopa Yanga

Kulinda ubingwa wao, ni lazima Yanga waifunge Simba kwa namna yoyote ile kwa kutegemea kundi lao la ‘yosso wenye vipaji.’ Yusuph Mhilu amekuwa mfano wa kuigwa hadi sasa. Kijana huyu ana nafasi ya kuanza katika safu ya mashambulizi sambamba na Mzambia, Obrey Chirwa na kwa mara ya kwanza anaweza kucheza ‘Dar es Salaam-Pacha’

Jitihada zake zimemfanya kuwa mbele ya Ibrahim Ajib. Said Juma Makapu-sijui ni kwanini hakutumika katika mchezo uliopita vs City pale Sokoine Stadium. Kabla ya Yanga kubanwa mbavu na kufungana 1-1 na Singida United katika uwanja wa Taifa walikuwa wameshinda michezo saba mfululizo ya ligi-na kukusanya alama zote 21-nyumbani na ugenini.

Ilikuwa ni wakati makocha aliyeondoka George Lwandamina, Shadrack Nsajigwa na Noel Mwandila walipokutana na rundo la wachezaji majeruhi-hasa  wale wa nafasi muhimu. Makapu alikuwa suluhisho na kiongozi mzuri katika beki ya kati-alicheza na nahodha Nadir Haroub, ama nahodha msaidizi Kelvin Yondani ama Vicent Andrew na alionyesha ni mchezaji bora katika timu.

Itapendeza kuona kijana huyu akianza katika kiungo cha chini mbele ya Kelvin na ningengependa kuona Nadir akijumuika nao katika ngome ya kati. Simba wanategemea zaidi safu yao ya mashambulizi. Emmanuel Okwi amekuwa akikimbilia zaidi upande wa kulia, nahodha John Bocco amekuwa akibaki eneo la kati ili kusubiri mipira inayozagaa, krosi na pasi za kupenyenyeza za Asante Kwasi.

Wawili hawa wamekuwa wakiziyumbisha safu nyingi za ulinzi msimu huu ndio maana Okwi anaongoza chati ya ufungaji akiwa na magoli 19, Bocco akifuatia akiwa na magoli 14. Uwepo wa Makapu ambaye wakati mwingine amekuwa akicheza ‘faulo za kitaalamu’ kutawafanya Okwi na Bocco kuwa chini ya ulinzi wa uhakika muda wote.

Naamini hii ni mechi ambayo hata Sir Alex Ferguson angekuwepo katika benchi la ufundi Yanga angempanga nahodha Nadir. Nadir ni mchezaji wa mechi kubwa siku zote, hajatumika sana na yupo fiti. Anaweza kumficha Okwi ama Bocco, huku uzoefu ukihitajika mno kwa beki ya kati ya Yanga na hapo ndipo napofikiria kumuacha nje Andrew.

Kelvn, Nadir na Makapu wameshacheza sana dhidi ya Okwi katika Dar-Pacha, na Yanga wana bahati wanakwenda kuwakabili washambuliaji hao wakiwa na walinzi watatu wa kati wenye uzoefu-Nadir, Kelvin na Makapu. Okwi na Bocco wamekuwa wakifungia uzoefu wao pia katika ligi hivyo ni lazima watazamwe kama wachezaji wa mechi kubwa japo hawakufunga katika michezo miwili waliyokutana msimu huu (Ngao ya Jamii na VPL mzunguko wa kwanza.)

Juma Abdul, na Mzimbabwe, Thaban Kamusoko wanaweza kuongeza namba ya wachezaji wazoefu ‘Dar-Pacha’ upande wa Yanga. Abdul bado atakuwa na mchango mkubwa pia katika ulinzi dhidi ya Shiza Kichuya ambaye tayari ameshaifunga Yanga katika michezo yote mitatu aliyokutana nao katika VPL akiwa mchezaji wa Simba.

Shiza amekuwa ‘kama shetani’ ambaye kikawaida mara zote hujitokeza wakati wa matukio mabaya. Staili yake ya kuvamia lango akitokea kati ya uwanja tangu kuondoka kwa Joseph Omog kumemfanya kijana huyu kuwa hatari sana katika upigaji wa pasi za mwisho. Amekuwa akikimbia na mpira huku akitazama juu-jambo muhimu kwa mchezaji ambalo mara zote huleta tofauti ya mchezaji na mchezaji.

Kama Kichuya atatumia zaidi upande wa kushoto, Juma anaweza kufanya kazi naye, na kama atatumia ujanja wake wa kushambulia akitokea kati mwa uwanja ndio maana nasisitiza uwepo wa Kamusoko, Papy Tshishimbi lazima uambatane na Makapu ili kuifanya timu yao kuwa ngumu katika ulinzi.

Kama Mhilu ataanza, inamaana mmjoa kati ya Rafael Daud na Pius Buswita atapaswa kuanzia benchi na hii inapaswa kumtokea Daud ambaye amefunga magoli mawili katika michezo minne iliyopita ya Yanga. Buswita anaweza kumvuruga raia wa Ghana James Kotei ambaye amekuwa akicheza mbele ya walinzi Juuko Murshid/Erasto Nyoni ama Yusuph Mlipili.

Katika michezo ya karibuni chini ya Lechantre, Nyoni, Shomari Kapombe, Jonas Mkude wamekuwa wakicheza zaidi eneo la kiungo. Timu nyingi zimekuwa zikiadhibiwa na Simba kwa kuamini watatu hao ndio wapishi wa magoli ya Simba-hapana, si kweli. Hawa wamekuwa walinzi wa kwanza muhimu wa Simba mchezoni ndio  maana kiasili wote si viungo washambuliaji.

Katika mfumo wa 3-5-2, Kotei, Juuko, Mlipili wamekuwa wakicheza kama walinzi-pacha wa kati. Nicolaus Gyan amekuwa akicheza kama ‘wing back’ wa kulia, na Asante Kwasi katika ‘wing back’ ya kushoto. Hawa ndiyo wapishi na waanzilishi wa mashambulizi yote hatari ya Simba-Kapombe ni nyongeza ya tatu na ili Yanga wamudu mechi watapaswa kuwatazama watatu hawa na kuwawekea mikakati.

Kocha aliyekuwa amepewa kibarua cha muda, Mwandila aliichezesha  Yanga katika mfumo wa 4-4-2. Sidhani kama kocha mpya Zahera Mwinyi atabadili sana timu hiyo aliyoanza kuionoa katikati ya wiki hii. Mfumo huu kwa Yanga ni mbaya, nasisitiza ni mbaya kwa sababu timu imekuwa ikitoa mwanya mkubwa kwa wapinzani kutawala kiungo.

Yanga ya sasa ‘ina-safa’ katika ufungaji, lakini bado wanaweza kutumia mfumo wa 3-5-2, ama 4-5-1 ili kudhibiti kiungo kwa kuwapa nafasi wachezaji wengi wa nafasi hii walionao kikosini. Ningekuwa na nafasi ya kushauri benchi lao la ufundi-mfumo sahihi wa kutumia ni 4-5-1. Abdul na Gadiel Michael katika beki za pembeni. Nadir na Kelvin katika beki ya kati. Makapu, Tshishimbi, Kamusoko, Rafael na Buswita katika kiungo. Chirwa katika mashambulizi.

Au 3-5-2, Kelvin, Nadir, Makapu kama walinzi pacha watatu pale kati, Abdul na Gadiel/Mwinyi Haji katika wing back, Kamusoko, Tshishimbi na Buswita/Rafael . huku mbele wakianza Chirwa na Mhilu/Buswita. Simba wana beki ya wasiwasi na Chirwa ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kucheza vizuri na kumalizia nafasi katika michezo mikubwa.

Bado naipa nafasi kubwa ya ushindi Yanga kutokana na aina na mwelekeo wa ligi, mechi hii inahitaji hamasa tu, na Yanga wana hamasa hiyo japo si rahisi kuiona. Usiwadharau, endelea kuwaogopa Yanga. Wanapoamua kufanya, wanajitolea hasa. Wana kikosi kizuri, beki imara, viungo wazuri na mshambuliaji ambaye anaweza kuwafungia goli muhumu.

Ibrahim Ajib

Kama atapewa nafasi katika mfumo wowote ule, beki ya Simba itakuwa matatizoni, lakini kijana huyo si wa kumtegemmea kutokana na mchezo wake usiovutia. Hajitolei uwanjani, amekuwa akipoteza sana mpira mchezoni, hakabi na hajui kwa nini Yanga inahitaji zaidi magoli yake kuliko ‘mbwembwe’ zisizo na maana ya kuleta ushindi kwa timu.

Mwanzoni mwa msimu niliandika makala na kusema ‘Ajib ni namba kumi hasa’, ilikuwa ni wakati alipoingia Yanga na kukutana mastaa wote wa timu katika ufungaji Amis Tambwe na Donald Ngoma wakiwa na majeraha huku Chirwa akitumikia adhabu. Lakini tangu alipocheza kwa kiwango cha chini vs Township Rollers ya Botswana katika ligi ya mabingwa mchezaji huyo ameonekana kuachwa mbali mno na Mhilu, Emmanuel Martin,  Buswita.

Bado anaweza kuthibisha ubora wake lakini kama hatoendelea kujituma ni wazi atakuwa ‘mzigo’ katika mchezo wa Jumapili hii. Kumchezesha Ajib vs Simba kwa sasa naona kama ‘mchezo wa kamari-kula ama kuliwa’ ila anaweza kuwa nyota wa mchezo kama atakuwa na ‘siku ya kujituma’ na Ajib anapokuwa mwenye jitihada, mabeki wengi hushindwa kumdhibiti-atafunga ama atapiga pasi za video zenye kuzaa matunda kwa wenzake.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here