Home Kimataifa Mabadiliko ya Arsenal hayatakuwa magumu kama ilivyokuwa Manchester United

Mabadiliko ya Arsenal hayatakuwa magumu kama ilivyokuwa Manchester United

11033
0
SHARE

Arsene Wenger kuondoka kwake kila mtu anasema lake, wengine wameshaanza kusema bora angebaki tu na wengi hao hawa wanaamini sio suala rahisi kubadili kocha uliyekaa naye muda mrefu na wengi wakiitolea mfano Manchester United.

Baada ya utawala wenye mafanikio makubwa wa babu SAF aliamua kuachia ngazi huku msimu wake wa mwisho akibeba ndoo, Fergie alichukua kombe tena akiwa na tofauti ya alama 11 na mshindi wa pili na hili likawa kombe lake la 5 katika misimu yake 7 ya mwisho.

Akaja kuichukua timu David Moyes, kilichotokea kuanzia hapo ni uhaba mkubwa sana wa makombe. United wakaanza kuanguka na taratiibu ikawa sio timu ile yenye spirit ya ushindi kama ile iliyoacha na Sir Alex Ferguson, watu wakamkumbuka babu.

Kuna mambo mawili au matatu yalimgharimu David Moyes, moja ambalo ni kubwa zaidi ilikuwa ni mzigo anaouchukua, unachukua timu kutoka kwa kocha ambaye achilia mbali makombe 49 aliyoipa timu lakini katika miaka yake 10(2003-2013) amebeba makombe ya EPL 8, Champions League na klabu bingwa dunia.

Moyes aliipewa United ikiwa United ambayo haiwezi kukaa miaka miwili bila ndoo, Moyes aliipewa United ambayo walikuwa miamba haswa, United ambayo ni watawala wa ligi na watawala wa kila mtu, hii ikaaminisha kila mtu wa United kwamba wao wanapaswa kushinda tu kwa kuwa wao ni United.

Achana na hilo, lakini la pili ambalo nalo ni kubwa zaidi. Wakati Ferguson anwapa United kombe la mwisho kabla hajaondoka alikuwa na miamba kama Robin Van Persie,Michael Carrick, Rio Ferdinand, Patrice Evra, Ryan Giggs na Nemanja Vidic hao ilikuwa roho ya United.

Nini kilitokea kwa Moyes? Wachezaji ambao walikuwa roho ya timu walikuwa wote wako na miaka 30 au wanakaribia 30. Moyes akachukua timu ambayo imeshaanza kuchoka na waliokuwa hawajachoka hawakuwa wachezaji muhimu sana kwa United.

Kina Paul Scholes, Giggs, Ferdinand tayari ukaanza kuwa mwisho mwishonwa soka leo, RVP naye akaanza kuchoka akaondoka, vivyo hivyo kwa Vidic na Evra na hapo Moyes ikambidi aonekane kama anaanza upya kutafuta watu wa kukaa nafasi za waliochoka.

Kwa Wenger sasa, mzee Wenger anamaliza msimu akiwa nafasi ya sita na huu ukiwa msimu mbovu kwake katika miaka 22, Arsenal wanamaliza msimu huku tofauti yao na timu iliyoko kileleni ni kubwa kuliko tofauti na timu iliyoko mkiani.

Tofauti na mrithi wa Fergie, kocha anayekuja Arsenal anapata nafasi ya kuanzisha utawala mpya EPL, japo mashabiki wanatamani awape kitu kipya tofauti na Wenger lakini kocha anakuwa hayuko katika presha kubwa tofauti na Moyes.

Kina Thomas Tuchel, Patrick Vieira, Luis Enrique au Thiery Henry ni makocha wa kisasa ambao wana njaa na kujenga utawala mpya baada ya utawala wa zamani wa SAF na kina Wenger kuondoka, aina ya vijana hawa wanaweza kuichukua Gunners bila presha yoyote na kuanza kuileta Arsenal ya kisasa.

Lakini jambo lingine ni aina ya kikosi ambacho mrithi wa Wenger anapewa, kuna vijana wengi wadogo ndani ya Arsenal ambao huu sasa ndio muda wao wa kucheza soka, asilimia kubwa ya wachezaji wa Wenger wana umri kati ya 20-28, na maingizo mapya msimu huu yanaonesha wazi Arsenal inazidi kuwa na kikosi cha ushindani.

Pierre Emerick-Aubameyang, Mesut Ozil na Henrikh Mkhitaryan wanaelekea 30, lakini anagalia Bellerin, Lacazette, Sead Kolasinac,Danny Welbeck, Iwobi wote wanacheza wakiwa na umri kati ya 23-27. Wenger tayari alitengeneza kikosi ambacho kinadumu mda mrefu.

Lakini kama hujui tu ni kwamba wakati wa SAF pale United David Gill alikuwa akifanya kazi bega kwa bega na Ferguson lakini baada ya Fergie kuondoka ndio Ed Woodward akawa mtendaji mkuu, na tofauti ya Gill na Woodward ni kwamba Gill alikuwa anajua kuhusu soka na timu lakini Woodward anajua tu kuhusu biashara ya mpira.

Gill alikuwa anaamini kuhusu kutengeneza aina ya timu ambayo itapata mafanikio kwa kubeba makombe na pesa itapatikana, lakini Woodward anaonekana japo naye anataka makombe ila anaamini sana kuhusu biashara nje ya uwanja, Woodward anaamini kuhusu mauzo ya jezi na matangazo ndio maana ananunua wachezaji wa kuuza jezi.

Arsenal kuna bwana aitwaye Ivan Gazidis, Ivan yuko tofauti sana na Woodward. Anajua soka, anajua kutengeneza timu na ni Ivan na Wenger ambao walikuwa wakifanya kazi bega kwa bega kuhakikisha Gunners wanaleta wachezaji sahihi. Naamini Arsenal hawatachukua muda kukaa vizuri baada ya Wenger kuondoka kama United walivyohangaika, tusubiri tuone.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here