Home Kimataifa Kwenye sanduku la Ballon d’Or kura za Salah zitalindwa kweli?

Kwenye sanduku la Ballon d’Or kura za Salah zitalindwa kweli?

15043
0
SHARE

Hakuna kitu kinachotafuna nyoyo za watu kama chuki na unafiki. Walio wengi hawapendi ukweli wa kile wasichokipenda uzidi kudumu. Tukiachilia ushabiki wetu na unazi tulio nao Mo Salah amekuwa na msimu bora kuzidi mchezaji yoyote ndani ya EPL.
Ametwa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi mara 3 na hii inadhihirisha wazi kuwa DALILI YA MVUA NI MAWINGU. Najua roho zinawauma hasa ndugu zangu upande wa pili wanaotokea mashariki mwa Jiji la Liverpool wakipitia mji wa Warrington umbali wa kilometa kama 50 sawa na maili 31 na wale vibaraka wa Mrusi waliomtelekeza. Enewei

Kinachonisikitisha zaidi ni kuamini kuwa mchezaji bora lazima timu yake ipate mafanikio. Huu ni uchuro ambao Sepp Blatter ataulizwa na malaika wa Michezo mbinguni. Walio wengi wanaamini ili ubebe Tuzo ya Mchezaji bora wa Dunia lazima timu yako itwae Makombe makubwa kama UCL. Wanasahau Rivaldo alibeba tuzo hiyo na kumwacha nje Andy Cole na Dwight York na Beckham waliobeba makombe manne kwa msimu.

Hizi kelele za kigezo cha mafanikio zimeshika kasi kwenye utawala wa Messi na Ronaldo. Kwa kuwa watu walishindwa kuteniganisha uwezo wao ikabidi kigezo cha mafanikio kitumike kujua Tui la Nazi na Maziwa. Kama naiona vita ha timu kiba na timu Mond. Ukiwagusia hao watu ni sawa na umepiga jiwa mzinga wa nyuki. Enewei

Ronaldo ni mmoja kati mchezaji bora kabisa wa muda wote. Najua mshindani mkubwa wa Salah ni Ronaldo. Ronaldo hana cha kupoteza. Najua anatamani Ballon D Or ya 6 ili kumpoteza mpinzani wake. Lakini nafsi yangu inaamini sio jipya kwake. Tayari tunaamini ni bora. Ballon D or 6 haiwezi kubadili chochote wala haiwezi kumfanya mashabiki wa Messi wampende. Kwa Ronaldo na Messi inatosha mazee. Au mnaonaje? Achukue mwingine sasa? Soka sio lao tu. Wakaushe tu

Mo Salah amekuwa na msimu bora zaidi kuzidi hao Messi na Ronaldo (mawazo yangu). Naposema msimu bora simaanishi makombe namaanisha uwezo, juhudi binafsi na msururu wa ufanisi chanya. Ronaldo kufunga magoli mengi ya UEFA pekee bado haimaanishi amekuwa msimu bora kuliko Salah.

Niwarudishe nyuma kidogo.

Mwaka ya 1986 kulitokea mshangao mkubwa sana. Ukuta maarufu uliojulikana kama Eastern Bloc yaani Mwamba ya Mashariki ulitawala magazeti mengi ya Ulaya. Walitokea vijana watatu ambao walishangaza dunia Oleg Blokhin, Alexander Zavarov wakiongozwa na Igor Belanov. Belanov alitwaa tuzo ya Ballon D Or mbele ya Garry Lineker na wachezaji wengine wakubwa.

Linekar alikuwa na mafanikio mengi sana kumzidi Belanov. Lineker Alitwaa tuzo ya mchezaj bora wa mwaka England, tuzo ya mchezaji bora wa waandishi wa habari, mpira wa dhahabu kombe la dunia, Tuzo ya Onze, alimaliza ligi ya magoli 30 kwenye michezo 41, alibeba kombe la Rous akiwa na timu ya taifa, pia alikuwa mfungaji bora wa ligi.

Belonov alikuwa na magoli 11 tu, na alitwaa kombe dogo la washindi wa UEFA, walifungwa fainali kombe UEFA Super Cup, na kubeba kikombe cha Soviet. Mimi siamini sana kwamba lazima eti Ubebe Uefa ndio uwe bora. Mbona Mwaka ule Victor Pițurcă akiwa na Steaua Bucharest waliifunga Barcelona kwenye fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya na hakuitwa hata kwenye orodha ya wachezaji bora watatu? Tena alibeba kombe la Romania, akabeba ligi ya Romania, akabeba Uefa Super Cup na klabu bingwa, lakini Belanov akabeba.

Kinachohitajika sio mafanikio ya timu ila burudani uliyoitoa kwa mashabiki. Mambo unayofanya kwa mwaka mzima. Hata tukisema leo Salah tuweke mafanikio yake lazima pia tuangalie na yale anayofanya uwanjani na sio kile kinachokwenda kwenye kabati. Ameisaidia Misri kwenda World Cup kwa kufunga magoli matano na kuwa mfungaji bora. Ameisaidia Liverpool kwa kiasi kikubwa. Liverpool ambayo kila mtu alijua ni tia tia maji. Wakati anatokea Roma wengi tulimwona mshamba tu kaja mjini. Leo hii hakuna anayetaka kukutana nae.

Haijalishi unacheza wapi, mashindano gani lakini ukifanya vyema unahitaji pongezi. Kwa mfano Belanov alianzia Odessa, SKA na Chernomorets. Akiwa na miaka 24 akajiunga na Dynamo Kyiv mwaka 1985 na mwaka ule ule akatwaa Ballon D Or. Hawakuangalia alianzia soka wapi na yupo wapi ila kwa kuwa aliwakosha nao wakaamua kumkosha.

Natamani sana Salah abebe tuzo hii. Amecheza vizuri sana. Bila shaka ni wakati wa kuwapa moyo vijana wengine sio kila siku wale wale tu. Mbona Belanov aliinuka mbele ya Akina Carrasco walioipeleka Barcelona kucheza fainali ya klabu bingwa kule Sanchez, Seville?

Mbona aliwakalisha chini akina Michael Platin? Platin alibeba Kombe la Serie A, alikuwa na magoli mengi kuliko Belanov, alishika nafasi ya tatu kombe la dunia na mwaka mmoja nyuma yake alitwaa Ballon D Or mara 3 mfululizo lakini bado hakuna aliyefumbia macho kipaji cha Belanov? Kwanini isiwe kwa Salah pia? Au nao wana gubu kama ndugu zangu wanaoamini kila ng’ombe ni wa mmasai?

Au mmeshasahau kama Mathias Sammer 1996 aliwashangaza De lima Na Shearer?

Kwenye takwimu za magoli aliachwa mbali sana. Hakuwa na mafanikio yeyote makubwa. Alifunga magoli matatu tu kwenye ligi. Shearer alikuwa na magoli 31 na alitwa kiatu cha dhahabu kwenye michuano ya Euro, na alikuwa mchezaji bora namba 3 duniani kwa mujibu wa Fifa. De lima alikuwa mchezaji bora duniani wa Fifa na namba mbili alikuwa George Weah. Si wote hawa Sammer aliwabwaga?

Ballon D Or sio tuzo ya mfungaji bora, sio tuzo ya mchezaji mwenye vikombe vingi ila ni tuzo ya mchezaji aliyefanya vyema zaidi na kuwakosha wengi licha ya ushabiki na historia zao. Je kwanini wamdhulumu salah? Au kisa mwarabu? Kama wilishindwa kuvumilia kwa George Weah tunaomba na mwaka watulie hivo hivo tuwakune. Ni muda wa Afrika pia. Sio kila siku wao.

Kama hawatompa itakuwa unafiki tu. Kuna wale waliopika uji mwingi wakati hawana maziwa na sukari wanakwambia tukibeba kombe la Dunia fulani atapata nafasi ya Ballon D Or. Shame on You, nani kawaambia??. Naona mnatafuta Tuzo kwa mechi 7 za Kombe la Dunia? Mtu amepambana mechi 38 za ligi leo mnapitia vichochoroni kwenda mjini mnasema nyie ni madereva wa Mabasi makubwa?

Messi na Ronaldo kwa sasa inatosha zamu ya wadogo zenu. Hata akina Kaka na Ronaldinho waliwapisha pia. Time for Afrika Now… najua mawakala ndio wale wale wale vibaraka wa Nike na Addidas ila sio mbaya Hongera Salah kwangu mimi ndie mshindi

Imeandaliwa na Priva Abiud. Unaweza kunifollow instagram (Privaldinho) pia usisahau kusubscribe Youtube Channel ya Dauda Tv. Asante.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here