Home Kitaifa Ibrahim Ajib anapaswa kujifunza kwa Mhilu ili awe mchezaji bora Yanga

Ibrahim Ajib anapaswa kujifunza kwa Mhilu ili awe mchezaji bora Yanga

12379
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

IBRAHIM Ajib ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, lakini si rahisi kwake kuwa mchezaji kamilifu kama hatoachana na mchezo wake usiozingatia nidhamu.

Kwa kipindi chote cha kwanza alipoteza mpira zaidi ya mara tano-kwa kunyang‘anywa kizembe na kupiga pasi zilizokosa mwelekeo. Ajib ni kama Paul Pogba-hajitumi vile inavyopaswa na wanapocheza angalu kwa jitihada kidogo utapenda kuwatazama. Anapaswa kujituma zaidi ili afikie malengo yake.

Nadhani huu ni wakati wa kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa kumsaidia huyu kijana, amwambie anapaswa kucheza kwa mtazamo wa kwenda mbele, apunguze uvivu, apunguze kupoteza mpira, awe makini katika upigaji wake pasi.

Ajib kama anataka kuendana na sifa anazopewa ‘mchezaji mwenye kipaji kikubwa’ ni lazima akubali kujibadilisha na kwa dunia hii ya sasa anaweza kupata kumbukumbu za michezo ambayo amepata kucheza.

Kwa kuanzia anaweza kuanza kutazama makosa yake katika mchezo wa playoff wa Caf Confederations Cup dhidi ya Wolaitta Dicha ambapo alipoteza sana mpira. Alicheza kivivu jambo ambalo haliwezi kumfanya awe bora zaidi.

Kwa wakati huu, Donald Ngoma, Amis Tambwe wakiwa na majeraha ya muda mrefu, wengi waliamini Ajib ataibeba Yanga katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza, lakini ni kijana mdogo, Yusuph Mhilu aliyeleta uhai katika safu ya mashambulizi.

Mhilu alionekana kucheza kwa kujituma mno licha ya kuwa na uzoefu mdogo aliweza kucheza kama mshambulizi hatari mbele ya walinzi wa Dicha. Alisimama kati ‘kiukakamavu‘ na mara nyingi alikimbia vizuri eneo lote la mbele-hasa upande wa kulia. Kuhaha kwa kijana huyo kulitoa nafasi ya Rafael Daud kuingia vizuri eneo la penalti la timu ya Dicha.

Mhilu alikuwa mchezaji bora wa mchezo huo ulipigwa Jumamosi iliyopita, na pengine sasa anastahili kuanza kikosi cha kwanza. Akiendelea kujituma bila shaka atafuata haraka nyayo za Simon Msuva ambaye wakati anaingia Yanga, Agosti, 2012 alikuwa na makosa mengi kiuchezaji-hasa kutazama chini wakati anapomiliki na kukokota mpira.

Mhilu anakimbia akitazama kila upande, bado anapaswa kurekebisha upigaji wake wa pasi ya mwisho-kusoma kugha ya mwili ya mchezaji anawetaka kumpasia na nafasi ya mlinzi wa timu pinzani. Ajib anaweza kutazama upya mchezo wao uliopita ili kuona jinsi kijana mwenzake alivyojituma na kuipa uhai timu.

Nilimuona Nsajigwa wakati akichezea Tanzania Prisons na kwa misimu yake saba ya mafanikio Yanga, pia nakumbuka namna alivyokuwa akisifiwa na mtangazaji wa zamani wa kandanda nchini Juma Nkamia wakati wa michuano ya Tusker Cup mwaka 2001 akiwa Tukuyu Stars mlinzi huyu wa zamani wa Taifa Stars alikuwa imara kutokana na ‘tabia yake’ ya kujituma uwanjani na kufuata maelekezo hivyo naamini anaweza kukaa na Ajib kama rafiki na kumshauri.

Ajib anajua kufanya ‘dribbling’  lakini tatizo lake ni kwamba anafanya hivyo bila kwenda eneo la hatari la timu pinzani, huku pasi zake za kurudi nyuma mara nyingi zikipotea au kukosa mwelekeo sahihi jambo ambalo ni hatari kwa timu yake. Anapenda kucheza mchezo rahisi hilo si jambo baya lakini anapaswa kufanya hivyo akiingia katika eneo la hatari kama alivyokuwa akifanya Mhilu.

Uchezaji wake unaweza kuamua ‘fomu’ ya timu nzima-kucheza vibaya ama vizuri. Ana uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za kufunga, na pale timu inapocheza vizuri naye atakuwa na nafasi ya kuwa bora zaidi. Amekuwa akijaribu pia kupiga mipira ‘iliyokufa’ lakini kukosa kwake mazoezi ya kupiga mipira hiyo kumemfanya aonekani si mpigaji mahiri. Kama atajibidiisha zaidi katika viwanja vya mazoezi atakuwa na nafasi ya kuifungia magoli muhimu timu yake na hivyo kuendelea kuwa bora.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here