Home Makala Zlatan apokonywa gari na Mino Raiola

Zlatan apokonywa gari na Mino Raiola

11155
0
SHARE

Sehemu ya 5
Ilipoishia…
Mapema kabisa Zlatan alifika na Porsche yake kali, akiwa amepiga koti moja matata la Gucchi. Wakiwa wanamsubiri Raiola, Zlatan alipigwa na bumbuwazi baada ya kumuona Raiola. Raiola aliingia akiwa amevaa ovyo sana, yaani alionekana wa kawaida mno.

Raiola alikuwa amevaa tisheti nyeupe na suruwali jinsi. Alikuwa amevaa kihuni uhuni tu kama mshkaji vile. Zlatan akahamaki kwa hasira, kama kawaida yake kwa kuwa alikuwa mwepesi wa hasira akafoka sana, akasema “sasa huyu? Ameambiwa sisi tunafanya kazi ya kuuza maparachichi hapa? Amemfuata nani hivi? Na anataka nini? Ana njaa au shida ya hela? Siwezi kuongea na matapeli mimi.

Akamuuliza Maxwell “Atatununulia nini huyu? Zlatan akasonya akasema hawa wana njaa na hatushindwi kuwanunulia chakula. Zlatan akamuita mhudumu aje kuwahudumia. Raiola akajibu kwa dharau agiza wewe nitalipa mimi.

Moyoni Raiola akajua pale hali ishaharibika. Alikata tamaa, kilichobaki ilikuwa kumvuruga au kumteka Zlatan kisaikolojia. Raiola Akatoa makabrasha yake kibao kwenye begi, akamfungulia mikataba kama mitano hivi, wa kwanza ulikuwa wa Christian Vieri, alikuwa na magoli 24 mechi 27, Filippo Inzaghi magoli 20 mechi 25, David Trezeguet magoli 20 mechi 24, kisha akamgeukia Zlatan akamwambia “sasa wewe, una magoli 5 kwenye mechi 25 utaniambia nini? Utauzwa kiasi gani? Nani atakutaka mchezaji wa hovyo kama wewe? Tena kibaya zaidi unanijibu mimi kwa nyodo? Hebu kaa chini kwanza tuongee?

Zlatan akasita kidogo, akiwa anashangaa Raiola akafunga begi lake, akamwita kijana wake ampe simu. Raiola akapiga simu, na mazungumzo yalikuwa kama hivi “ndiyo nipo nae hapa ila analeta jeuri” Baada ya sekunde kadhaa akasema, sawa bosi nitajitahidi kuongea nae. Alivyokata simu akamwambia Zlatan hiyo ni simu ya bosi wa Juve kaa chini tuongee kama hutaki pia waweza kwenda.

Zlatan akawa anamwangalia sana huyu jamaa lakini akawa amekosa majibu. Raiola akamwambia, pesa sio kila kitu. Usiwe na tama ya fedha ukiwa bado huna jina kubwa. Cha msingi tafuta umaarufu na jina kubwa kwenye soka kabla ya mambo mengine.

Baada ya mazungumzo ya muda mrefu walifanya makubaliano kwa pamoja na kukubaliana kufanya kazi. Kabla ya yote Raiola alimwomba Zlatan Kwanza ampatie funguo zake za gari, pili akamsihi kuwa kuanzia siku ile aachane kabisa na maisha ya ubishoo kwa kuvaa nguo zenye fasheni za kimarekani. Jukumu Zlatan alilopewa ni kuvaa suti tu.

Alimisihi aishi kama mtu msomi na sio mhuni mhuni. Hii ilikuwa kazi sana kwa Zlatan kwa kuwa tayari yeye amekulia maisha ya kihuni tokea utoto wake. Zlatan aliona kama jamaa na anamzingua sana.

Zlatan aliwaza sanaa kuhusu ile orodha ya mikataba ya Raiola. Akajiona mpumbavu. Akagundua ameridhika na maisha na amekuwa mzembe sana ndio maana hafungi magoli kadiri iwezekanavyo. Siku zote kwenye maisha huwa hatukosei kuchagua njia ila tunakosea kuchagua kasi ya safari yetu na tunahangaika na mambo mengine ambayo hayatuhusu.

Kama wewe ni mchezaji wa kitanzania fanya uamuzi sasa kuwa unataka kwenda wapi na hapo ulipo ni mbali na unapotaka kwenda au lah. Usipende kuridhika na mafanikio uliyopata ikiwa kuna mafanikio mengine zaidi ya hayo. Kama unapanda ngazi hakikisha unafika mwisho au kilele cha ngazi. Usiogope ni umbali gani umekwenda, ila hakikisha unafika kileleni. Vitu alivyokosa Zlatan katika maisha yake ya soka pale Ajax ni mtu atakayemsukuma kwenda mbele. Je wewe umechagua watu wa aina gani nyuma yako.

Raiola alikubali kusimama nyuma ya Zlatan kwani aliamini kuwa ngazi ya Zlatan ni ndefu na yenye mafanikio. Alikuwa kila siku anampigia simu saa 11 asubuhi na kumwambia “we mpuuzi amka ufanye mazoezi” kuna wakati Zlatan aliona kama jamaa anamnyima uhuru wake.

Na hili pia lipo kwa wachezaji wetu wa Tanzania wana tabia ya kuwakataa wale watu wanaosimama nyuma yao au kuwapuuzia wale waliosukuma kwenda mbele kwa kuwa wanajiona wamefika. Usiwakatae wale wanaokusukuma kwenda juu hata kama umewazidi mafanikio maana mafiga haya thamani ya chakula kinachopikwa jikoni.

Zlatan baadae aligundua kuwa sauti moja huanzisha nyingine. Alianza kugundua kuwa jina lake lilikuwa likiimbwa sana uwanjani kuliko mchezaji yoyote hasa baada ya ujio wa Raiola katika ufanisi wake.

“Kuna wakati nikahisi Yule mjinga amehonga mashabiki wanishangilie kinafiki” alisema zlatan. Zlatan akagundua kiwango chake kimepanda sana mara baada ya kuona magazeti ya ulaya yakitangaza sana habari zangu. Kila nikipita mtaani nasikia habari zangu tu. Hii changamoto kwa Akina Ajib na Kichuya.

Mambo yamwendea Mrama
Msimu uliofuata, ugomvi mkubwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kati yake na Mido ulipamba moto. Ilifika kipindi Mido akaomba kuuzwa au Zlatan aondoke. Tafrani kubwa lililipuka mwaka 2003 kwenye mechi dhidi ya mahasimu wao wakubwa Feynoord. Hassan Mido ambaye amewahi kukipiga Tottenham aliwekwa benchi kwenye mchezo huo. Mido anasema “nilikuwa na hasira sana sikuanza mchezo ule.

Nilipoingia uwanjani tulikuwa chini magoli mawili. Nilikuwa namfokea kila mchezaji uwanjani. Hata nilipomfokea Zlatan nae alinifokea. Nikachukia kitendo cha Zlatan kunijibu vibaya kwani sikuwa na lengo baya ila nilitaka kufanya vile ili kila mtu ajitume tupate matokeo.

Niliona Zlatan kama anataka kuanzisha ugomvi. Wachezaji wote walikaa kimya kwa sababu walielewa lengo langu ila Zlatan akajitia ujeuri na kujiona nunda. Nilipewa mpira na Zlatan alikuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga ila sikumpa pasi makusudi kwa sababu tayari lengo langu la kufoka lilitengeneza chuki. Zlatan nae alipopata mpira aligoma kunipa pasi. Kuna wakati nilitoa mpira nje makusudi. Mpira ulipoisha nilimtukana Zlatan matusi ya nguoni, Zlatan nae alimrudishia tusi lile lie.

Baada ya majibizano Mido akakasirika akamrushia Zlatan mkasi aliokuwa ameshikilia usoni na hamaki kubwa ilizuka na baada kurusha mkasi ule kila mtu alikimbia kwa kilichotokea.

Unataka kujua kilichoendelea basi fuatilia makala zijazo.

Imeandaliwa na Privaldinho (Instagram)

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here