Home Kitaifa Ngumu Kumeza imezigusa Simba na Yanga

Ngumu Kumeza imezigusa Simba na Yanga

10175
0
SHARE

Vilabu vya Tanzania na timu yetu ya taifa vinapotolewana na kushindwa kufuzu hali ile huwa haitokei kwa bahati mbaya ila kwa kuzidiwa mipango na wapinzani. Wapinzani wetu ni wajanja kupekuwa taarifa zetu mapema na kujua uimara wetu na udhaifu wetu kisha taarifa zinatupwa kwenye vitengo mbalimbali kwa ajili ya kufanyia kazi.

Wakati Yanga wanaivaa Township ninauhakika walikuwa hawajui lolote kuhusu timu ile ya Botswana zaidi ya kujua wanatoka nchi gani na mji tu wanaocheza, ni watu wa namna gani, wana watu gani hatari hawakujua, hali kadhalika kwa Simba hali ilikuwa hivyohivyo.

Timu zetu zilipita hata raundi iliyopita kutokana na wapinzani wao kuwa dhaifu, wale St. Louis na Gendarmerie wangekuwa imara kidogo tu huenda timu zetu zingekwamia pale. Tulihamasika kutokana na historia za nchi zile kimpira.

Mpira wa kisasa lazima timu ziwekeze kwenye teknolojia pamoja na kitengo cha ujasusi wa kujua wapinzani wanacheza aina gani ya mifumo, mbinu za kiufundi ikiwa ni pamoja na uwezo wa kutoa vikosi muda mfupi kabla ya mchezo hii inapelekea mpinzani kutojua timu inakuja na mfumo gani kutokana na kuangalia aina ya wachezaji walioanza.

Kitengo cha ujasusi ndani ya timu kazi yake kubwa ni kujifunza, kufikiri na kuelewa mambo waliyokuwanayo timu pinzani na ni mara chache huelezwa kama taarifa au jinsi ya kupata taarifa.

Dereva taxi mmoja anasema alikuwaga anauza CD na VHS za mechi za vilabu vya Tanzania kwa vilabu vya nje kabla ya mapinduzi ya YouTube. “Kuwa na mechi za Simba na Yanga kwa timu ngeni kutoka nje nilikuwa natengeneza dola 2000 kwa VHS au CD, teknolojia imetuharibia sana hawa Township au Al Masry zamani ilikuwa lazima wangenitafuta wiki moja au mbili kabla ya mechi.”

Intelijensia inahusiana na mamuuzi yatakayochukuliwa na pili maamuzi hayo yatatokana na utabiri utakaofanya kutoka kwenye taarifa zilizokusanywa. Township Rollers na Al Masry walifanikiwa kupata matokeo chanya pale kwa mchina kutokana na vitengo vya kukusanya taarifa za kutosha za Yanga na Simba kisha kuzigeuza elimu kwa wachezaji wao.

Jamaa mmoja anasema hata mechi ya Simba kuchezwa saa 12 jioni ilikuwa ni msukumo kutoka kwa mafarao ambao waliketi chini na baadhi ya wajumbe na kununua fikra zao ambao walipitisha mchezo huo uchezwe saa 12 jioni na wababe hao wachache walipendekeza kwenye mawazo yao yakapita kitu kilichotoa nafasi kwa mafarao.

Staili ya maisha ya namna hii ndiyo inapelekea mpira wetu kutopiga hatua kila siku kutokana na vinega wachache kuwaza matumbo yao na sio uzalendo. Kwa upande mwingine ufinyu wa kufikiria mapato ya mlangoni kuliko kufikiria kusonga mbele ndiyo kumeigharimu Simba.

Visingizio vya viongozi wa Yanga wanajifichia kwenye kivuli cha wanakikosi kidogo kutokana na majeruhi walionao kwenye timu ndio maana wametolewa kwenye klabu bingwa lakini uhalisia angalia historia ya miaka 10 iliyopita utagumndua majeruhi msimu huu ndio kimbilio lakini historia inaonesha wamevuka mara moja tu kati ya hizo kuingia kwenye makundi.

Kocha wa Township alikaririwa akisema kuwa, aliwafuatilia Yanga katika michezo tisa kabla ya kukutana nao lakni Lwandamina alikuwa amebung’aa tu na ligi ya bongo na kombe la FA halafu unategemea uingie makundi ya ligi ya mabingwa kwa staili hiyo? Kwa ubora gani wa ligi hadi uchukulie sawa maandalizi ya kuiendea mechi ya Njombe Mji iwe sawa na Township au Al Masry?

Simba na Yanga hawakufanya maandalizi kama yale tunayoyaonaga kwenye mechi yao. Waliwachukulia kawaida Al Masry na Township kama timu za kawaida zisizo na historia kubwa hivyo wakaona hakuna haja ya kufanya maandalizi kama wanavyofanyaga pindi wakipangwa na Zamalek, Al Ahly ama TP Mazembe.

Ngoja uone maandalizi watakayofanya kwenye mchezo wa ligi, wengine wataenda Pemba na wengine Unguja au Bagamoyo. Bonus kubwa wataahidiwa, malimbikizo yatalipwa, yote ni kwa ajili ya kuwafurahisha wanachama na washabiki zao.

Viongozi wa timu hizi hawaoni mbali na ndiyo maana wadhamini toka nje ya Tanzania ni vigumu kuja kudhamini timu hizi sababu kubwa historia katika michuano ya kimataifa ina wahukumu. Kuna wakati unaweza kusema sikio la kufa halisikii dawa, hakuna mwaka ambao timu hizi zimepata timu nafuu kuelekea katika hatua ya makundi kama wakati huu.

Mwaka 2015 baada ya timu yetu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kula wiki kule Birda Algeria, kaka yangu Charles Boniface Mkwasa akiwa kocha wa kikosi cha stars alilalamika kwamba kwa nini hawa Caf kila mwaka wanatupangia timu kubwa kutoka Afrika Magharibi au Kaskazini si katika ngazi ya vilabu au timu ya taifa.

Nahisi Caf walisikia kilio chake, msimu uliopita Yanga ilitolewa na Zanaco ya hapo Zambia unatembea kilomita chache tu kutoka Tunduma, msimu huu walipangiwa Watswana wazee wa ‘makhitikhiri’ wamewatupa nje ya mashindano na kuwakosesha mabilioni ya fedha na sasa wameangukia kwa Wahabeshi, tusubiri tuone ya Mungu mengi tayari wenye timu yao wameanza kujazana ujinga kupitia hesabu nyepesi za kurahisisha kwamba ukigawa kwa mbili basi inaweza kukubali kote.

Ufukara wa kufikiri unaanzia hivi, hawa Wahabeshi walisumbuliwa sana na Zimamoto ya Zanzibar ambao Yanga waliwafunga 5-0 katika michuano ya Mapinduzi hivyo Yanga kapata ubwete kuelekea katika hatua ya makundi ila wanasahau Wahabeshi hao wamewaondoa mashindanoni magwiji wa Afrika Zamalek ya Misri.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here