Home Kitaifa Mwanasheria alivyochambua hukumu ya makamu wa Rais TFF

Mwanasheria alivyochambua hukumu ya makamu wa Rais TFF

4827
0
SHARE

Baada ya kamati ya maadili kumfungia makamu wa rais wa TFF Michael Richard Wambura kumekuwa na mijadala mingi miongoni mwa wadau wa soka, baadhi wakihoji kama kanuni na sheria zilifuatwa kulingana na namsha shauri linalomhusu Wambura lilivyoendeshwa kwa haraka na kutolewa hukumu.

Kwa mujibu wa tff, Machi 13 2018 Wambura alipewa wito ili afike mbele ya kamati ya maadili machi 14, 2018 kwa ajili ya kutoa maelezo juu ya tuhuma tatu zilizokuwa zinamkabili, machi 15 tff ikatangaza hukumu ya kumfungia maisha Wambura kujihusisha na shughuli za soka.

Baadhi ya wanasheria wametoa mtazamo wao juu ya kinachoendelea juu ya sakata hilo, Alex Mgongolwa ni mmoja wa mawakili waandamizi nchini ametoa ufafanuzi juu ya suala zima la kamati ya maadili inavyotakiwa kufanya.

“Kuna kuwa na kamati ya maadili lakini kuna kuwa na kamati ya rufaa ya maadili ili kumpa nafasi mtu ambaye hajaridhika na maamuzi ya kamati ya maadili kuweza kukata rufaa kwenda kamati nyingine. Ni mfumo tu wa utoaji haki ndio ulikuwa unatuongoza katika kutengeneza kanuni hizi, dhamira ya kamati ya maadili, kamati ya nidhamu ni mfumo unaoitwa nusu ya mfumo wa mahakama.

“Mfumo wa nusu ya mahakama ni ambao unatoa haki na unafuata kanuni za msingi za utoaji haki kwa mfano haki ya kusikilizwa, kutoa ushahidi, na ushahidi wenyewe kufanyiwa upembuzi na kufikia uamuzi. Kwa hiyo kwa maana ya kamati, dhamira ni yake ni kutoa haki lakini kwa maana ya utendaji na utekelezaji inadhamiriwa pia kamati hizo zitende haki.

“Makosa yanayopelekwa kwenye maadili ni vizuri ikafahamika si kila kosa ni la maadili, lazima utofautishe makosa ambayo ni ya kimaadili kwa maana yale yanayowabana viongozi wawe katika tabia ambayo haiudhalilishi mpira hayo ndiyo maadili ambayo yameainishwa katika kanuni. Kama kiongozi ukikiuka maadili hayo unapelekwa kwenye kamati ya maadili. Kama kosa ni la kinidhamu unapelekwa kwenye kamati ya nidhamu kama kosa linahusiana na sheria za nchi (linahusiana na mambo ya jinai) unapelekwa katika sheria za mfumo wa nchi.

“Ni vizuri ikafahamika miundo hiyo ipo hapo kwa ajili ya kutenganisha mamlaka na madaraka.

Namna kesi ya kumfungia Michael Richard Wambura ilivyoeneshwa kwa jinsi ulivyofuatilia unafikiri taribu na kanuni zilifuatwa?

“Kwa kuwa jambo hilo bado lina nafasi ya kwenda kwenye kamati ya rufaa, nisingependa kulizungumzia sana lakini ambacho ningetaka nizungumze kwa wakati huu lililopo ni kwamba kanuni za msingi za uendeshaji mashauri ya kutoa haki ni lazima zifuatwe na tunavyosikia ni kwamba kanuni hizo zilifuatwa. Kwa hiyo kwa yeyote yule ambaye hajaridhika na uamuzi huo ndio maana kanuni hizo zimetoa nafasi ya kwenda kwenye rufaa na hata rufaa hiyo ukiwa hujaridhika na maamuzi bado mfumo wa utoaji wa haki wa mpira wa miguu unatoa nafasi kubwa zaidi kwenda ngazi nyingine mpaka Caf.

“Kwa maana ya kukosea, mimi kama mwanasheria chombo kukosea katika utoaji wa maamuzi ni kitu ambacho nakitazamia, ni cha kawaida na ndiyo maana kunakuwa na ngazi mbalimbali za kukata rufaa na chombo kile kinachosikiliza rufaa kinajikita katika kuona kanuni za utoaji haki zilifuatwa? Huwezi ukalijua hilo mpaka mlalamikaji akueleze kwamba anachokilalamikia ni nini?

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here