Home Kitaifa Pointi 23 kati ya 30 ugenini, pointi 21 mfululizo, Lwandamina ni tishio

Pointi 23 kati ya 30 ugenini, pointi 21 mfululizo, Lwandamina ni tishio

13433
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

USHINDI wa michezo saba mfululizo ambao mabingwa mara tatu mfululizo na watetezi wa taji la ligi kuu Tanzania Bara-Yanga SC wameupata kwa hakika ni ‘habari mbaya‘ kwa wale ambao waliamini matatizo ya kiuchumi yatawakwamisha mabingwa hao mara nyingi zaidi bara.

Kikosi hicho cha Mzambia, George Lwandamina kilidhaniwa kitaanguka mahala, lakini ushindi katika uwanja wa Samora, Iringa, Nangwanda Stadium, Mtwara na ule wa FA Cup dhidi ya Majimaji FC katika uwanja wa Majimaji, Songea unadhihirisha nisemacho mara kwa mara- kuwa mabingwa hao watetezi ‘wana tabia yao wenyewe‘ ambayo imeshawasaidia mara kadhaa kutwaa mataji ya ligi ‘wakati ambao palidhaniwa watashindwa.‘

Pointi 21 bila kuangusha hata moja

Baada ya kuchapwa 2-0 na Mbao FC katika uwanja wa Kirumba, Mwanza, Desemba 30, mabingwa hao watetezi wamemudu kuzishinda Ruvu Shooting, Azam FC, Lipuli FC, Njombe Mji FC, Majimaji, Ndanda FC na Kagera Sugar FC. Ushindi huo usio na kikomo umewafanya kufuta gap la pointi nane walilokuwa wameachwa na viongozi wa ligi kufikia mwisho wa Desemba, 2017.

Kama wataifunga Stand United kama ‘navyotaraji‘ Jumatatu hii katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kikosi cha Lwandamina kitakuwa pointi sawa na vinara wa muda mrefu wa ligi-mahasimu wao Simba SC.

Kushinda mchezo wa nane mfululizo na kukusanya alama 24 pasipo kuangusha hata pointi kwa hakika si jambo dogo. Yanga wanashinda licha ya kwamba hawachezi mchezo wa kuvutia. Wanapaswa kuendelea na mkakati wao wa -pointi tatu kwanza.

Pointi 23 kati ya 30 ugenini, kwa nini wasitwae taji la 4 mfululizo?

Ndiyo, Yanga hawachezi mchezo mzuri katika kila mechi, lakini wamekuwa na matokeo bora katika michezo yao kumi waliyokwisha icheza ugenini. Ikiwa bado wanakabiliwa na safari nne ngumu, Morogoro vs Mtibwa Sugar FC, Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City FC, kisha dhidi ya Mwadui FC huko Shinyanga, mabingwa hao mara 27 wa kihistoria wamemudu kukusanya alama 23 kati ya 30 katika michezo yao kumi ya ugenini.

Waliangusha pointi mbili-mbili walipolazimisha sare ya kufungana 1-1 na Majimaji, na katika suluhu vs Singida United katika uwanja wa Namfua. Wamepoteza mchezo mmoja dhidi ya Mbao FC (mchezo pekee waliopoteza hadi sasa katika VPL msimu huu).

Kushinda kwao Njombe, Kagera, Shinyanga dhidi ya Stand United, Iringa, Chamanzi Complex, na dhidi ya Shooting ni kielelezo kingine kwamba-licha ya wachezaji, bechi la ufundi na wafanyakazi wengine katika timu kuendelea kukosa mishahara, bado wazo la ubingwa wa nne mfululizo linafanyiwa kazi-tena kwa umakini na tahadhari kubwa.

Matokeo mazuri katika viwanja vya ugenini na mfululizo wa ushindi tangu kuanza kwa mwaka mpya ni ‘tishio‘ ambalo linapeleka presha kwa Simba ambao wameangusha alama nne katika michezo mitatu iliyopita. Lwandamina anaweza akawa bado hajatengeneza alama ya mchezo wake lakini kwa namna mambo yalivyo tangu kuwasili kwake Desemba 2016, kunanifanya niendelee kuwa na subira juu yake.

Ameikuta Yanga ikiwa na majeruhi ya wachezaji muhimu kwa muda wote wa miezi yake 14 sasa, si hivyo tu, wachezaji hawalipwi kwa wakati, yeye pia akisotea mshahara wake wa miezi miwili iliyopita. Lwandamina amenifundisha pia jinsi ya ‘kujifunza kuhusu matatizo‘ kwani utulivu wake na imani anayoionyesha kwa wachezaji wake ni chachu ya kuwasahulisha matatizo ya nje ya uwanja wakati wa dakika 90‘ za mchezo.

Kitendo cha kocha huyo wa zamani wa Zesco United kuwaamini na kuwapa nafasi vijana kama golikipa Ramadhani Kabwili, Said Musa, na viungo kutoka kikosi cha pili Maka Edward na Yusuph Mhilu kinaonyesha ni jinsi gani, Lwandamina anavyoweza kuongeza upana wa kikosi chake kinachowakosa, Donald Ngoma, Thaban Kamusoko, Amis Tambwe.

Lwandamina ana kikosi kidogo, na hicho hicho amekuwa akienda nacho katika VPL, FA na ligi ya mabingwa Afrika. Pius Buswita, Emmanuel Martin wametokea kuwa wachezaji muhimu katika ufungaji wa magoli. Kabla hawakutarajiwa kuibeba timu kama inavyotokea sasa.

Ibrahim Ajib, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Said Juma Makapu wote hawa wanafanya vizuri kutokana na ‘msukumo‘ wa kupata matokeo kutoka kwa benchi lao la ufundi.

Pointi 3 kwanza

Kuna jambo niliwashauri Simba baada ya sare yao ya kufungana Mwadui 2-2 Simba. Nilisema, unapocheza ligi huku ukiwa na mtazamo wa kutwaa taji la ubingwa kuna wakati unapaswa kucheza mchezo wa kujilinda zaidi hasa pale mnapokuwa mkiongoza mechi.

Katika mchezo uliopita Yanga 3-0 Kagera, mabingwa hao watetezi mara baada ya kufunga goli la kuongoza dakika ya 53‘ kwa njia ya mkwaju wa penalti, walicheza kwa kujilinda zaidi kwa hofu ya goli hilo kusawazishwa.

Kagera walitawala mechi kwa dakika kama kumi hivi lakini walichoshwa na wachezaji tisa wa Yanga waliokutwa wakilinda lango lao. Walipochoka wakashambuliwa wao na kujikuta wakiruhusu magoli mengine mawili ndani ya dakika 13 za mwisho. Hii Ndiyo mbinu ya kushinda ubingwa, na Yanga hawaipuuzi, imewasaidia na itawabeba zaidi.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here