Home Kitaifa Himid anaamini Azam ‘wameteleza’ akiwakumbusha Yanga, Simba ‘mcheza kwao hutuzwa’

Himid anaamini Azam ‘wameteleza’ akiwakumbusha Yanga, Simba ‘mcheza kwao hutuzwa’

8973
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

NAHODHA wa Azam FC, Himid Mao Mkami anaamini katika soka ‘Mcheza kwao Hutuzwa’ mahala kokote pale duniani. Himid amesema hayo wakati nilipofanya naye mahojiano Alhamisi hii.

Kiungo huyo wa timu ya Taifa ya Taifa ya Tanzania mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi amezungumza mengi kuhusu mwenendo wa klabu yake msimu huu, pia akizungumzia ushiriki wa vilabu vyetu Yanga na Simba katika michuano ya klabu barani Afrika.

www.shaffihdauda.co.tz: Habari yako nahodha, unaendeleaje na maumivu (Himid alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya goti yaliyopelekea kupelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi na klabu yake).

Himid: Namshukuru Mungu naendelea vizuri. Hivi sasa nimeshaanza mazoezi na timu ‘kidogo kidogo’ nikiendelea hivi kwa uwezo wa Mungu naweza kurudi uwanjani mapema zaidi ya matarajio.

www.shaffihdauda.co.tz: Kama nahodha unadhani timu yenu mko katika njia sahihi wakati huu mkiwa nyuma kwa alama 12 dhidi ya viongozi wa ligi huku ikiwa imesalia michezo 12 kabla ya kumalizika kwa msimu?

Himid: Nafikiri tumeteleza  kidogo. Kusema kweli tumepoteza pointi nyingi ndani ya muda mfupi sana, lakini kilichotutokea sisi kinaweza kutokea kwa yeyote yule japo sio rahisi.

www.shaffihdauda.co.tz: Mlimaliza nafasi ya nne msimu uliopita, ikiwa ni mara yenu ya kwanza kuwa nje ya ‘top 2’ baada ya kufanya hivyo kwa misimu mitano mfululizo iliyoambatana na taji moja msimu wa 2013/14. Mwendo wenu si mzuri msimu huu, je, mnaporomoka? Nini unadhani kinapaswa kufanyika?

Himid: Nafikiri msimu uliopita ni tofauti kidogo na huu, kwa kuwa uliopita tulianza ligi kwa kusua sua zaidi. Msimu huu tumeanza vizuri na hatupo sehemu mbaya sana lolote linaweza kutokea. Nafasi bado tunayo kumaliza nafasi ya juu zaidi ya msimu uliopita. Cha kufanya ni kuendelea kupambana huku tukiamini tunaweza kufanya kitu msimu huu.

www.shaffihdauda.co.tz: Azam FC haijapata ushindi dhidi ya timu yoyote katika orodha ya timu tano za juu katika msimamo wa ligi kuu msimu huu. Katika michezo mitano ambayo tayari mmecheza dhidi ya Simba (mara mbili,) Mtibwa, Yanga na Singida mmefunga magoli matatu tu, unadhani nini kinapaswa kufanyika ili mfunge magoli ya kutosha hasa dhidi ya washindani wenu wa juu?

Himid: Nafikiri ni sisi wachezaji wenyewe na watu wote wa timu kujua nafasi ya timu na kilichotufanya tukawa juu huko nyuma ili tukifanye sasa na kuongeza zaidi. Kiukweli ni lazima upate pointi tatu dhidi ya timu za juu ili uwe na nafasi ya kuwa bingwa.

www.shaffihdauda.co.tz: Mpo robo fainali FA Cup (Azam FC vs Mtibwa Sugar FC)  naamani kama timu nyingine malengo yenu pia ni kutwaa kikombe hicho. Azam FC hamkupata nafasi ya kucheza Caf msimu huu baada ya kufanya hivyo kwa misimu mitano mfululizo. Unadhani mpo katika nafasi gani ya kutwaa ubingwa huo wa FA msimu huu na je, kama timu m-memiss lolote kutokucheza kwenu Caf msimu huu?

Himid: Lengo la klabu ni kufika fainali na kuchukua kombe. Hiyo ni nafasi iliyo wazi kwetu kupata tena nafasi ya kucheza mashindano ya Caf. Tunaamini hii ni nafasi yetu ya wazi hata ukitazama matokeo yetu tangu mwanzo wa michuano hii ni mazuri zaidi ya mashindano yote tuliyoshiriki/tunayoshiriki msimu huu. Naamini tutaendelea hivihivi hadi mwisho.

Tume-miss sana mechi za Caf maana ni nafasi nzuri kwa timu na mchezaji mmoja mmoja kujiuza, kama unavyojua watu wengi duniani wanafuatilia mashindano hayo.

www.shaffihdauda.co.tz: Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Caf msimu huu, timu za Yanga na Simba zitakuwa na michezo dhidi ya Township  Rollers ya Botswana na Al Masry ya Misri, unadhani wanakutana na wapinzani wanaostahili katika hatua hii ya kwanza?

Himid: Wapo katika mashindano ya Caf msimu huu, wanatakiwa wajitahidi kufika mbali zaidi ya tunapokwamiaga timu za Tanzania. Wamekutana na wapinzani wanaostahili kukutana nao ukizingatia hii ni michuano inayoshirikisha mabingwa kutoka katika nchi tofauti, kwa hiyo unatakiwa kuwa tayari kukutana na mpinzani yeyote. Maandalizi na utayari wao ndio utakaoleta tofauti.

www.shaffihdauda.co.tz: Huu ni msimu wa 20 tangu Caf ilivyoanza kutumia mfumo wa ligi ya makundi,  ni mara tatu tu timu za Tanzania zimewahi kufika hatua hiyo. Mara mbili Yanga (1998 ligi ya mabingwa, na 2016  Confederation Cup) na mara moja Simba (2003 ligi ya mabingwa), timu zetu zimekuwa zikiangushwa na nini ukizingatia wewe ni ‘muhanga’ mara tano mfululizo tena ukiichezea klabu moja?

Himid: Kwa mtazamo wangu naona huwezi kuwa na timu inayopata tabu kupata ushindi katika ligi ya ndani halafu ikafanikiwe Caf. Tunajidanganya. Nafikiri njia pekee ni kuandaa timu zaidi itakayopambana katika ligi ikiwa na kikosi kipana. Mfano, tazama barani Ulaya, timu kama FC Bayern Munich, Barcelona, Manchester City zina vikosi vyenye uwezo zaidi ya ligi za ndani, ni rahisi kwao kufanya vizuri hata katika Champions league.

www.shaffihdauda.co.tz: Inawezekana timu hizo za ulaya zinafanikiwa kutokana na ubora na upana wa vikosi vyao kama unavyosema, ila kwa nini timu kama Al Hilal na El Merreikh za Sudan, TP Mazembe ya DR Congo na sasa tunaona klabu za Afrika Kusini na Zambia zinafuzu kwa hatua ya makundi Caf. Kama suala la upana wa vikosi, Azam FC mmewahi kusuka vikosi vipana lakini kipi kiliwaangusha, Rabat, Khartoom, Beira, Tunis ambako mlikwenda kucheza michezo ya marejeano mkiwa na ushindi?

Himid: Ndio, hata timu za Afrika Kusini hivi sasa zimebadilisha ‘mentality’ kutoka kwenda mashindanoni na timu za kawaida hadi kwenda na timu za ushindani wa ukweli Caf. Timu za kiarabu zimekuwa changamoto kubwa kwetu. Wenzetu wametuacha mbali sana, wapo ‘serious’ katika kila kitu ndio maana matokeo yao hayadanganyi.

www.shaffihdauda.co.tz: Ni kweli ‘mcheza kwao hutuzwa’ katika soka la Afrika?

Himid: Ni kweli, si Afrika pekee ni dunia nzima.

www.shaffihdauda.co.tz: Unawakumbusha nini Yanga na Simba kuelekea michezo yao ya Caf, Jumanne na Jumatano ijayo?

Himid: Nafikiri wanajua nini cha kufanya, nawatakia kila la kheri na sina cha zaidi.

www.shaffihdauda.co.tz: Asante sana kwa muda wako

Himid: Asante pia, tuko pamoja.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here