Home Kitaifa Taarifa zimeifikia Yanga Lwandamina anataka kuondoka

Taarifa zimeifikia Yanga Lwandamina anataka kuondoka

11584
0
SHARE

Taarifa zimeanza kueneza kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari kwamba George Lwandamina anatakiwa na klabu ya Zesco United ya Zambia huku mkataba wake na klabu ya Yanga ukitarajiwa kumalizika mwezi Juni mwaka huu, Katibu Mkuu wa Yanga Charles Boniface Mkwasa amesema anachofamu ni kwamba Lwandamina bado ni kocha halali wa Yanga.

“Hizo habari hata mimi nimezisikia pia, kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya waandishi wa habari wamekuwa wakiniuliza. Ninachokifahamu mimi ni kwamba, George bado ni mwalimu wetu na mkataba bado unaendelea, pia yupo na timu mtwara kwa hiyo kama kuna lolote basi atatujulisha”- Charles Boniface Mkwasa.

Ikiwa mkataba wa Lwandamina na yanga unaelekea ukingoni, yanga hawastushwi na taarifa hizi?

“Kama kuna timu ina maslahi kuliko huku huwezi kumzuia na mara nyingi mtu anapofanya taratibu zake za kupata kazi nyingine huwa hatangazi, inapokamilika anakuja kuaga kwa hiyo siwezi nikasema kwa kuwa mwenyekuamua ni yeye lakini klabu na wanachama bado wana imani naye. Sasa anapokuwa anaamua inakuwa ni jukumu lake sisi hatuwezi kuingilia.

Kama ikitokea Zesco ikampa kile anachokihitaji, Mkwasa amesema bado maamuzi yatabaki mikononi mwa Lwandamina kuamua  afanye kazi wapi na Yanga haiwezi kumpangia wala kuingilia maamuzi yake.

“Siwezi nikasema lolote, lakini huwezi kumlazimisha mtu kufanya kazi lakini chaguo ni lake kuamua afanye kazi huku au kule, wapi kuna maslahi bora au wapi anaweza kufanya kazi kwa ufanisi mzuri. Kwa hiyo, sisi hatuwezi kumpangia wala kumsemea kwamba itakuwaje, yeye ndiyo mwenye maamuzi.”

Mkwasa amekanusha baadhi ya sababu zinazotajwa kuwa huenda zikapelekea Lwandamina kuikacha klabu hio, miongoni mwa sababu hizo ni uongozi wa Yanga kutotekeleza baadhi ya mapendekezo yake wakati wa usajili.

“Siwezi kusema kwamba kuna baadhi ya vitu vilipuuzwa katika mapendekezo yake wakati wa usajili kwa sababu suala zima la usajili tulifuata matakwa ya mwalimu sasa kama kuna changamoto nyingine hizo sizifahamu. Sisi kama klabu bado tuna nia ya kufanya kazi na yeye.”

Wameshaanza maandalizi kwa ajili ya kumwongezea mkataba mpya? “Bado muda upo kwa sababu mkataba wake nadhani unamalizika mwezi juni kama sikosei, kuna kamati inashughulikia masuala ya usajili kwa hiyo muda utakapofika watakaa kama kamati na kufanya tathmini kisha watakuja na tamko kwamba ataendelea au vinginevyo.”

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here