Home Kitaifa Mafanikio ya Msuva yanapogeuka changamoto kwa mdogo wake

Mafanikio ya Msuva yanapogeuka changamoto kwa mdogo wake

10940
0
SHARE

James Msuva ni mdogo wake Simon Msuva ambaye kwa sasa anakipiga kwenye klabu ya Difaa el Jadida ya Morocco, james ni miongoni mwa wachezaji wa mbao ambao wanafanya vizuri kwa sasa tofauti na wakati alipojiunga na klabu hiyo ya Mwanza ambapo alikuwa anaanzia benchi lakini siku za hivi karibuni amekuwa miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha kwanza.

James ameelezea changamoto mbalimbali anazokabiliana nazo kwenye soka la Tanzania ili kufikia malengo yake pengine hata pale alipofikia kaka yake.

“Namshukuru Mungu toka nilipotoka hadi nilipo sasa hivi, kuna mabadiliko makubwa ambayo nimeyaona hususan nilivyojengwa kiakili na kimwili, kumenibadilisha kwa namna moja ama nyingine kwa sababu ligi yetu ya Tanzania inachangamoto nyingi kama usipokuwa na utimamu wa mwili na akili huwezi kucheza.”

“Namshukuru mwalimu wangu (Etiene Ndayiragije) na uongozi wa Mbao kwa kukiona kipaji changu na kukibadilisha, waliamini kwamba James huyu waliyenaye kipindi fulani akiendelezwa na aka-focus atabadilika.”

“Kwa sasa kuna maendeleo mengi kwa sababu nilivyokuwa mwanzo ni tofauti na nilivyo sasa, napambana na najitoa ukizingatia kuna ndugu yangu (Simon Msuva) ambaye ameshatoka Tanzania na nilikuwa naona changamoto nyingi wakati anahaingaika na kupambana kabla ya mechi zake, vitu vyote hivyo nilivichukua kama changamoto kwangu na sehemu ya kujifunza.”

James ametaja baadhi ya vitu ambavyo anajifunza kutoka kwa kaka yake kuelekea kwenye mafanikio katika soka.

“Uvumilivu, alivumilia sana kwa sababu alikutana na mambo mengi kama matusi, fedheha  na maneno mengi lakini aliamua kuvumilia akimini hii ni safari ndefu na haiishii Tanzania na ipo siku atafika anapotaka na kweli amesogea, hivyo ni vitu ambavyo najifunza kutoka kwake.”

Unaambiwa kuwa James Msuva anapata changamoto kubwa kutokana na kaka yake kufanya vizuri nje ya mipaka ya Tanzania kwa sababu watu wengi wamekuwa wakiwalinganisha.

“Nina deni kubwa sana hasa kipindi ambacho anafanya vizuri kwa kufunga. Kwa kweli ananipa changamoto kubwa sana kwa sababu watanzania tunatabia ya kulinganisha mambo, kwa mfano mtu anaweza akahoji kwa nini mimi sifanyi mambo ambayo yanafanywa na Simon wakati huo anasahau ilimchukua miaka mingi hadi kufika hapo. Halafu mimi nina njia zangu siwezi jua nitafika vipi alipo yeye lakini naelewa kujituma na uvumilivu ndiyo kutanifikisha huko.”

James anaamini anaweza kufikia malengo yake ya kucheza nje ya nchi bila kupita kwenye vilabu vikubwa vya Tanzania endapo tu atafanya vizuri kwenye klabu anayoitumikia lakini ikitokea vilabu hivyo vikamuhitaji atakwenda kufanya kazi.

“Mpira ni malengo lakini pia kuna watu wanakuangalia zaidi ya wewe unavyojitazama, mimi natamani sana nicheze mpira nje ya hapa lakini kuna kitu kinaitwa changamoto, kakaangu kila siku ananisisitiza nitengeneze kwanza ndani licha ya mimi kutamani kucheza nje. Kwa hiyo naamini nikikomaa hapa nitafikia malengo, siwezi kusema natamani kucheza Simba, Yanga au Azam nipo tayari kucheza timu yoyote itakayovutiwa na mimi.”

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here