Home Kimataifa Tathmini kuelekea mchezo wa Chelsea na Barcelona

Tathmini kuelekea mchezo wa Chelsea na Barcelona

11095
0
SHARE

Na Haatim Abdul.

Bila ya kuangalia ubora wa timu zote mbili wala fomu walizonazo siku zote mechi ya Chelsea na Barcelona haijawahi kuwa rahisi na ndio maana tutegemee bonge moja la mechi hapo kesho.

Timu hizi zimekwisha kutana mara 15 tangu mwaka 1995. Kila mmoja ameshinda mara 5, kupoteza mara 5 na kutoka sare mara 5. Hio ikutoshe kuwa kila mmoja anapaswa kufanya kazi ya ziada ili kuweza kupata matokeo.

Chelsea wakiwa kama wenyeji ni wazi moja kati ya maeneo makubwa ambayo wanapaswa kuyadhibiti ni eneo la kiungo. Wanapaswa kuwadhibiti kabisa kina Sergio Busquets, Paulinho na kina Andres Iniesta na japo kwa mtazamo wangu mtu kama Bakayoko nisingependa kuona akianza kwani anaweza asilete ufanisi unaotakiwa kwenye hilo.

Lionel Messi bila shaka atakuwa ana hamu ya kuvunja mwiko wake wa kutofunga dhidi ya Chelsea na kikubwa ambacho Chelsea wanaweza kukifanya na ikawa sababu ya Messi kushindwa kumwona Thibaut Courtois ni kumkaba muargentina huyo kitimu na sio kumpa mtu mmoja jukumu la kufanya hivyo kwa maana ya Man to Man. Kwanini? Kikubwa ni kwamba Messi anaweza kumsababishia kadi kirahisi mchezaji na hii inaweza ikawa na madhara kwa upande wao. Cha kufanya ni kumwacha auchezee mpira ikisha Chelsea wacheze kitimu na kuziba nafasi na mianya yote.

Kwa upande wa Chelsea mchezaji tishio zaidi ni Eden Hazard na kama atacheza kama false 9 inaweza kuwa ni faida ya ziada kwa Chelsea. Kwanini? Hazard ana kasi jambo ambalo mabeki wa kati wote wawili Gerard Pique na Samuel Umtiti hawana na hii kasi yake inaweza kuwa ni faida kwa Chelsea hasa pale watakapokuwa wanashambulia kwa kushtukiza. Faida ya uwanja wa Nyumbani, Kukidhibiti kiungo, kumkaba Messi kitimu lakini pia hata kumchezesha Hazard kama namba 9 ya uongo kunaweza kuwapa nafasi kubwa Chelsea ya kuondoka na ushindi.

Nikija kwa Barcelona hakuna timu yenye fomu bora zaidi Ulaya msimu huu kushinda Barcelona na klabu hiyo imepoteza mchezo mmoja tu kwenye mashindano yote msimu huu na yenyewe ni dhidi ya Espanyol kwenye Catalan Derby kwenye mechi ya kwanza ya robo fainali ya kombe la mfalme.

Kama kuna silaha moja ya siri kwa Ernesto Valverde ni kiungo wa kibrazili Paulinho. Kwanini? Amekuwa akiipa Barcelona vitu viwili kwa wakati mmoja msimu huu akiwa kama kiungo. Ubora mkubwa kwenye eneo la kiungo lakini amekuwa akifunga magoli pia. Ni mtu ambae anapenda sana kuingia kwenye nafasi nyuma ya mabeki na kufunga.

Eneo hatari kwa upande wao ni eneo la ushambuliaji. Lionel Messi, Luis Suarez na Paulinho kwa pamoja wamefunga mabao 61 kwenye mashindano yote msimu huu. Ni wazi safu hiyo ya ushambuliaji inaweza kuiadhibu safu yoyote ya ulinzi hata hii ya Chelsea.

Barcelona hii ya sasa inaweza isiwe na ubora kama wa ile ya miaka takribani 6 nyuma lakini ni ukweli kwamba hii ya msimu huu iko kwenye wakati mzuri zaidi mpaka sasa.

Barcelona ya Ernesto Valverde inashambulia na kumiliki mpira lakini pia iko vizuri zaidi kiulinzi tofauti na ile ya Jose Enrique. Tofauti na tulivyozoea hata kuelekea kwenye mechi hii na Chelsea, Barcelona wanaweza kupata matokeo kokote msimu huu. Ni mechi itakayoamuliwa na ubora wa timu zote mbili na jinsi walimu watakavyochanga karata zao lakini pia uwezo binafsi wa mchezaji mmoja mmoja waliozoeleka kubadilisha matokeo na kuuamua michezo.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here