Home Kitaifa Mchezaji asiye zungumzwa, tuna-enjoy show zake za kibabe

Mchezaji asiye zungumzwa, tuna-enjoy show zake za kibabe

15061
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

  • “Jitumeni uwanjani kama Said Juma Makapu mfanikiwe.”

MIEZI 30 iliyopita wakati Said Juma Makapu aliposajiliwa na kocha Hans van der Pluijm na kuanza kuichezea Yanga msimu wa 2014/15, timu hiyo ilikuwa na viungo-walinzi kama Mnyarwanda, Mbuyu Twite na Salum Telela.

Alianza taratibu kuingia katika kikosi cha kwanza. Makapu hakuwa na uwezo mkubwa wa kupiga pasi kama Frank Domayo ambaye alikuwa ‘mhimili’ wa Yanga katikati ya uwanja lakini kiwango chake katika uzuiaji kilikuwa bora kila alipopewa nafasi.

Ni mchezaji hasa wa kiungo wa kati kwani hupendelea zaidi kucheza eneo hilo kwa muda mwingi akiwa uwanjani. Ukabaji wake wa nguvu, uwezo wa kupora mipira na kucheza faulo za ‘kitaalam’ ni kati ya mambo ambayo yananivutia sana kutoka kwa kiungo huyo mwenyeji wa Zanzibar.

Kwa aina ya mchezo wake-kupenda kubaki mbele ya walinzi wake kumekuwa kukiisaidia sana Yanga kila anapokuwepo uwanjani. Makapu hana mambo mengi, anapenda kupeleka mpira haraka kwa mchezaji aliye katika nafasi.

Ni ngumu sana kuona umuhimu wake uwanjani lakini pale anapofanyiwa mabadiliko mara nyingi pengo lake huonekana. Makapu ni namba sita wa kizamani ambaye anakaba zaidi kuliko kushambulia hili ni jambo ambalo linafanya wengi kutomuona sana uwanjani.

Anaibeba Yanga kwa sasa

Balaa la majeraha ambalo limekuwa likiiandama Yanga katika miezi ya karibuni limefanya mabingwa hao watetezi katika ligi kuu Bara kuhangaika msimu huu lakini katika michezo ya karibuni Makapu ameonyesha kuwa wachezaji wengine wanaweza kuendeleza ‘uhai’ wa timu wakati huu nyota kama Thabani Kamusoko akikosekana kwa miezi mitatu sasa.

Kocha msaidizi Shadrack Nsajigwa alipokaimu nafasi ya George Lwandamina katika michezo kadhaa wakati kocha huyo alipopatwa na matatizo ya kifamilia alianza kumchezesha Makapu kama mlinzi wa kati-wakati mwingine na nahodha Nadir Haroub ama, Vicent Andrew ama Kelvin Yondani na kijana huyo ameonekana kumudumu vizuri.

Utulivu wake wakati anapokaba na namna anavyoweza kuchukua mpira kutoka kwa mpinzani wake ni jambo ambalo limepelekea hadi kocha Mkuu, Lwandamina kumtumia Makapu katika eneo la ulinzi wa kati na hakika ni wakati wa kumpa sifa zake kijana huyu.

Amekuwa akijituma uwanjani na kuwahamasisha wenzake na kwa umri alionao bado ana mengi ya kufanya. Baada ya msimu wake wa kwanza kuwa mzuri, Makapu amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara na hata pale alipoonekana yuko fiti na kupewa nafasi alionyesha kukosa kujiamini.

Mchezo dhidi ya Azam FC alicheza vizuri sana-akiituliza timu hata wakati ilipokuwa ikishambuliwa. Ameendelea kuonyesha kiwango kizuri mechi hadi mechi na jambo hili halimuongezei thamani yeye tu bali limekuwa likiisaidia pia timu yake.

Kama wachezaji wengine wa Yanga watajituma kwa kiwango kama cha Makapu watafanya vizuri zaidi kama timu. Yupo katika mwenendo mzuri kiuchezaji, na atahitaji kuendelea kufanya vyema zaidi ili kuwa bora zaidi kwa mafanufaa ya timu yake. Wachezaji wengine nao waanze kujituma na kusahau matatizo ya nje ya uwanja ili kuinyanyua tena Yanga na kuirudisha katika ubora wake uliozoeleka.

Apewe mkataba mpya

Kuna baadhi ya wachezaji ambao mikataba yao ya kuichezea Yanga inakwenda kumalizika, Makapu ni miongoni mwao. Kusubiri hadi mwishoni mwa mkataba ndiyo asainiwe tena haifai. Yanga wanaweza kuanza kuwasaini tena wachezaji ambao kocha anaona wanamfaa kuendelea kuichezea Yanga msimu ujao ili kupunguza presha na mwanya wa klabu nyingine kumtwaa.

Makapu ni kijana bado na stahili yake ya uchezaji ni ‘taipu’ halisi ya Yanga.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here