Home Kitaifa Yanga nawakumbusha ‘kushindwa kujiandaa ni kujiandaa kushindwa’

Yanga nawakumbusha ‘kushindwa kujiandaa ni kujiandaa kushindwa’

8240
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

MABINGWA wa soka Tanzania bara, Yanga SC watashuka tena dimbani Jumatano hii kuwavaa Majimaji FC katika mchezo wa raundi ya 18 ligi kuu Tanzania Bara. Yanga wapo nyuma kwa alama saba dhidi ya vinara-mahasimu wao Simba SC ambao watakuwa ugenini kucheza na Mwadui FC siku ya Alhamisi.

Ushindi ‘kiduchu’ katika mchezo wa raundi ya awali dhidi ya St. Louis Club kutoka Shelisheli katika ligi ya mabingwa Afrika haukuonekana kufurahiwa sana na wapenzi wa timu hiyo. Yanga walicheza kwa kiwango cha chini kwa mara nyingine huku baadhi ya wachezaji wakionekana kukosa morali.

Wanachopaswa kufanya

Kushindwa kufunga walau magoli mawili dhidi ya St. Lousi katika uwanja wa nyumbani upande wangu sitazami kama ni tatizo kwani katika misimu ya karibuni ya Caf mabingwa hao mara 27 wa kihistoria nchini wamekuwa na tabia ya kupata matokeo bora zaidi katika viwanja vya ugenini.

Msimu wa 2016 waliitoa APR ya Rwanda katika mchezo wa raundi ya kwanza baada ya kuifunga timu hiyo 1-0 ugenini. Matokeo ya nyumbani yalikuwa 1-1. Msimu uliopita pia tulishuhudia Yanga ikianza na ushindi wa 1-0 nyumbani dhidi ya wawakilishi kutoka Visiwa vya Comoro, Ngaya Club lakini waliweza kuichapa timu hiyo mabao 5-1 kwao na kusonga mbele, hivyo kwa aina ya timu ambayo wanacheza nayo sitazamii kuona wawakilishi wetu hao wanaondolewa katika michuano.

Yanga wapo katika michuano yote wanayopaswa kucheza msimu huu, wapo katika mbio za kutetea ubingwa wao wa ligi kuu, wapo 16 bora ya michuano ya FA Cup, pia wapo katika michuano ya Caf Champions league na kama watavuka raundi hii ya awali itamaanisha kuwa wataendelea kuwepo katika michuano ya Caf hadi mwezi wa nne kwa maana hata kama watatolewa katika raundi ya kwanza katika ligi ya mabingwa wataangukia katika michuano ya kombe la Shirikisho.

Wakati katika ligi ya mabingwa Afrika kukiwa na michezo miwili ya mtoano-nyumbani na ugenini, na ikiwa mshindi atashindwa kupatikana katika muda wa dakika 180 timu huingia katika upigaji wa mikwaju ya penati tano-tano na mshindi husonga mbele, katika FA Cup ni tofauti kidogo kwani timu hazipati nafasi ya kujiuliza baada ya dakika 90 za kwanza kumalizika.

Inapotokea kufungana kwa matokeo sheria ya mikwaju ya penati hutumika kusaka mshindi. Sidhani kama Yanga wamekuwa na maandilizi mazuri katika michezo ya mtoano. Katika michezo miwili ya FA walipata nafasi ya kucheza na timu za daraja la pili (Reha FC na Ihefu FC) sasa wanaenda kucheza na Majimaji FC katika mchezo ujao wa raundi ya 16 bora.

Dhidi ya Reha walifunga magoli mawili ndani ya dakika kumi za mwisho na kusonga mbele, walisubiri hadi dakika ya mwisho kabisa ya mchezo kusawazisha kwa kiki ya penati vs Ihefu jambo ambalo liliwapa nafasi ya kufika hatua ya kupigiana penati tano-tano.

Katika mikwaju hiyo Yanga ilipoteza penati ya tano ambayo Obrey Chirwa alikosa. Kama si ukosefu wa kujiamini Ihefu wangefuzu, lakini kipa Youthe Rostand aliweza kuzuia mikwaju mitatu na kuibeba timu yake hadi raundi ya 16.

Tangu kuanza kwa msimu huu Yanga imepoteza michezo miwili kwa njia ya penanati. Walipoteza mbele ya mahasimu wao Simba katika Ngao ya Jamii, pia walianguka vs URA ya Uganda katika nusu fainali ya michuano ya Mapinduzi.

Chirwa kwa upande wake ndiye mchezaji aliyepoteza mikwaju mingi ya penati kwa timu yake hadi sasa huku mara tatu akikosa ndani ya mwaka huu. Kwanini, kwa miaka mitatu sasa Yanga imekuwa ‘nyanya’ katika mikwaju ya penati? Chini ya Hans walipoteza mara kadhaa na sasa tayari naona wamejenga ‘tabia yao’ ya kutojiamini’ inapofika muda wa mikwaju ya penati.

Kitu kinachoshangaza zaidi si Chirwa tu anayekosa penati mara kwa mara, bali tatizo hilo lipo karibia kwa timu nzima jambo ambalo linaonyesha dhahiri kuwa timu hiyo haifanyii mazoezi ya kutosha eneo hilo. Kwa timu inayocheza michuano miwili ya mtoano ni makosa makubwa kutofanya mazoezi ya upigaji wa mikwaju ya penati na Yanga hawawezi kukwepa ukweli huu.

Hawajachelewa, wana wiki mbili za kujiandaa dhidi ya mchezo wa marejeano vs St. Louis pia wana wiki tatu za kujiandaa na mchezo wa FA dhidi ya Majimaji FC hivyo wanaweza kufanya mazoezi ili kujiimarisha zaidi kwa maana katika michezo hii ya mtoano ni rahisi game kufika katika hatua ya penati.

Yanga kama timu wameonekana kupoteza kujiamini kila inapofika wakati wa mikwaju ya penati na kama timu nyingine zingekuwa zinahimili mchezo wa kawaida dhidi yao na kulazimisha sare ndani ya dakika za kawaida za mchezo ni rahisi kwao kusonga mbele kama watatulia katika mikwaju ya penati.

Ili kurejesha kujiamini kwao katika upigaji wa mikwaju ya penati ni lazima wakubali kufanya sana mazoezi na kitendo cha kushindwa kufanya hivyo kitawaondoa katika michuano siku za mbeleni hata mbele ya wapinzani dhaifu.

Wanaweza kuiondoa St. Louis kwa vile timu hiyo ya Shelisheli imeonekana hainawezi kufunga na Yanga wanaongoza tayari lakini dhidi ya Majimaji tena katika uwanja wa Majimaji, Songea mahala ambako wameshinda mara moja tu katika kipindi cha miaka ya karibuni hii inaweza kuwa tofauti.

Majimaji wanaweza kuzuia Yanga wasifunge, pia wamekuwa na tabia ya kufunga goli/magoli vs Yanga jambo ambalo linaweza kuwa tatizo kwa mabingwa hao wa Bara. Nahodha wa zamani wa Jamhuri ya Ireland na Manchester United, Roy Keane ana msemo wake fulani ‘kushindwa kujiandaa, ni kujiandaa kufungwa’ hivyo Yanga wafanyie kazi kwa kiwango kikubwa upigaji wao wa mikwaju ya penati, ili kujiandaa na changamoto hiyo itakapowafika kwani wapo katika michuano ambayo inawalazimu kuwa tayari na bora katika upigaji wa mikwaju ya penati.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here