Home Kitaifa Ubora pekee ndiyo unapaswa kuongezwa, si kuwakataza mashabiki Simba kuwazomea Yanga

Ubora pekee ndiyo unapaswa kuongezwa, si kuwakataza mashabiki Simba kuwazomea Yanga

7461
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

KUELEKEA ufunguzi wa michuano ya Caf upande wa vilabu wikendi hii wawakilishi wa Tanzania Bara, timu za Yanga na Simba zote zitaanzia nyumbani michezo yao ya raundi ya kwanza. Yanga ambao watacheza michuano ya mabingwa Afrika kwa msimu wa tatu mfululizo na wanne ndani ya miaka mitano wataikaribisha St. Louis Suns kutoka visiwa vya Shelisheli.

Wana fainali wa Caf Confederation Cup 1993, Simba SC wao watakuwa wakicheza mchezo wao wa kwanza wa Caf baada ya kusubiri kwa miaka mitano. Simba itakutana Gendarmerie Nationale kutoka Djibouti. Licha ya kwamba mpira ‘una-dunda’ ila sitaraji hata kidogo kuona timu yoyote ya Bara ikiondolewa katika raundi hii ya awali kutokana na kukutana na timu zinazotoka katika nchi za mwisho mwisho kabisa katika viwango vya soka Afrika na duniani kiujumla.

Jambo muhimu la kukumbukwa

Nitakuwa narudia kile ambacho nimepata kukiandika takribani miaka sita iliyopita-timu zetu zinapaswa kukumbuka umuhimu wa michuano ya Caf kwa maendeleo ya soka la Tanzania. Tanzania bara imekuwa ikitoa wawakilishi wawili tu katika michuano ya Caf kwa miaka 15 mfululizo tangu Shirikisho hilo la soka Afrika lilipoamua kuvunja michuano ya Kombe la Washindi Afrika mwaka 2003 na kuyaunganisha na iliyokuwa michuano ya Kombe la Caf.

Miaka ya nyuma kabla ya CAf kuanza kuboresha michuano yake , ligi ya mabingwa ilikuwa ikijitegemea, kombe la Caf vilevile lilikuwa likijitegemea sawa na lile la washindi. Hii ilifanya kila nchi barani Afrika kutoa wawakilishi watatu katika michuano hiyo-bingwa wa nchi alikuwa akipata nafasi ya moja kwa moja kucheza klabu bingwa, mshindi wa pili alikuwa akienda kucheza michuano ya Caf huku nafasi ya muwakilishi wa kombe la washindi kwa hapa nchini ilikuwa ikichukuliwa na ama bingwa wa FA au timu ya tatu itakayomaliza katika ligi kuu.

Kwa zaidi ya ‘muongo’ mmoja sasa tangu Caf ilipoboresha michuano yake kuna nchi 12 ambazo zimekuwa zikitoa wawakilishi wawiliwawili katika michuano ya vilabu barani humu-timu mbili zimekuwa zikipata nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa na nyingine mbili zimekuwa zikipata nafasi ya kucheza Confederation Cup. Kwa ukanda wa Cecafa ni Sudan tu ambao wamekuwa wakipeleka wawakilishi wawiliwali katika kila michuano ya Caf.

Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Djibout, Somalia, Sudan Kusini, Eritrea, Zanzibar na Tanzania bara zote zimekuwa zikipeleka timu mbili tu kiujumla katika michuano yote ya vilabu inayoandaliwa na Caf. Ni tofauti na wenzetu wa Kusini kama Angola, Afrika Kusini, Zimbabwe, na Zambia ambao wao wamekuwa wakipata nafasi mbilimbili katika kila michuano.

Sidhani kama ubora wa timu zao za Taifa ndiyo sababu ya wao kupata nafasi zaidi katika michuano ya vilabu bali naamini ni kutokana na namna klabu zao zinavyojitahidi kupambana na kutoa ushindani katika michuano hiyo. Wala hawapendelewi na wala nafasi hizo wanazopewa hazitokani na maendeleo ya ligi zao bali ni kutokana na klabu zao kucheza kwa kiwango kizuri katika michuano husika mwaka hadi mwaka.

Mara ya mwisho kwa timu kutoka Zambia, Zimbabwe ama Angola kutwaa ubingwa wa Caf ni lini? Sasa mbona wamekuwa na nafasi nyingi zaidi yetu? Haya ndiyo maswali muhimu tunayopaswa kuyatafutia majibu yake na si kukumbushana kuhusu namna ya kushangilia ama kuzomeana sisi kwa sisi wakati klabu zetu zinapokuwa zikicheza na timu kutoka ng’ambo.

Leo hii ni ‘aibu’ kuona klabu iliyoanzishwa miaka 80 iliyopita ikiitisha mkutano na wana habari na ikisema hadharani ‘hatupaswi kuzomeana!’ hii inamaana kutafuta majibu ya kwanini wamekuwa wakiondolewa mapema katika michuano ya kimataifa huku mafanikio yao pekee yakiwa ni kufika hatua ya makundi ya Champions league mwaka 2003.

Simba kwanini ilifungwa 0-1 nyumbani, 4-0 ugenini na Recreativo de Libolo mara ya mwisho walipocheza michuano ya Caf mwaka 2013? Hapa ndipo kwa kuanzia na si kulazimisha watu wazomee au kushangilia kitu wasichokuwa tayari kukishabikia au kukizomea. Huu ni wakati ambao vilabu vyetu vyenyewe vinapaswa kuongeza ubora wao katika michuano ya Caf na kitendo cha wao kufanya vizuri kwa misimu mitano mfululizo kunaweza kuwafumbua macho Caf hivyo wakatutazama na kutuongezea timu.

Miaka sita iliyopita nilisema nafasi mbili tu kwenda Caf hazitoshi kwa klabu za Tanzania lakini nyongeza hiyo haiwezi kupatikana ikiwa kila msimu klabu zetu zinaondolewa mwanzoni tu mwa michuano. Hili si la mshabiki, ni jukumu la klabu, wachezaji na benchi la ufundi ni wao wanapaswa kupandisha viwango vyao katika michuano ya Caf na kufanya mambo kwa umakini mkubwa.

Kama Simba na Yanga zitafika walau hatua ya makundi msimu huu, na kwa misdimu mitatu hadi mitano ijayo ikawa hivyo kwa wawakilishi wengine itakuwa ni rahisi sana kwetu kupewa nyongeza ya timu jambo ambalo ni muhimu sana kwa maendeleo ya mpira wetu hivi sasa.

Timu 20 kuwania nafasi moja tu ya kuwakilisha nchi katika ligi ya mabingwa ni jambo baya kwa maendeleo ya soka ila kama kutakuwa na nafasi tatu za uwakilishi kutoka katika ligi yetu itasaidia kwa kiasi kikubwa mno kuongeza ubora katika VPL. Sudan, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Nigeria, Cameroon, Senegal, Libya, Ghana, Misri, Morocco, Tunisia, Algeria wala hawabebwi na ubora wa ligi zao bali ni namna wanavyocheza kwa kiwango cha juu katika michuano ya Caf.

Ukitazama katika nchi 12 ambazo zimepewa upendeleo wa kutoa jumla ya wawakilishi wanne katika michuano ya Caf utagundua kuwa katika ligi zao mabingwa ni walewale tu kila msimu kama ilivyo hapa kwetu. Hii inamaanisha kuwa ushindani wao uko vilevile katika ligi zao lakini inapofika wakati wa michuano ya Caf hupandisha viwango vyao mara mia zaidi na hii ndiyo huleta tofauti.

Tutazame sababu hizi na kuzifanyia kazi kwa maana mashabiki siku zote watashangilia wanavyovipenda na watazomea pale wasipopapenda hivyo huu si wakati wa kuombana msaada wa ushangiliaji bali ni wakati wa kila mmoja katika klabu zetu wawakilishi kuongeza umakini, kujituma ili kupata ubora katika michuano ya Caf.

Nadhani sisi tumekuwa makini zaidi katika michuano ya ndani kuliko ile ya kimataifa ndiyo maana wachezaji wetu hawajitumi ipasavyo katika michuano ya Caf. Naamini kama tukipandisha kiwango chetu katika kila idara wakati wa michuano ya Caf tutapiga hatua haraka lakini kwa namna inavyoonekana bado hatujajiandaa vya kutosha ndio maana klabu inaitisha mkutano na wana habari na kuomba mashabiki wao wasizomee timu pinzani yao.

Mara zote ‘shabiki’ ni mtu anayependa kupita kiasi na kinyume chake pale anapochukia ni ‘mtu anayechukia kupita kiasi’ mtu wa Yanga kamwe hawezi kuishangilia Simba ila anaweza kuwapongeza wanapofanya vizuri, hivyo tufanyie kazi sababu za msingi zinazotuangusha kila mara na kupandisha kiwango chetu kuanzia kiuchezaji, kimaandalizi kuelekea michuano ya Caf wikendi hii.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here