Home Kitaifa Tshabalala anataka nafasi Simba

Tshabalala anataka nafasi Simba

9713
0
SHARE

Mchezaji bora wa ligi kuu Tanzania bara msimu uliopita (2016/17) Mohamed Hussein Zimbwe Jr kwa sasa hachezi mara kwa mara kwenye kikosi cha simba, maswali mengi yameanza kuibuka kuhusu nafasi yake kwenye kikosi cha wanamsimbazi kutokana na uwezo unaooneshwa na asante kwasi anayefanya vizuri kwenye eneo la kushoto.

Kumbukumbu zinaonesha kwamba, Zimbwe Jr alicheza mechi zote za msimu uliopita kwa dakika zote 90 na kumfanya kucheza dakika zote 2,790 za mechi 30 za ligi. Kutokana na kutoonekana uwanjani mchezaji huyo kijana amesema endapo atapata nafasi ataonesha uwezo wake.

“Mpaka sasa kuna mengi yanaendelea lakini nafikiri kikubwa ni nafasi, mwalimu ndiyo mtu wa mwisho sasa hivi tuna timu pana kwa hiyo kila anayepata nafasi anafanya vizuri na timu inapata matokeo hata mimi nikipata nafasi nitafanya vizuri ili timu ipate matokeo, hilo ndiyo jambo la muhimu.”

Kama unakumbuka, Zimbwe Jr alipata majeraha kwenye mchezo wa fainali ya kombe la shirikisho Tanzania bara (Azam Sports Federation Cup) Mei 27, 2017 ambapo alishindwa kuendelea na mchezo. Kutokana na majeraha hayo amekiri kwamba mchezaji anahitaji muda kurejea katika ubora wake.

“Mchezaji ukitoka kwenye majeraha inakuwa vigumu kurudi kwa haraka, unakuwa unarejea taratibu nashukuru kwa sasa nipo vizuri kinachotakiwa ni nafasi, endapo nikipata nafasi kuna kitu nitaonesha.”

Simba itarejea kwenye mashindano ya kimataifa jumapili hii ya Februari 11, 2018 kupitia mashindano hayo Zimbwe Jr anaamini ni fursa ya kujitangaza kwa wachezaji wenye malengo ya kucheza nje ya nchi.

“Kuna faida nyingi za kushiriki mashindano ya kimataifa, ukitaka kujitangaza vizuri ni lazima ukutane na watu tofauri, naamini kupitia mechi hizi za kimataifa tutakuna na mawakala wa wachezaji.”

“Ninachoamini unapokwenda kucheza nje ya nchi mawakala wanakufuatilia na unaporudi wanafuatilia pia ili kuangalia muendelezo wa mchezaji kwa hiyo kwa sisi vijana ambao bado tuna muda mrefu wa kucheza na tuna malengo ya kucheza nje ya nchi nafikiri hii ni fursa nzuri kwetu.”

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here