Home Kitaifa Asante Kwasi ‘anapomtupa’ Zimbwe Jr katika ‘maji marefu’

Asante Kwasi ‘anapomtupa’ Zimbwe Jr katika ‘maji marefu’

13254
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

MCHEZO wake wa kwanza tu katika ligi akiichezea Simba alifunga bao. Na kuanzia hapo amekuwa tishio si tu kwa wachezaji wa timu pinzani bali hadi kwa mchezaji bora zaidi wa klabu yake msimu uliopita, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr.’

Namzungumzia mlinzi ‘kiraka’ raia wa Ghana, Asante Kwasi ambaye alifunga goli la pili la Simba katika ushindi ‘usiotarajiwa’ 4-0 vs Singida United mwezi uliopita. Kwasi alifunga goli hilo baada ya kuvunja mtego wa kuotea uliowekwa na walinzi wa Singida United na kuwahi pasi ndefu ya mbali iliyopenyezwa na kiungo Said Ndemla.

Ni beki ‘haswa’

Kutokana na mfumo wa kiuchezaji wa Simba-kukaa sana na mpira nakuanzisha mashambulizi kutokea nyuma kwenda mbele, Kwasi ameweza kuingia rahisi katika mchezo wa timu hiyo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira, kukaba, kuanzisha mashambulizi  na kushambulia kwa mipira yake mirefu inayofika kwa walengwa.

Kusema kweli, licha ya kwamba tangu kuanza kwa msimu huu, Erasto Nyoni ameonekana bora katika beki za pembeni lakini katika michezo minne iliyopita ambayo Simba imecheza ikiwa na Kwasi katika upande wa kushoto mlinzi huyo ameongeza kitu.

Licha ya kuwa ni ‘chachu’ kwa mashambulizi ya Simba akitokea upande wa kushoto, uwezo wake wa kucheza katika nafasi na kuziba mianya ya kupitishwa mpira katika ‘njia’ kwa wachezaji wa timu pinzani kunanikumbusha baadhi ya walinzi bora zaidi wa kushoto waliopata kutokea katika timu hiyo katika miaka ya karne mpya.

Kwasi anapora vizuri mpira ikitokea hivyo ila kutokana na mwili wake wa kawaida yeye amekuwa akitegemea zaidi kuziba njia za wapinzani. Ni mbabe katika kukaba na uwezo wake wa kucheza nafasi zote za beki ya kati kumemfanya kuwakumbusha mara kwa mara walinzi wenzake jambo ambalo limekuwa likiongeza umakini katika timu yao.

Kama mshambuliaji

Baada ya michezo yake minne ya VPL akiwa Simba huku akiwa tayari amefunga goli moja na kutengeneza mawili likiwemo lile alilofunga Emmanuel Okwi vs Azam FC siku ya Jumatano hii, bila shaka Mghana huyu anaacha maswali kuhusu hatma ya Zimbwe Jr ambaye amecheza michezo miwili tu kati ya 17 ambayo timu yake imecheza msimu huu.

Zimbwe anapaswa kujituma zaidi katika viwanja vya mazoezi ili kurejesha nafasi ambayo aliiopoteza hata kabla ya ujio wa Kwasi. Alikuwa ‘nguzo’ ya Simba katika beki ya kushoto wakati timu hiyo iliposhinda Taji la FA msimu uliopita huku yeye akitwaa tuzo ya mchezaj bora wa klabu na ligi kuu.

Majeraha ambayo aliyapata kwenye mchezo wa fainali ya FA msimu uliopita yamechangia kumrudisha nyuma nahodha huyo msaidizi wa Simba na ujio wa Kwasi ni ishara nyingine mbaya kwake kama hatakaza ‘buti’ lake na kupigania nafasi.

Kwasi anajituma jambo ambalo lipo pia kwa Zimbwe Jr, ila yeye amekuwa akiangushwa na uwezo wake uleule wa kila siku huku akicheza nafasi moja tu kwa usahihi. Zimbwe Jr alitengeneza magoli mengi ya Simba msimu uliopita lakini stahili yake ya kushambulia bila kuzingatia nafasi yake ya ulinzi inaweza kuendelea kumuangusha kama hatabadilika.

Kwasi tangu yupo Mbao FC msimu uliopita na baadae Lipuli ameonekana kuwa kikwazo kwa washambuliaji wa timu pinzani lakini pia amekuwa na faida ya kufunga magoli kwa timu yake kutokana na uwezo wake wa kufuatilia mashambulizi yanayotokea nyuma na kuhakikisha anafika katika eneo ambalo anadhani mpira wa mwisho utafika.

Hii inatokana si tu tamaa ya mchezaji husika katika kushambulia bali uwezo pia wa kuusoma mchezo na kufanya maamuzi sahihi katika wakati sahihi. Kushambulia kwake hakumuondolei sifa yake uwanjani mchezaji wa nafasi ya ulinzi na hii inatokana na umakini ambao amekuwa nao anapokuwa ndani ya nusu uwanja ya eneo la timu yake.

Zimbwe Jr amtazame Kwasi

Zimbwe Jr ni kati ya wachezaji ambao wanapaswa kuongeza umakini kwa kiasi kikubwa hasa katika uzuiaji na upigaji wake pasi ili kumuondoa Kwasi katika nafasi ya beki wa kushoto.

Kuendelea kumuona mchezaji bora wa klabu na VPL msimu uliopita akishika shavu lake katika benchi ni jambo lisilopendeza lakini katika mchezo wa soka ni rahisi kupanda kuliko kubaki katika kilele na Zimbwe Jr asipostuka mapema anaweza kufuata nyayo za wachezaji bora wa msimu ambao ‘walipotea’ mara tu baada ya kushinda tuzo hiyo. Kwa sasa lazima tukubali ukweli kuwa Kwasi amemuweka katika ‘maji marefu mno’ Zimbwe Jr ni wakati wake wa kujiokoa sasa.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here