Home Kitaifa Jicho La 3: Simba SC vs Azam FC ni ‘pacha’

Jicho La 3: Simba SC vs Azam FC ni ‘pacha’

10676
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

WAKATI mwingine kwenye mchezo wa soka ni rahisi mno kuongea kuliko kutenda, ndiyo maana licha ya kucheza michezo 16 pasipo kupoteza-wakiwa pointi nne nyuma ya mabingwa watetezi, Simba bado wana safari ndefu kabla ya kurudisha ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara Bara waliotwaa kwa mara ya mwisho msimu wa 2011/12.

Kushinda 4-0 dhidi ya wapinzani imara-Singida United huku wakicheza vizuri kumewafanya mashabiki wa mabingwa hao mara 16 wa kihistoria kuamini kuwa ‘huu ni msimu wao.’ Simba wameshinda dhidi ya Mbeya City FC, Tanzania Prisons-Mbeya, Kagera Sugar FC-Bukoba mahala ambako katika misimu ya karibuni wamekuwa wakiangusha pointi.

Inawezekana wapo katika ‘umbo’ la kuwafunga wapinzani wao wowote, lakini michezo dhidi ya Azam FC, Mtibwa Sugar FC, Yanga SC katika raundi ya kwanza ilionyesha kitu kingine tofauti kuwa msimu huu kuna timu walau tano zenye uwezo wa kucheza vizuri dhidi ya timu kubwa-Lipuli FC ni timu ya nne kupata sare vs Simba katika jiji la Dar na sare ya 2-2 dhidi ya Mbao FC pale Kirumba Stadium inaonyesha ni kiasi gani pia michezo ya ugenini inavyoweza kuwa migumu msimu huu.

Simba vs Azam FC

Kuelekea mchezo huu wa Jumatano hii, Simba wapo mbele ya Azam FC kwa alama tano, huku wakiongoza ligi kwa tofauti ya pointi nne dhidi ya mabingwa watetezi Yanga. Azam FC bado inaonekana ‘kusuasua’ lakini hadi kufikia raundi ya 16 wamekuwa katika mwendo ambao unawafanya kuendelea kushindania taji. Simba wanafahamu fika kitendo cha kuifunga Azam FC itawafanya kuwa mbele ya mabingwa hao wa 2013/14 kwa alama nane na watarudisha gepu la pointi kutoka nne hadi saba dhidi ya Yanga.

Hii ni sababu mojawapo ambayo itawasukuma sana kusaka matokeo. Wameshindwa kuifunga Azam FC katika michezo minne mfululizo waliyokutana katika michuano tofauti. Azam FC iliifunga Simba 1-0 katika fainali ya Mapinduzi Cup 2017, wakaishinda tena 1-0 siku chache baadae katika mchezo wa mzunguko wa pili wa ligi kuu, wakalazimishwa suluhu-tasa katika uwanja wa Azam Complex katika mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu huu, wakaichapa tena Simba 1-0 katika mchezo wa hatua ya makundi katika Mapinduzi Cup mwezi uliopita.

Azam FC bado hawajaonyesha kiwango kizuri wakicheza ugenini msimu huu. Katika michezo minne ya karibuni wamefanikiwa kushinda miwili (vs Tanzania Prisons-0-2 ugenini) na Ndanda FC (3-1 nyumbani) wamepoteza mchezo mmoja ( vs Yanga 1-2-nyumbani) na wametoa sare mchezo mmoja (dhidi ya Majimaji 1-1-ugenini) Kufunga magoli saba katika michezo minne iliyopita ni dalili njema kwa kocha Mromania Aristica lakini baada ya kuonekana wana zuia vizuri mwanzoni mwa msimu sasa wameonekana kushuka kwa kiwango chao katika ulinzi ndiyo maana wameruhusu magoli manne katika michezo minne iliyopita.

Nahodha, Himid Mao-katika fullback ya kulia, Mzimbabwe Bruce Kangwa katika fullback ya kushoto, Yakub Mohamed na Aggrey Morris katika beki ya kati wanaweza kutazama namna ya kurekebisha makosa yao ili kuendeleza rekodi yao ya kutoruhusu goli vs Simba. Azam haijaruhusu goli lolote katika michezo minne iliyopita waliyokutana na Simba na uwezo wao huo wa kujilinda umekuwa ukiwapa matokeo.

Simba imefunga magoli 38 katika michezo 16 iliyopita, washambuliaji wake watatu-Emmanuel Okwi (amefunga magoli 12), nahodha John Bocco (amefunga magoli tisa) na Shiza Kichuya (mwenye magoli sita) wamekuwa tishio msimu huu na watu ambao wamekuwa wakiwapa matumaini makubwa mashabiki wa timu hiyo hadi sasa. Walinzi wa Azam FC waliweza kumzima Bocco-mfungaji bora wa muda wote wa Azam FC wakati walipokutana naye katika mchezo wa mzunguko wa kwanza lakini Bocco wanayekwenda kukutana naye Jumatano hii ni tofauti kabisa na yule wa mwezi Septemba.

Bocco alifunga goli la juhudi binafsi na kuipa ushindi wa 1-0 Simba dhidi ya Prisons, akafunga magoli yote mawili vs Ndanda FC katika uwanja wa Nangwanda, hakufunga vs Singida tu katika michezo iliyopita ya Simba kwani alifunga moja ya magoli mawili vs Kagera Sugar, pia ametoka kufunga magoli mawili wikendi iliyopita katika ushindi wa 4-0 vs Majimaji FC.

Ni kwa namna gani

Azam FC wanaweza kumzima mchezaji huyo anayejituma zaidi hivi sasa pale Simba hilo ni jambo litakalotegemea uwezo wa timu nzima huku stahili yao ya kucheza soka la uvumilivu nikitaraji kuona ikiendelea kuwabeba. Simba licha ya ubora wao katika ufungaji-kiasi si wavumilivu hasa pale mechi inapokuwa ngumu upande wao.

Azam FC wamekuwa wakianza mchezo vs Simba kwa kasi na wamekuwa na bahati ya kufunga goli la uongozi mapema na baada ya hapo wachezaji wote wanacheza kwa uvumilivu kuhakikisha wanalinda goli hilo hadi mwisho. Okwi akikimbia upande wa kushoto atakutana na Mzimbabwe, Kangwa, Kichuya atakutana na Himid hii inaleta picha kuwa Simba watapa wakati mgumu kama watategemea zaidi mbio na maarifa ya Okwi na Kichuya kwa maana wanakutana na walinzi wenye stamina na wanaozuia kwa nguvu, akili.

Kukosekana kwa Mghana James Kotei upande wangu naona kutaleta mapungufu katika ubora wa Jonas Mkude. Kotei ni mchezaji muhamasishaji na kama angeungana na Mkude na Said Ndemla Simba wangekuwa na nafasi kubwa ya kutawala mchezo na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga wakitokea kati mwa uwanja. Bado sijaweka imani ya moja kwa moja katika uwezo wa upigaji pasi wa Mkude namna anavyojituma uwanjani.

Hii ni mechi ambayo Azam inaweza kutawala kati mwa uwanja kama kiwango cha Mkude kitakuwa chini katika upigaji wa pasi. Yahya Zayd, Frank Domayo, Salum ni baadhi ya wachezaji ambao wako ‘sharp’ kuiwahi mipira inayopotezwa hovyo na wapinzani kati mwa uwanja na kupiga hara pasi za mbele.

Simba hawana tatizo katika ulinzi, na Azam FC ni kati ya timu ‘butu’ kiufungaji hivyo inaweza kuwa mechi itakayosimamisha shilingi na kama ukiniambia-nibet, matokeo ningechagua 0-0 au 0-1 kama Simba watafanya makosa walau mawili katika eneo lao la ulinzi.

Kurejea kwa Shomari Kapombe na kiwango cha Asante Kwassi kumefanya Simba kuwa na balansi nzuri katika mashambulizi na uzuiaji. Walinzi hao wa pembeni wameonyesha kuichezesha vizuri timu tangu Kapombe alipoingia uwanjani akitokea benchi na kuichezea Simba mchezo wake wa kwanza dhidi ya Kagera.

Uimara pia wa Azam katika sehemu za pembeni unataraji kuupendezesha mchezo huu ambao hakuna anayetaka kupoteza. Shaban Idd ni kijana anayeweza kutumia vizuri nafasi ndogo inayopatikana hivyo Erasto Nyoni na Yusupf Mlipili/Juuko Murshid wanapaswa kuwa makini na kijana huyo kwani ana shabaha na uwezo wake wa kumfahamu Aishi Manula unaweza kumpa tamaa ya kujaribu mahesabu yake kila atakapopata upenyo. Kasi yake akicheza na Zayd inawweza isionekane tatizo kubwa kwa Simba lakini hawa ni vijana wawili wakuchungwa sana na wanaweza kuisimamisha Simba.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here