Home Kitaifa Tumeziona timu zilizopanda VPL msimu ujao, bingwa nani? Hii ndiyo njia mbadala

Tumeziona timu zilizopanda VPL msimu ujao, bingwa nani? Hii ndiyo njia mbadala

6236
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

TIMU Sita ambazo zimefanikiwa kupanda ligi kuu Tanzania Bara msimu ujao kutoka ligi daraja la kwanza tayari zimefahamika baada ya kukamilika kwa michezo ya Kundi A Jumatatu hii. JKT Tanzania, African Lyon, na Coastal Union zimerejea tena ligi ya juu, Biashara United, Alliance Schools Academy na KMC zikipanda kwa mara ya kwanza.

Kupanda kwa timu hizi ni mafanikio makubwa kwao, lakini kwa hakika ligi hiyo imekuwa ikiendeshwa vibaya mno, huku TFF na wasimamizi Bodi ya ligi wakishindwa kufanya jitihada za kuiboresha. Ukiachana na malalamiko mengi kuhusu waamuzi na uchezeshaji wao uliodaiwa kuzipendelea zaidi timu za nyumbani-sijui ni zipi kwa maana kila timu ilikuwa ikilalamika inapocheza ugenini-TFF imeshindwa kutatua tatizo hilo.

Sawa, timu hizo zimepanda lakini nani bingwa wa ligi hiyo? Ni aibu kwa ligi kubwa nchini kama hiyo kukosa bingwa wakati hata ligi za mitaani huwa zinatoa mshindi wa jumla katika michuano husika. Kushindwa kupatikana kwa bingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa pili mfululizo ni ‘udhaifu’ ambao unapaswa kutatuliwa haraka na pia bingwa wa FDL hapaswi kupatikana kwa namna ambayo alipatikana bingwa wa mwisho-Mwadui FC msimu wa 2014/15.

Njia mbadala

Nimekuwa nikifuatilia ligi mbalimbali za barani Ulaya-zile za juu na za chini pia na huko nimekuwa nikivutiwa na namna vyama/mashirikisho ya soka ya maeneo husika yanavyopambana kila uchao kuhakikisha ligi zao zinachezwa kwa ushindani. Ushindani ndiyo msingi wa kutengeneza ubora katika mashindano husika na katika hili kuna mambo mengi ambayo yanapaswa kutazamwa. Mfano, kwa takwimu zilizotoka mwezi uliopita, ligi daraja la kwanza England-Championship imekuwa minongoni mwa ligi tatu bora zinazotazamwa zaidi duniani. Inafuatiliwa zaidi ya La Liga-ligi ambayo imekuwa ikiwatoa washindi wa mataji ya Ulaya mwaka hadi mwaka katika misimu ya karibuni.

Championship iko juu ya La Liga ligi ambayo imetoa washindi wa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia mara 16 katika karne hii. Ushindani uliopo katika ligi hiyo unavutia sana. Kwanza kuna timu 24-baada ya kila timu kucheza michezo 46-mbili za juu zinapanda ligi kuu moja kwa moja huku kiongozi wa ligi akitwaa ubingwa. Kuanzia timu iliyomaliza nafasi ya tatu hadi ile ya sita zitacheza michezo ya ‘play off-nusu fainali’ nyumbani na ugenini, washindi wanakutana fainali na mshindi anapanda daraja kukamilisha timu ya tatu baada ya zile mbili za mwanzo.

Ili kuongeza ushindani hadi mwishoni mwa msimu-kuanzia nafasi za juu hadi chini ya msimamo-timu ya mwisho katika zile tatu zinazopaswa kushuka daraja la pili haitashuka moja kwa moja bali itacheza na mshindi wa play off kutoka ligi daraja la pili na anayeshinda anapanda.

Kama ile iliyopo Championship itashinda ‘play off’ dhidi ya timu ya tatu iliyotakiwa kupanda daraja la kwanza kutoka ligi daraja la pili basi haitashuka. Hii inaongeza ushindani kwa timu sita hadi nane ambazo za chini ya msimamo kwani zitakuwa zikiitolea macho hadi ile nafasi ya kucheza michezo ya play off na timu kutoka chini. Kama chini ya msimamo kunakuwa na ushindani wa timu nane-kuwania nafasi moja ya upendeleo ya kutoshuka.

Timu nane zinakuwa na nafasi ya kupigania kuingia sita bora, nane nyingine zinakuwa na nafasi ya kupigania kupanda ligi kuu moja kwa moja. Ujerumani, Italia, Romania, Poland, Ubelgiji, Ufaransa, Hispania, Holland, Hispania ni baadhi ya nchi ambazo utaratibu wake wa timu kupanda ligi ya juu zaidi unavutia na TFF kwa kushirikiana na bodi ya ligi wanaweza kutazama huko na kujifunza zaidi na baadae kutumia baadhi ya taratibu nzuri ambazo zitaupendezesha na kuuendeleza mchezo huu nchini.

Kwa vile ligi kuu ya Vodacom kuanzia msimu ujao itakuwa ikishirikisha timu 20 huku zikiwania nafasi moja tu ya ‘ubingwa’ ili kuiwakilisha nchi katika michuano ya Caf, TFF na Bodi ya ligi wanakabiliwa na changamoto kubwa kuhakikisha ushindani unakuwepo. Kama kutakuwa na timu nane ama kumi zenye uwezo wa kushindania taji tutapata ligi bora lakini kama zitaendelea kubaki Yanga, Simba na Azam FC ni wazi hakutakuwa na ligi bora bila kuumiza akili na kutafuta majawabu.

Ligi ya makundi imeshapitwa na wakati na timu ishirini kugombea nafasi moja tu yenye maana ni wazi si rahisi kupata ubora. Hivyo basi ni lazima waendeshaji wakae na wadhamini na kutazama namna ya kuboresha zawadi kwa kila nafasi katika msimamo wa ligi-kuanzia nafasi ya kwanza hadi ya 17.

Mfano, timu itakayomaliza nafasi ya 17 itapata milioni 30, itakayomaliza juu yake itapata kiasi cha juu zaidi hadi kufika kwa bingwa. Timu zitakazomaliza nafasi ya 20 na 19 zawadi yao ni kushuka dara, na ile itakayo maliza nafasi ya 18 ipewe nafasi ya upendeleo kucheza na timu ya tatu ambayo ilipaswa kupanda ligi kuu kutoka ligi daraja la kwanza. Hii itategemea pia na muundo wa ligi daraja la kwanza utakavyokuwa.

Hapa kunasaidia kuwepo na ushindani kwa timu nane chini ya msimamo, lakini pia kutaifanya FDL kuwa na ushindani zaidi na hivyo kutatengenezwa ubora unaotakiwa.

Kuzikataa timu za taasisi moja katika ligi moja

Katika ligi daraja la kwanza iliyomalizika Jumatatu hii kulikuwa na timu nane za Majeshi, timu mbili za taasisi na sita za uraiani. Kulikuwa na timu mbili za Jeshi la Polisi-Polisi Tanzania FC na Polisi Dar FC na bahati mbaya zote zilipangwa kundi moja. Kulikuwa na timu nne za Jeshi la kujenga Taifa (JKT)-JKT Tanzania, JKT Mgambo (zilipangwa kundi moja), JKT Mlale na JKT Oljoro, pia kulikuwa na timu mbili za jeshi la Wananchi-Rhino Rangers na Transit Camp (zilipangwa kundi moja) TFF haipaswi kukubali tena kuona timu za Taasisi moja zikicheza ligi moja.

Inapaswa kuwashinikiza wamiliki wa vilabu hivyo kufuata taratibu zinazokubalika katika uendeshaji wa soka la kisasa hivyo watafute haraka namna ya kuondoa mkanganyiko wa kuwa na timu zenye maslahi mamoja. Kuendelea kuwa na timu za Taasisi moja hakutaweza kutuletea maendeleo yanayotakiwa katika soka japo ni kweli Polisi Tanzania imeshindwa kupanda baada ya kuharibiwa na Polisi Dar iliyoshuka daraja katika mchezo ambao Polisi Tanzania waliondolewa kileleni na kushindwa kururejea tena mechi tatu kabla ya kumalizika kwa ligi.

Isiwe makundi tena

Timu 16 zishindane katika mfumo wa ligi ya mzungo mrefu. Ligi ya makundi hasa kwa ligi muhimu kama daraja la kwanza imepitwa na wakati na kama timu haina uwezo wa kucheza ligi yenye michezo 30 timu hiyo haipaswi kucheza ligi kuu kwani haijiwezi na kama timu haijwezi kuwa nayo ligi kuu ni sawa na kubeba mzigo mzito usiojua unaupeleka wapi.

Hata kama si kwa mfumo nilioupendekeza, TFF na Bodi ya ligi wanapaswa kuhakikisha ligi ya msimu ujao inachezwa kwa mfumo wa ligi na si michuano kama ilivyo sasa. Michezo 14 kuipandisha timu ligi kuu ni michache mno na njia pekee ya kuepukana na hilo ni timu 16 kucheza pamoja zenyewe kwa zenyewe-nyumbani na ugenini.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here