Home Kitaifa Si tu kuifunga Mwadui Jumatano hii, Yanga waelewe bila ubingwa ‘wamekwisha’

Si tu kuifunga Mwadui Jumatano hii, Yanga waelewe bila ubingwa ‘wamekwisha’

7329
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

LICHA ya kushindwa kufika walau fainali ya michuano ya Mapinduzi Cup 2018, mabingwa mara tatu mfululizo na watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara, timu ya Yanga haikuwa na michuano mibaya huko visiwani Zanzibar kwani katika michezo sita waliyofanikiwa kucheza ndani ya siku kumi hawakupoteza mchezo ndani ya muda wa kawaida, huku pia wakipata funzo zaidi kuhusu upigaji wao usioridhisha wa mikwaju ya penalti.

Yanga ilizifunga timu zote nne kutoka Zanzibar na walionyesha namna walivyo na uwezo wa kupambana siku waliyosawazisha dakika za mwisho vs Singida United-timu bora ya michuano hiyo iliyomalizika kwa Azam FC kutwaa ubingwa huo kwa mara ya pili mfululizo wikendi iliyopita.

Waelewe bila ubingwa wameanguka

Kocha msaidizi Shadrack Nsajigwa aliisimamia timu hiyo kuanzia mchezo wa hatua ya 32 bora-kombe la FA dhidi ya Reha FC ambao Yanga walionekana kuhangaika mno hadi kuiondoa timu hiyo ya ligi daraja la pili kwa kuifunga 2-0, akiwakosa wachezaji wake muhimu huku kocha mkuu George Lwandamina akiwa kwao Zambia alikohudhuria msiba wa mtoto wake.

Nsajigwa-nahodha mshindi kiuchezaji klabuni hapo aliiongoza Yanga katika mchezo uliopita wa ligi kuu dhidi ya Mbao FC. Kukosekana kwa kocha Mkuu, Lwandamina katika mchezo dhidi ya Mbao FC kuliwaathiri Yanga lakini huyu alikosekana kwa sababu zisizozuilika. Nsajigwa alimtumia Amis Tambwe katika safu ya mashambulizi licha ya Mrundi huyo kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na matatizo ya goti.

Hakuwa na chaguo bora la klabu msimu huu katika ufungaji Obrey Chirwa alikuwa nje ya timu kwa sababu za kimaslahi. Kuna wakati huwezi kuona madhara ya kukosekana kwa mchezaji kama Chirwa tena katika mechi muhimu. Hii ni kutokana na tabia ‘mbaya’ ya kudharau ambayo watanzania baadhi tunayo.

Kiongozi anaweza kuchukulia kawaida tu kukosekana kwa mchezaji kama Chirwa tena kwa sababu zinazowahusu moja kwa moja kwa kuamini wapo wachezaji wengine wanaweza kuibeba timu. Ndiyo, timu si mchezaji mmoja lakini wakati mwingine hata wakati fulani wa mchezo dhidi ya Mbao kikosi cha Yanga kilionekana kumuhitaji zaidi Chirwa licha ya Mbao kucheza wakiwa pungufu.

Yanga wameshajijengea tabia yao wenyewe ya kutoka chini ya msimamo na kutwaa ubingwa, lakini wasisahau kuwa tabia yao hiyo imekuwa ikiwaletea mafanikio kutokana na msukumo wa pamoja kati ya wachezaji, benchi la ufundi na uongozi na huu ndiyo wakati wao sahihi wa kushikamana zaidi kwani wakianguka watasubiri kwa muda kuiwakilisha nchi katika michuano ya Caf kwa maana FA ni michuano ya ‘patapotea’ huku wakiwa na kumbukumbu ya kukwamia nusu fainali msimu uliopita.

Wasikubali kirahisi kuwakosa wachezaji wao muhimu katika mchezo wowote kwa sababu za kimaslahi. Kama itatokea majeraha kama yanayowakabili Donald Ngoma, Tambwe na Thaban Kamusoko ama adhabu ya kufungiwa aliyokutana nayo Chirwa basi huo ni wakati mwafaka wa wachezaji wengine kuthibitisha uwepo wao katika klabu hiyo.

Yanga wasitosheke kwa mafanikio yaliyopita, bali wayachukulie kama njia ya kuboresha mafanikio zaidi ya klabu. Kuishinda Mwadui FC ni tarajio la wana-Yanga wengi Jumatano hii ili kupunguza gape la pointi tano waliloachwa na timu za Simba na Azam FC, lakini washinde huku wakionyesha kweli ni timu bingwa tetezi yenye kiu ya kufanikiwa zaidi.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here