Home Kitaifa Anguko la Simba liliandaliwa, Omog alikosa meno, Djuma haijui klabu

Anguko la Simba liliandaliwa, Omog alikosa meno, Djuma haijui klabu

11191
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

KUMUACHA Method Mwanjale na kumsaini Asante Kwasi katika usajili uliopita wa dirisha dogo ni muendelezo wa usajili mbovu wa ‘Mr. Kazinyingi’ pale Simba SC. Sitaacha kuwaambia ukweli na huu ni ukweli wangu mwingine kuhusu mwelekeo wa klabu hiyo katika miezi hii mitano kabla ya kumalizika kwa msimu.

Mwanzoni mwa msimu niliandika makala na kusema, Azam FC inaweza kushinda ubingwa wa ligi kuu msimu huu ‘ikipenya’ katikati ya mabingwa mara tatu mfululizo na watetezi wa taji Yanga SC na Simba SC ambayo ndiyo klabu iliyofanya usajili wa gharama kubwa zaidi msimu huu. Baada ya mwenendo wa Mtibwa Sugar FC katika game za mwanzo niliipa pia nafasi timu hiyo bingwa mara mbili ya zamani Tanzania Bara ikiwa watatumia vizuri uwanja wao wa Manungu Complex, Turiani, Morogoro.

Yanga niliwapa nafasi kubwa pia ya kushinda ubingwa wa nne mfululizo kutokana na mseto wao mzuri wa wachezaji na aina ya sajili zao zilizopendekezwa na benchi la ufundi.  Simba sikuipa nafasi ya ubingwa na sababu kubwa iliyonifanya niamini timu hiyo haina nafasi ya kushinda ubingwa ni kuendelea kumkumbatia kocha Joseph Omog, ukosefu wa busara na utulivu.

Kufikia raundi ya 12 ya ligi Simba inaongoza kwa tofauti ya magoli dhidi ya Azam FC. Timu zote hazijapoteza mchezo, zimeshinda michezo saba na kutoa sare mara tano kila moja, zikiwa na alama sare 26. Je, unaamini Simba inakwenda kumaliza ukame wa misimu mitano bila taji la VPL?

Kumuacha Omog ambaye tayari alionyesha udhaifu

Sahau kuhusu sajili ‘bab-kubwa’ zilizosimamiwa na mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu hiyo wakati wa usajili wa dirisha kubwa katikati ya mwaka uliopita. Hadi kesho nitaamini sajili hizo hazikuwa mapendekezo ya kocha Omog na kwa kiongozi anayetaka maendeleo ni lazima atahoji moyoni mwake-huyu kocha vipi? Tunamsajilia wachezaji lakini hasemi chochote.

Omog alikuwa akifanya kazi ‘za waajiri wake’ na si klabu ndiyo maana nilisisitiza mara kadhaa kuendelea kuwa na Mcameroon huyo ni makosa kwa sababu hawezi kuipaisha klabu kwa wachezaji wa kusajiliwa. Omog alipaswa kujiuzulu mwenyewe baada ya kuona anaingiliwa katika kila maamuzi. Alimtaka Yusuph Ndikumana lakini uongozi ukamletea wachezaji wengine watatu tena ambao hakuwahitaji, lakini akakubali kuwapokea.

Omog hakumtaka Haruna Niyonzima kwa sababu aliona timu ikinyanyuka zaidi msimu  huu kwa kuwategemea Mohamed Ibrahim, Said Ndemla, Muzamiru Yassin na Shiza Kichuya ambao waliisaidia klabu kukaribia kutwaa ubingwa msimu uliopita. Lakini kukubali kufanya kazi na wachezaji aliosajiliwa kwa kocha wa kimataifa kama yeye niliamini kunatokana na maslahi binafsi aliyokuwa akipata-kama mshahara na posho.

Nilijua wazi atafukuzwa kwa maana asingeweza kutengeneza timu inayocheza vizuri kutokana na rundo la wachezaji wapya ‘aliosajiliwa.’ Omog alikuwa tayari ametengebneza nusu ya tarajio la timu aitakayo pale Simba na kutokana na kikosi chake kilichopita niliona kocha huyo alikuwa anasumbuliwa na tatizo moja tu-timu kufunga magoli.

Wakati anakuja alikuta tayari kuna wachezaji wamesajiliwa lakini ni wachezaji ambao walimfaa na kama kocha wa kimataifa alipaswa kusimamia usajili na kuhakikisha anapata wafungaji-labda Emmanuel Okwi, Nicholas Gyan, John Bocco lakini kuonyesha hakuwa makini katika kutatua tatizo hilo Laudit Mavugo, Juma Liuzio, wote wamebaki hivyo akalazimika kufanya kazi na washambuliaji saba kwa wakati mmoja jambo ambalo ni aibu kwa kocha mkubwa yeyote.

Kuachwa kwa Mwanjale hayakuwa mapendekezo yake lakini kwa vile hakuwa na ‘meno’ akasifia usajili wa Kwasi ambaye kwa Simba haikuwa na haja naye kutokana na uwepo wa Erasto Nyoni, Yusuph Mlipili, Salim Mbonde,  Mwanjale, Juuko Murshid-ambao ukimtoa Juuko wengine wote walisajiliwa June-Agosti mwaka uliopita.

Kwasi alikuwa pacha wa Ndikumana pale Mbao FC msimu uliopita lakini Omog alimuona Ndikumana kutokana na umakini wa meneja/wakala wa beki huyo raia wa Burundi ‘wapiga’ dili walishindwa kumsaini kwa kigezo kuwa dau lake ni ghali mno-sasa mbona wamemsaini Kwasi kwa pesa zaidi ya aliyotaka Ndikumana? Huku Mghana huyo akiwa mchezaji wa tano kusajiliwa katika beki ya kati ambayo Omog alijua suluhisho ni Ndikumana.

Usajili wa James Kotei haukuwa na mbwembwe nyingi lakini Mghana huyo ni kielelezo tosha kuwa Omog alikuwa na uwezo wa kutazama vizuri wachezaji  na kutengeneza kikosi kama angepewa uhuru wa kufanya hivyo. Ila sikumtaka kwa sababu hakuwahi kuwa imara kama ilivyowahi kuwa kwa makocha wenzake wa kimataifa waliamua kuacha kazi baada ya kuingiliwa katika majukumu yao.

Mzambia Patrick Phiri, Moloto, Papic, Tom Saintifiet, Brandts, Hans van der Pluijm wote hawa wamewahi kuonyesha misimamo yao kwa viongozi wa klabu za Simba na Yanga ambao walidiriki kuwaingilia katika kila majukumu yao ya kujenga  kikosi walichokitaka.

Omog alipaswa kufukuzwa mapema na kisha angepatikana kocha anayestahili kuwaendeleza wachezaji waliosajiliwa ‘ki-holela’ Nilimpenda sana Mganda, Jackson Mayanja-ni kocha ambaye anajua sana kutengeneza kikosi kinachocheza mchezo wa kushambulia na kutawala mechi. Lakini sasa nashangazwa sana kuona Mrundi Masoud Djuma akielekea kupewa majukumu hayo.

Hata kama wanataka kumpima, kwa kweli Simba watajutia zaidi uamuzi wa kumpa majukumu ya ukocha mkuu kocha huyo.

Kwanza anaonekana haijui klabu, hajui tamaduni ya kiuchezaji ya klabu ndiyo maana amekuja na mfumo wa 3-5-2 ambao kwa kweli hauwezi kuleta tija hadi kwa mashabiki ambao wamezoea kuona vikosi vyao vikali vikishambulia mwanzo-mwisho.

Kama Djuma atapewa kukaimu nafasi ya Omog hadi mwishni mwa msimu Simba wanaweza kumaliza nafasi ya nne, tano na pengine ya sita katika ligi hii. Weka hili katika utimamu wako wa akili. Simba waliandaa wenyewe anguko lao kwa kusajili hovyo na kumkumbatia kocha asiye na meno-muoga wa kuhoji.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here