Home Kitaifa Ndanda vs Simba ndio ilipaswa kucheza saa 8 mchana si Lipuli vs...

Ndanda vs Simba ndio ilipaswa kucheza saa 8 mchana si Lipuli vs Shooting

3580
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

KUELEKEA michezo mitatu ya ligi kuu Tanzania Bara leo Jumamosi, mabadiliko ya muda wa baadhi ya michezo kwa kigezo cha kuonekana ‘live’ Azam TV hayako ‘fair’. Mfano mchezo wa Lipuli FC vs Ruvu Shooting ambao umepangwa kuanza saa nane mchana pale Samora Stadium, Iringa.

Kwa mtazamo wa kawaida tu, unaweza kuniambia ipi mechi iliyopaswa kuanza mapema kati ya Ndanda FC vs Simba SC (Nangwanda Stadium, Mtwara) Mtibwa Suga FC vs Majimaji FC (Manungu Complex, Turian,) na Lipuli vs Shooting?

Wingi wa mashabiki viwanjani

Hili ndiyo hitaji linalopigiwa kelele sana hivi sasa na wanasoka. Kumekuwa na uhamasishaji mkubwa ambao umekuwa ukifanywa hadi na vyombo vya habari kuwakumbusha watu umuhimu wa kujitokeza viwanjani. Sikatai Lipuli na Shooting kucheza muda huo kwa kigezo cha michezo mingi ipate kuonekana ‘moja kwa moja’ lakini nani ataenda uwanjani saa nane kutazama mchezo kama huo wakati hata katika muda wa kawaida uliozoeleka Tanzania bara (mechi kuchezwa saa kumi jioni) watazamaji husuasua.

TFF inapaswa kulitazama hili kwa umakini mkubwa kama kweli wanataka kuwarejesha watazamaji viwanjani. Kama dhamira hasa ni kuonyesha michezo mingi basi ile ya timu kubwa za Yanga SC na Simba ndiyo inapaswa kuchezwa mapema zaidi kwa kuwa timu hizi zina mashabiki wengi ambao hata wakiambiwa timu yao itacheza saa tano asubuhi watajitokeza tu uwanjani, lakini si kwa wale wa Lipuli na Shooting.

Kuzinyima mapato klabu ndogo

Timu kama Lipuli kwa sasa huwezi kukataa kuwa wanategemea kwa kiasi kikubwa kuendesha klabu kutokana na pesa zinazopatikana kutoka katika mapato ya milangoni. Hata ‘wakubwa’ Yanga na Simba hutegemea mapato ya milango kukava baadhi ya maeneo ya kiuchumi klabuni mwao.

Kuwachezesha klabu ndogo tena zikicheza wenyewe kwa wenyewe katika soka la sasa hapa Tanzania ni uonevu mkubwa. Nimewahi kucheza muda huo, najua nini nachomaanisha hapa. Unadhani hata hao Yanga ama Simba wanaweza kukubali kucheza saa nane mchana wakati ipo fursa ya wao kukosa mapato na kupata mengi ikiwa watacheza jioni? Tafakari.

Uamuzi huu unaweza kuwa na faida zaidi kwa wafuatiliaji wa ligi kwa maana watakuwa wakiona nini kinaendelea viwanjani, lakini hatupaswi kulazimisha kwa sasa na kama tutalazimisha tuanze hivyo kwa game za timu kubwa kama wanavyofanya kwingineko barani Ulaya.

Kuzichezesha timu ndogo kama Lipuli kwa muda wa mchana ‘angavu’ si tu unawanyima haki yao ya kimsingi-kuchagua muda wa mchezo kuanza kama wanavyofanya Azam FC, lakini pia timu hizi zinakosa mapato kwani muda huo kila uwanja wa Tanzania huwepo jua kali na watu kukimbia joto hilo la jua. TFF inapaswa kuangalia upya kuhusu hili la muda wa baadhi ya michezo kama kigezo ni kuonekana kwa mechi nyingi basi kwa leo Ndanda vs Simba ilipaswa kuchezwa mchana si Lipuli vs Shooting.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here