Home Kitaifa Urudishiwe unahodha wako, Mkude ‘mwalimu wako’ mzuri ni James Kotei, kama Makapu...

Urudishiwe unahodha wako, Mkude ‘mwalimu wako’ mzuri ni James Kotei, kama Makapu alivyomfunza Telela

17577
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

WAKATI mbinu za kocha Hans van der Pluijm zilipoanza ‘kukubali’ mwanzoni mwa mwaka 2015, uchezaji wa haraka haraka huku akipiga pasi na kusogea mbele wa Salum Telela kama kiungo-wa chini-mzuiaji niliamini ndiyo siri ya Yanga SC kuanza kucheza mchezo wa kupendeza.

Lakini ghafla Telela akawa anaachwa nje huku kiuchezaji Said Juma Makapu akionekana kucheza zaidi mchezo wa kupiga pasi na kubaki katika maeneo yake ya ulinzi katikati ya uwanja.

Nilimuuliza siku moja moja Telela, ‘Una tatizo lolote la majeraha yanayosababisha usicheze?’ Telela ni kati ya wachezaji ambao wanapenda kukubali ukweli na kuufanyia kazi, alinijibu, “Kocha ameniambia nimtazame Makapu anavyocheza.” Kwangu lilikuwa jibu kamilifu na mara moja na mimi nikaanza kumtazama kwa umakini mkubwa na kumfuatilia Makapu.

Nilichokuja kugundua na ambacho nilikuja kumwambia pia Telela, “Kocha anataka ucheze zaidi katika eneo la ulinzi hata kama unashambulia.” Makapu ni mchezaji ambaye kazi yake uwanjani kwa mbinu za Hans ilikuwa ni kusaidia zaidi uimara wa beki ya kati wakati huohuo akianzisha pasi sahihi kwa kiungo wa mashambulizi ama kushambulia kwa pasi za mbali.

Telela alikuja kuwa mchezaji muhimu katika mbinu za Hans kabla ya ujio wa Thaban Kamusoko, na hilo lilichangiwa na yeye mwenyewe kujifunza kutoka kwa uchezaji wa mchezaji mwenzake tena wakati huo Makapu akiwa kina wa U20.

Kuchanganya kwake style yake ya ushambuliaji na ile ya uzuiaji ya Makapu kulimjenga zaidi Telela na kuonekana mchezaji ambaye anaweza kulinda beki yake, kuanzisha mashambulizi na kushambulia kwa pasi timilifu za umbali mrefu.

Ni zamu ya Jonas mkude kujifunza kutoka kwa James Kotei

Kabla ya ujio wa Mghana, James Kotei katika kikosi cha Simba mwaka mmoja uliopita, Jonas Mkude alikuwa si tu nahodha wa kikosi hicho bali mchezaji ambaye ni nadra kumuona nje ya kikosi kinachoanza mchezo.

Nakumbuka moja ya nukuu ya Mkude wakati alipofanya mahojiano na mwandishi mmoja nchini kuwa, hatishiki na ujio wa Mghana huyo na yuko tayari kupambana kuitunza nafasi yake kama kiungo-mlinzi wa Simba.

Wakati Mkude alipotangazwa kuwa nahodha wa timu kuchukua nafasi ya Hassan Isihaka katikati ya mwaka 2015, nilipingana na uamuzi huo kwa kuamini mchezaji huyo hajafikia ukomavu wa kubeba majukumu hayo makubwa katika timu.

Ulikuwa ni wakati ambao Mkude hakuwa katika kiwango bora huku yeye mwenyewe akishindwa kujiongoza katika maisha ya nje ya uwanja. Iliripotiwa mara kadhaa kuhusu tabia yake ya nje ya uwanja. Pia hata uwanjani Mkude licha ya kuonekana ni mchezaji wa kikosi cha kwanza lakini ndani ya uwanja hakuwa bora.

Alikuwa ni kati ya wachezaji waliokuwa wakipoteza sana mpira huku pasi zake nyingi zikienda mahala si sahihi. Ujio wa Kotei ulikuja wakati mwafaka, kwanza kumfundisha Mkude jinsi ya kucheza kwa nguvu, umakini, kujituma, na kutofanya makosa mengi ya kupoteza mpira katika eneo hatarishi la timu yake.

Kotei namchukulia kama ‘nahodha asiyevaa beji’ kutokana na jinsi anavyocheza kwa kujituma huku akiwahamasisha wenzake na kuwakumbusha mara kwa mara kuhusu umakini mchezoni. Anajua kuzuia na inapotokea akashambulia hushambulia kwa malengo ambayo ni mara chache hafanikiwi.

Mkude ameonekana kujituma hasa baada ya kutokuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza mbele ya Mghana huyo na katika michezo michache aliyopata nafasi ameonyesha ni kiasi gani anaweza kushindana na Mghana huyo na kushinda vita ya namba-japo si rahisi tena.

Kotei amekuwa na uwezo wa ziada wa kucheza nafasi zote tano za nyuma-kuanzia namba 2 hadi 6, lakini huonekana mchezaji kamilifu wakati anapokuwa akicheza katika nafasi ya kiungo.

Mkude anaweza kumshinda Mghana huyu kwa sababu ana kipaji cha ziada katika ufundi na mbinu, lakini ni lazima akubali kumfuatila Kotei na kujifunza namna ya kucheza kama kiongozi uwanjani, mpambanaji na kutokuwa tayari kupoteza hovyo mpira.

Inawezekana kocha wake Joseph Omog hajampatia siri ya yeye kupoteza nafasi mbele ya Kotei lakini kama atatulia na kumtazama Mghana huyo jinsi anavyopambana uwanjani na kupiga pasi za uhakika zenye malengo chanya bila shaka Mkude atakuwa mchezaji ambaye anastahili kuwa kiongozi wa wenzake-nahodha.

Amekuwa sehemu ya timu hiyo kwa misimu sita sasa, hivyo kuona akivuliwa kitambaa na kupewa ‘kibabu’ toka ng’ambo ya nchi ilikuwa ni sawa na funzo ambalo Sir Alex Fergus alimpitisha Wayne Rooney wakati wa ujana wake kiuchezaji-kabla ya baada kuwa nahodha mzuri wa Manchester United. Mkude aongeze jitihada zake, ajifunze kutoka kwa Kotei atamshinda raia huyo wa Ghana kwa maana hakuna mwalimu mwingine mzuri zaidi ya yeye mwenyewe.

Telela alikuja kumpiku tena Makapu baada ya Hans kumwambia tu, ‘mtazame Makapu’ anavyocheza. Ilikuwa ni ujumbe ulio wazi kuwa ‘hapaswi’ kucheza mbali na eneo lake hata kama atashambulia.

Tatizo kubwa la Mkude ni kucheza kivivu, kupiga pasi mkaa-moja nzuri-mbili mbovu, kutowahamisha wenzake na wakati kocha anapoona hivi huku kukiwa na mchezaji anayeweza kufanya hivyo kwa walau asilimia 70 atampa nafasi.

Mrudishieni Mkude kitambaa chake cha unahodha baada ya kutemwa kwa Mzimbabwe Method Mwanjale ambaye alipewa nafasi hiyo baada ya kuvuliwa Mkude katikati ya mwaka huu.

Upande wangu, Mohamed Hussein bado hana sifa za kuwa nahodha na utakaponiuliza ni nani sasa anafaa nje ya Mkude nitakwambia, Mganda Juuko Murshid au Mghana, Kotei ikiwa Mkude atachukua funzo la Telela kwa Makapu na kuliweka akilini.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here