Home Kitaifa Huu si wakati mwafaka wa kumuachia Mwinyi Haji aondoke Yanga

Huu si wakati mwafaka wa kumuachia Mwinyi Haji aondoke Yanga

9742
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

IMEKUWA ni bahati kubwa kumuona, Gadiel Michael akicheza kwa zaidi ya miezi sita mfululizo pasipo kupata majeraha. Mlinzi huyo wa kushoto wa Yanga alikuwa na misimu mitano migumu Azam FC kutokana na balaa la majeraha ambayo yalikuwa yakimuandama kila baada ya muda jambo ambalo lilitishia kukua kwa kipaji chake.

Tangu alipochukua nafasi ya Mzimbabwe, Bruce Kangwa aliyekuwa katika michuano ya AFCON 2017-Gabon na kikosi cha Zimbabwe mwezi Februari, Gadiel amekuwa akicheza mfululizo pasipo kupata majeraha. Kitendo cha kucheza bila maumivu kulifungua tena nafasi yake katika timu ya Taifa ya Tanzania na ile ya Tanzania Bara huku akiwa chaguo la kwanza mbele ya Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr.’

Yanga ilimsaini Gadiel, Septemba mwaka huu akitokea Azam FC na uwepo wake umemfanya aliyekuwa mlinzi chaguo la kwanza katika beki ya kushoto klabuni hapo, Mwinyi Haji kupoteza nafasi yake.

Mwinyi ambaye alikuwa akichuana na Oscar Joshua katika nafasi hiyo kwa misimu mitatu mfululizo sasa ameshindwa kabisa kumuondoa Gadiel na hivyo kushindwa kuichezea Yanga mchezo wowote kati ya 11 iliyopita katika ligi kuu msimu huu.

Licha ya kutotumika klabuni kwake, kocha wa timu ya Taifa ya Zanzibar, Hemed Morocco alimjumuhisha mlinzi huyo mwenye uwezo wa juu katika upigaji wa krosi katika kikosi chake ambacho kilishiriki michuano iliyomalizika wikendi iliyopita ya Senior CECAFA Challenge Cup 2017 nchini Kenya.

Katika michuano hiyo ambayo Zanzibar Heroes walifanikiwa kufika fainali nakupoteza mbele ya wenyeji kwa changamoto ya mikwaju ya penati waliweza kuonyesha kiwango kizuri jambo ambalo limewafanya baadhi ya wachezaji kutakiwa na klabu kadhaa za huko Kenya.

Mwinyi ni kati ya wachezaji wa Zanzibar Heroes ambao wanatakiwa na AFC Leopards. Kwanza ifahamike Leopards ni kati ya timu nne kubwa Afrika Mashariki hivyo kitendo cha mchezaji huyo kutakiwa na klabu hiyo ni jambo zuri lakini kwa sasa nadhani Yanga haipaswi kumruhusu mlinzi huyo wa kushoto kuondoka kwa maana hakuna muda wa kutafuta mbadala wake.

Usajili wa Caf tayari umefungwa hivyo kitendo cha kukubali kumuuza Mwinyi itakuwa ni kosa kwa maana hakutakuwa na mchezaji mbadala wa Gadiel endapo itatokea tatizo la kadi ama majeraha.

Yanga wasijidanganye kwa kuamini Gadiel anaweza kuwa bora kwa msimu mzima ndiyo maana nasisitiza hawapaswi kumuachia Mwinyi hivi sasa labda kama kungekuwepo na mbadala wake.

Bahati mbaya ni Geofrey Mwashuiya pekee ambaye anaweza kucheza nafasi ya beki namba tatu lakini wing huyu wa kushoto si mzuri katika uzuiaji hivyo Yanga hawapaswi hata kufikiria kuhusu barua ya Mwinyi ambaye ameiandikia klabu yake akiomba aruhusiwe kuondoka ili kujiunga na klabu hiyo kubwa ya Kenya.

Kuna FA Cup, ligi kuu na mapema mwaka ujao watakuwa wakicheza Caf Champions league hivyo kuwa na michuano yote hii kunaweza kuongeza uchovu na majeraha kwa kikosi chao wakati wowote huku rekodi ya nyuma ya Gadiel ikinipa shaka kama anaweza kucheza vyema kama sasa kwa miezi sita iliyobaki msimu huu.

Ndiyo maana nasema huu si wakati mwafaka wa Yanga kumuachia Mwinyi kwani hawatapata mbadala wake jambo ambalo linaweza kuja kuwagharimu mbeleni.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here