Home Ligi Miezi 13 tangu aondoke Afrika Kusini, Ndanda FC ni klabu ya tatu...

Miezi 13 tangu aondoke Afrika Kusini, Ndanda FC ni klabu ya tatu ya chini kwa ‘Robinho wa Tanzania’

10146
0
SHARE

Na Baraka Mbolembole

MIEZI 13 tangu aliposhinikiza kuvunjwa kwa mkataba wake wa miaka mitano Free State Stars ya ligi kuu Afrika Kusini, kiungo-mshambulizi, Mrisho Ngasa amejiunga na klabu yake ya tatu na ya nane katika kipindi cha miakla 12 ya uchezaji wake soka la ushindani.

Wakati Kagera Sugar FC ilipomsaini Ngasa mwaka 2005 akitokea Mwanza haikutarajiwa kama angechukua muda mfupi kuwa staa mkubwa katika soka la Tanzania huku akiwa mchezaji muhimu wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kilichoshirikifainali za kwanza za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani-CHAN 2009, Ivory Coast.

‘Robinho’ huyu wa Tanzania alisajiliwa Yanga baada ya msimu mmoja tu tangu aanze kucheza ligi kuu Tanzania Bara mwaka 2006. Usajili wa Ngasa ulikuwa ukihitimisha misimu saba ya mafanikio kwa kiungo Said Maulid ‘SMG’ katika kikosi cha mabingwa hao mara 27 wa kihistoria.

SMG alikuwa wing-namba saba mahiri zaidi katika soka la Tanzania kati ya mwaka 2000 hadi 2007, lakini Ngasa katika pambano la raundi ya kwanza la Caf Champions League 2007 kati ya Yanga na Petro Atletico ya Angola vilifanya mashabiki wengi wa soka nchini kumuhusu Ngasa ambaye ndiyo kwanza alikuwa U19.

Aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Mbrazil Marcio Maximo anaweza kuwa mshindi katika vita yake dhidi ya wachezaji mastaa wakati huo akiinoa Stars, Athumani Idd ‘Chuji’, Haruna Moshi ‘Boban’, na golikipa bora zaidi kuwahi kutokea nchini katika karne mpya, Juma Kaseja lakini shinikizo ambalo alipata kutoka kwa mashabiki walihoji kila mara kuhusu kutojumuhishwa kwa jina la Ngasa katika teuzi zake za vikosi lilimshinda hivyo miezi sita baada ya kiwango cha juu dhidi ya waangola hao Machi, 2009 Ngasa alikuja kuitwa kikosini na huko pia akaonekana ‘mtu anayeenda kumaliza uwepo wa SMG’ katika timu ya Taifa.

Licha ya kusema mara kadhaa kuwa wakati wa Ngasa kuichezea Stars bado haujafika, Maximo yeye mwenyewe aliishia kumpachika jina la Mbrazil mwenzake Robinho de Souza ambaye alikuwa akichukuliwa kama ‘Pele Mpya.’

Ngasa ni mchezaji ambaye alitumia kasi yake vizuri uwanjani. Stahili yake ya kushambulia akitokea pembeni ya uwanja ilifanya afunge magoli mengi kwa sababu mabeki wa timu pinzani walishindwa kuendana na kasi yake iliyoambatana na ufundi mwingi wa kumiliki mpira.

Ngasa ni kati ya viungo washambuliaji waliopata kushinda tuzo kadhaa za ufungaji bora. Ameshinda tuzo ya ufungaji katika michuano ya CECAFA Challenge Cup mara kadhaa, pia alifunga magoli 16 na kushinda tuzo ya ufungaji bora katika ligi kuu Bara msimu wa 2010/11.

Huyu ni mhezaji aliyefunga magoli mengi zaidi akiichezea Taifa Stars kama takwimu zikikusanywa, lakini kwa sasa ni ‘aibu’ kwake kujiunga na Ndanda FC timu ambayo inacheza ligi ili kupigania kutoshuka daraja.

Ngasa ameshindwa hata kwenda Mtibwa Sugar FC, Kagera Sugar FC timu ambazo zimekuwa zikiwaokoa wachezaji wengi waliopotezwa ama kujipoteza kimpira na kuwafanya wawe washindani tena. Kitendo cha yeye kusajiliwa kwa mkataba wa miezi sita tu kinaonyesha ni kiasi gani hakuwa na thamani tena baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa mwaka mmoja na Mbeya City FC.

City ni timu nyingine ya chini ambayo hakupaswa kujisajili nayo hasa ukizingatia ni yeye mwenyewe aliyeomba kuvunjwa kwa mkataba wake uliokuwa umesalia miaka minne Free State. Kung’aniza kuondoka Afrika Kusini mahala ambako si tu ni salama kwa kipaji chake, bali alikuwa akipewa kila kitu hata zaidi ya kile alichokuwa akipata Yanga na Azam FC.

Kuichagua Fanja FC ya Oman kwa hakika ni ‘juto’ ambalo kamwe Ngasa hatakuja lisahau kimpira hasa ukizingatia tayari alikuwa amesogea kiumri huku Yanga-klabu anayoipenda zaidi ikiwa tayari inatazama njia nyingine kwa kuwaamini vijana kama Saimon Msuva ambaye sasa anacheza ligi kuu ya Morocco katika klabu ya Al Jadida.

Ngasa alipotoka Afrika Kusini mwezi Septemba, 2016 aliamini atasajiliwa kwa mara ya tatu na klabu ya ndoto zake, lakini aliyekuwa kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm alizuia hilo kwa kuwaambia uongozi uliokuwa unampigia debe kuwa, kumrudisha Ngasa ni sawa na kuwaua kimpira Msuva, Geofrey Mwashuiya na vijana wengine ambao tayari alikuwa amewatazama kwa jicho la tatu kwa Yanga ya sasa na baadae pia.

Kutangatanga kwa Ngasa hivi sasa ni matokeo ya kupenda kupita kiasi. Licha ya kuzichezea Kagera Sugar (20005-2006), Yanga (2006-2010), Azam (2010-2012), Simba (2012-2013) kwa mkopo, Yanga (2013-2015), Free State (2015-2016,) Fanja (Oktoba 2016-Novemba 2016,) Mbeya City (Desemba 2016-Desemba 2017,) na sasa Ndanda FC hakuwezi kuondoa ukweli kuwa mchezaji huyo bora wa pembeni kwa wakati wake nchini hakuwahi kuwa na washauri wazuri, ama yeye mwenyewe aliendekeza mapenzi yake kwa klabu ya Yanga tu na kusahau soka linachezwa kwa wakati na muda hausimami.

Kwa mchezaji ambaye Gianfranco Zola alimtabiria mafanikio wakati alipokuwa West Ham United ya England kwa majaribio miaka tisa iliyopita, kuchezea Ndanda FC si jambo baya kwake lakini ni kwa nini Ngasa si mshindani tena? Miezi 13 klabu tatu! Ya nne itafuta Juni mwaka ujao panapo majaliwa, ni kwanini? Kuanguka kwake ni sawa na anguko la falme ya Haile Selassie pale Ethiopia. Nakukubali sana ‘Mrisho Khalfan Ngasa wa Mwanza’

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here