Home Kitaifa Yohana Mkomola ‘ingizo’ lingine bora linalopaswa kuwakumbusha uelekeo wa Yanga

Yohana Mkomola ‘ingizo’ lingine bora linalopaswa kuwakumbusha uelekeo wa Yanga

6924
0
SHARE

NA Baraka Mbolembole

SIJAWAHI kumuona Fiston Kayembe akicheza, lakini kwa ‘timu ya ufundi’ ambayo ilikuwa karibu na raia huyo wa DR Congo kwa wiki kadhaa watakuwa wameridhisha na kuona mlinzi huyo wa kati anafaa kuongeza nguvu katika safu hiyo kwa kushirikiana na Kelvin Yondan, nahodha Nadir Haroub, kijana Pato Ngonyani na Vicent Andrew.

Katika raundi kumi za awali katika ligi kuu Tanzania bara msimu huu, Kelvin, Andrew, Pato na Nadir wote wamefanikiwa kucheza lakini bado kuna walioamini kocha George Lwandamina anapaswa kuongeza ‘mtu mpya’ ambaye atakuwa na uwezo wa kuongoza safu yote ya ulinzi. Kama, Kayembe anafaa hilo litakuwa jambo zuri kwa wawakilishi hao wa Tanzania katika Caf Champions League 2018.

Yohana Mkomola ni ingizo ‘bab-kubwa’, pengine inatosha sasa

Lingekuwa jambo la kushangaza sana Yanga kumsaini tena mlinzi raia wa Togo, Vicent Bossou ambaye ni mchezaji wa kwanza wa kigeni kususia kucheza mechi msimu uliopita kutokana na ucheleweshwaji wa mishahara. Elias Maguli si ‘straika wa Yanga’ japokuwa ni mshambulizi mzuri, kwa Daniel Lyanga labda angefaa, ila usajili wa  kijana U18, Yohana Mkomola  ulihitajika.

Kwa wafuatiliaji wa makala zangu watakuwa wanafahamu ni vipi nimekuwa na ‘shahuku’ ya kutaka kuona Yanga ikicheza mechi ikiwa na wachezaji 11 wa kitanzania katika kikosi kinachoanza mchezo. Si kwa maana ya ‘uzalendo’ kwanza, la hasha hivi sasa kuna vijana wa kitanzania ambao wanaweza kuchukua pesa za klabu zetu kubwa na kuwapa mataji ya ndani mbele ya wachezaji raia wa kigeni.

Japokuwa si shabiki wa Yanga ila nakumbuka tangu kuingia kwa Yusuph Manji kama mfadhili wa timu hiyo yapata miaka 12 iliyopita kuna wachezaji wengi sana wa kigeni wamesajiliwa na wengine kuachwa ndani ya muda mfupi kutokana na kushindwa kufanya kile kilichotarajiwa. Ilifikia wakati ambao kocha Mserbia, Dusan Kondic licha ya kutambua kanuni za usajili wa wachezaji wa kigeni nchini kuruhusu-wachezaji kumi tu,  yeye alisajili wachezaji 12 mwaka 2010.

Hii yote ilikuwa ni kuifanya klabu kupenya miongoni mwa timu nane bora katika soka la Afrika (kufika walau hatua ya makundi) lakini kwa kipindi chote hicho Yanga imefanikiwa kufika nane bora ya michuano ya  Caf mara moja tu (mwaka 2016) ilipotolewa hatua ya 16 bora ya Champions league na kuangukia katika ‘play off’ ya Confederation Cup ambako walivuka.

Hii ina maanisha wachezaji wengi wa kigeni licha ya kusainiwa na kulipwa kiasi kikubwa cha pesa, bado wameishia kuisaidia klabu kutawala soka la ndani ya Tanzania na Afrika Mashariki na Kati pekee. Jambo hili linaweza kufanywa na vijana wa Kitanzania. Wanachohitaji ni kujitunza, kupambana na kuwa tayari kufikia ndoto zao na ndoto za soka la kulipwa hutimizwa kirahisi pale klabu inapofika mbali katika michuano ya kimataifa.

Usajili wa Mkomola ni nyongeza muhimu katika safu kali ya mashambulizi pale Yanga. Kijana huyu anaweza kupenya haraka katika kikosi cha kwanza kwa sababu ana uwezo wa kucheza vyema katika mifumo ya 4-4-2 na 4-3-3.

Sikuhitaji na sitapenda kuona Yanga ikimuacha mchezaji yoyote yule katika safu yao ya mashambulizi lakini ujio wa Mkomola unaweza kuwafanya wamruhusu Matheo Anthony kuondoka hata kwa uhamisho wa mkopo kwa maana hajatumika kwa misimu miwili na nusu sasa jambo ambalo wakati mwingine linasababishwa na kukata tama kwa mchezaji kutokana na ushindani uliopo.

Mkomola anaweza kucheza na Chirwa, Donald Ngoma, Amis Tambwe, au Ibrahim Ajib ni yeye mwenyewe anayeweza kuamua kwa kujituma kwani sababu za kusajiliwa kwake ziko wazi-ni mfungaji kijana mwenye shabaha, kasi, nguvu na uwezo wa kukimbiza mpira. Yanga ilihitaji nyongeza ya mshambulizi? Hapana, lakini usajili huu wa Mkomola ni sahihi kwa maana unakuja wakati ambao klabu inateswa na majeraha ya wachezaji wao nyota. Sasa inatosha, waachane na huyo Bwalya.

Ieleweke Yanga wanapoelekea

Ni kusuka kikosi bora ambacho kitawahusu zaidi wachezaji wazawa. Unaweza usione mabadiliko makubwa ya timu ya Yanga iliyoshinda mataji manne katika misimu mitano iliyopita ya VPL kama utatazama ‘juujuu’ lakini ukichunguza kwa makini tayari Lwandamina ametengeneza timu mpya na bahati nzuri amekutana na utawala ambao unaweza kumsikiliza, kushauriana kuhusu mambo ya usajili.

Leo hii Yanga ina, Juma Abdul, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Mwinyi Haji, Kelvin, Nadir, Pato, Andrew, Said Makapu, Juma Mahadhi, Pius Buswita, Rafael Daud, Ibrahim Hajib, Yusup Mhilu, Emmanuel Martin, Geoffrey Mwashuiya, Matheo, Ramadhani Kabwili, Beno Kakolanya na wazawa hawa wameonyesha kuwa wanaweza kufanya vizuri na kama kikosi hicho kitaendelea kuwa pamoja kuanzia msimu ujao watakuwa moto sana.

Mtibwa Sugar FC, Kagera Sugar FC, JKT Ruvu, Tanzania Prisons Mbeya City FC ni baadhi ya timu ambazo kwa nyakati tofauti zilituonyesha kiwango kizuri cha soka la kutandaza chini wakati zilipokuwa na vikosi vya wachezaji wazawa waliokaa pamoja kuanzia miaka miwili. Hivyo hata kwa Yanga wanaweza kuwa hivyo japokuwa wataendelea kusaini na kuhitaji huduma ya wachezaji kutoka ng’ambo.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here