Home Kitaifa Anachofanya Mudathir ndio maana halisi ya mchezaji kutolewa kwa mkopo

Anachofanya Mudathir ndio maana halisi ya mchezaji kutolewa kwa mkopo

10640
0
SHARE

Ukifuatilia wachezaji kadhaa waliowahi kutolewa kwa mkopo, Mudathir Yahya ameonesha tofauti kubwa sana hata mabosi wake pale Azam watakuwa wanatamani kumrudisha kwenye kikosi chao. Utofauti ninaouzungumzia hapa ni kwamba, wachezaji wengi ambao hutolewa kwa mkopo biashara yao na klabu zao (zilizowatoa kwa mkopo) huwa ndio imemalizika.

Kibongo-bongo kumtoa mchezaji kwa mkopo hutumika kama kichaka cha kumalizia shgughuli na mchezaji husika, baadhi ya timu wanatumia vizuri usajili wa mkopo lakini timu nyingi zinapomtoa mchezaji kwa mkopo huwa harudi tena.

Mchakato wa kumtoa mchezaji kwa mkopo kwenda klabu nyingine huwa una mambo mengi nyuma yake, malengo pia yanatofautiana, timu inayomchukua mchezaji inakuwa inamuhitaji kwa wakati huo kwenda kumtumia kutokana na mapungufu ya mchezaji wa namna hiyo ambaye yupo kwenye timu nyingine lakini hatumiki labda kwa kukosa nafasi kwa hiyo atakapokwenda kwao atapata nafasi.

Faida inakuja kwa pande zote mbili wale wanaopata wanakuwa wamepata mtu sahihi wa kuwafanyia kazi na kule anakoondoka wanakuwa wamepata faida inawezekana ikawa mara mbili. Faida ya kwanza mchezaji wao anakuwa amepata fursa ya kwenda kukuza kiwango chake lakini pia faida nyingine inaweza kuwa wakapata nafuu kwenye gharama za kumhudumia mchezaji husika.

Inawezekana klabu ikawa na mchezaji inamlipa inatumia gharama zingine lakini mchezaji hatumiki hivyo inakuwa ni hasara kwa klabu, kwa hiyo akitolewa kwa mkopo akawa analipwa na klabu iliyomchukua (lakini hapa inategemea na makubaliano ya timu mbili) lakini lengo mama la timu inayomtoa mchezaji kwa mkopo ni kuhakikisha kiwango chake kinaongeza kwa sababu atapata fursa ya kucheza.

Timu inayomtoa mchezaji kwa mkopo inaweza ikaweka sharti kwamba, mchezaji wao lazima acheze kama atakuwa fit, (huyu mchezaji ni muhimu kwetu lakini kutokana na ufinyu wa nafasi anashindwa kutumikakwa hiyo akija huko lazima mumtumie). Miongoni mwa majukumu ya kocha ni kupandisha viwango vya wachezaji, mchezaji aliyetolewa kwa mkopo anaweza kukutana na kocha ambaye anauwezo mkubwa wa kupandisha viwango kwa wachezaji kaaminiwa na kujengwa.

Mudathir ametoka Azam kwenda Sindida United akapewa kitambaa cha unahodha (nahodha wa Singida ni Nizar Khalfani lakini hapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza) hii inaashiria kwamba, mwalimu na benchi la ufundi wameonesha imani kubwa juu yake, kwa hiyo wanamuongezea majukumu.

Kwa upande wa pili kitambaa cha unahodha kinaweza kuwa kimempa deni Mudathir akajiuliza mimi nimefika hapa kwa mkopo nimewakuta wachezaji lakini napewa jukumu uongozi akaona ni imani iliyopitiliza hivyo anajitoa kwa uwezo wake wote kuhakikisha timu inapata matokeo.

Wakati Mudathir anaondoka kwa mkopo, Azam walimsajili Salmin Hoza (kutoka Mbao FC) katika nafasi ileile aliyoiacha Mudathir, swali la kujiuliza ni kwamba, kulikuwa na sababu gani ya kumtoa Mudathir kama kulikuwa na wachezaji wa ziada katika nafasi husika? Kwa nini walimtoa mchezaji (Mudathir) wakamleta Hoza katika nafasi ileile?  Wakati huo kuna Kingue, Himid, Domayo wote wanacheza nafasi hiyo, labda ilikuwa ni nia njema ya Azam kulinda kiwango cha Mudathir kutokana na uwepo wa wachezaji wengi katika nafasi anayocheza Mudathir.

Mudathir ameonesha kiwango kikubwa tangu alipojiunga na Singida United, amekuwa msaada mkubwa katika eneo la kiungo la timu hiyo huwezi kutaja mafanikio ya Singida United bila kumtaja kijana huyu kutoka Zanzibar.

Ubora wake kwenye kikosi cha Hans van Pluijm ulimshawishi kocha wa timu ya Taifa Stars Salum Mayanga kumuongeza kwenye kikosi chake baada ya kukosekana Erasto Nyoni  na Mzamiru Yassin kabla ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Benin mwezi uliopita. Alichokifanya kwenye mchezo huo uliochezwa ugenini kimebaki kuwa historia.

Kwa sasa yupo na kikosi cha Zanzibar Heroes kinachoshiriki kombe la Chalenji nchini Kenya, Mudathir akiwa katika ubora wa hali ya juu alitamba kwenye eneo la kiungo akisaidiana na Mohammed Issa ‘Banka’ na kuwafunika Rwanda. Alifunga goli la kwanza katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa Zanzibar kuibuka washindi kwa bao 3-1.

Asante Mudathir kwa kutuonesha maana halisi ya mchezaji kutolewa kwa mkopo.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here