Home Kitaifa Mtazamo wa Shaffih Dauda kuhusu sinema ya Ngoma na Yanga

Mtazamo wa Shaffih Dauda kuhusu sinema ya Ngoma na Yanga

13376
0
SHARE

Ishu ya Ngoma kuondoka huku klabu yake ikiwa haina taarifa zake inatafsiriwa tofauti na kila mmoja, mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe aliondoka nchini na kuelekea nchini kwao kisha kukaa kwa muda huku uongozi wa Yanga ukiwa haujui kinachoendelea, kwa sasa amerejea na kupokelewa na klabu yake akiwa na ripoti inayoeleza alikuwa akitibiwa majeraha yake yanayomsumbua. Hadi sasa bado uongozi wa Yanga haujatoa tamko rasmi kuhusu hatua za kinidhamu zitakazochukuliwa dhidi ya mshambuliaji huyo.

Mchambuzi wa masuala ya michezo Shaffih Dauda amezungumzia sakata hilo la Ngoma na Yanga, japo hakusema waziwazi nini kinatakiwa kufanyika lakini mtazamo wake unaonesha klabu inapaswa kuchukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya Ngoma ili iwe fundisho kwake na kwa wachezaji wengine. Lakini kwa upande mwingine Dauda ameeleza inaweza kuwa ngumu kwa Yanga kutoa adhabu kwa Ngoma endapo mchezaji huyo anaidai klabu.

“Mchezaji anaondoka bila taarifa halafu anakuja na ripoti ambayo anaijua yeye na daktari wake na akapokelewa, inaonesha udhaifu na inaashiria ndani ya klabu hakujatengemaa, kuna matatizo makubwa. Namna Mkwasa anavyozungumzia suala la Ngoma inaashiria amekata tamaa.”

“Mchezaji ambaye ana mkataba halali na klabu anaondoka vipi kwenda kusikojulikana bila uongozi wa timu yake kupewa taarifa? Anakaa siku anazotaka mwenyewe, anarejea na kupokelewa, lazima kuna tatizo.”

“Ipo siku anaweza akaamua kutohudhuria mazoezi kwa makusudi, kama anaweza kuondoka bila taarifa na kukaa zaidi ya mwezi anarejea na ripoti ya daktari, atashindwaje kukacha mazoezi halafu akasema sikuwa sawa nilikuwa nahisi kuumwa nikaenda zahanati nimegundulika nina Malaria. Wakati mwingine viongozi huwa wanawalea wenyewe hawa wachezaji.”

“Inawezekana kuna matatizo mengine, kwa uzoefu wangu, mchezaji kufika hatua hiyo unaweza ukasikia hajalipwa mshahara wake kwa miezi miwili au mitatu, kwa hiyo na yeye anakuwa na jeuri anaweza akasema kama hamjanilipa hadi sasa mnategemea mimi naishije na familia yangu?”

Hivi karibuni zilienea tetesi kwamba, huenda Ngoma ataachwa katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili kutokana na uongozi wa Yanga kuchoshwa na tabia za nyota huyo kuondoka bila kutoa taarifa. Ikaelezwa kocha mkuu wa Yanga George Lwandamina hafurahishwi na tabia za mchezaji huyo kujiona yupo juu ya klabu hivyo akauomba uongozi umtafutie striker mwingine na kumpiga chini Ngoma.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here