Home Kimataifa Mohamed Salah, popote ulipo, vuta kiti uagize juisi ya miwa

Mohamed Salah, popote ulipo, vuta kiti uagize juisi ya miwa

11888
0
SHARE

Na Halidi Mtumbuka

Mohamed Salah! Hana bahati huyu Mwarabu wa Misri. Amekosa bahati aliyotunukiwa Jack Wilshere, nayo ni kuzaliwa kwenye udongo unaoongozwa na Malkia. Wilshere alibahatika, akatokeza kwenye vichwa viingi vya habari Uingereza, baadae tukamsahau kama dunia ilivyomsahau Muammar Gadaffi.

Alichobahatika ni kimoja tu, kuufanya mpira uwe rahisi machoni kutoka kwenye mifumo migumu ya kwenye makaratasi. Amebahatika kasi, unaweza kumuona akiwa anatiririka na mpira mithiri ya maji yatiririkapo juu ya mlima Udzungwa. Kitu kigumu hakijawahi kutiririka lakini miguu ya Salah, inatiririka, haikokoti tu mpira!

Maamuzi ya haraka aina ile uwanjani huweza kufanywa na seli pekee ndani ya mwili wa mwanadamu. Hizi ni zile zinazohusika na urejeshaji wa majibu baada ya taarifa kupokelewa na kutafsiriwa ndani ya ubongo wa mwanadamu. Tukio huwa ni haraka kama ambavyo umeme hukifikia kifaa baada ya kuruhusiwa kupita katika njia yake.

Kuna wakati unaweza kuwaza hivi Jose Mourinho alikua sahihi kweli kumtoa kwa mkopo kumpeleka Fiorentina? Alijua thamani ya kuvuja kwake jasho kwa bidii uwanjani? Mourinho alitambua kuwa thamani ya kuutuliza kwake mpira juu ya gamba lake la mguu ilikua ni kubwa zaidi ya Juan Cuadrado? Kuna wakati tukubali tu, lilikua ni dili kichaa!

Maamuzi ya Mourinho ni yake peke yake hapa ulimwenguni. Salah huyu wa Liverpool chini ya Jurgen Klopp si yule wa Fiorentina na mara kumi zaidi ya yule wa Roma. Si tu ule wakati ambao mpira hugusana na viatu vyake tu bali nyakati nyingi uwanjani huzunguka kwa faida.

Ukipata fursa ya kuzunguka mitaa kadha wa kadha nchini Misri hakuna shaka kwamba neno sahihi linaloweza kukuthibitishia uwezo na heshima yake kwenye dunia anayoishi ni kubwa mno. Utasikia wakimuita ‘Messi wa Misri’. Hakuna shaka kwa kuwa yupo Messi mmoja tu, na Misri yupo Messi wa taifa hilo, nae ni Mohamed Salah.

Septemba 5, 2017 jijini Alexandria wingu la furaha lilitanda kila kona ya majukwaa ya Dimba la Borg El Arab, nchini Misri huu ndio uwanja ambao unabeba karibia robo tatu ya mechi zote ngumu nchini Misri kuanzia ngazi ya vilabu hadi timu ya taifa.

Siku hiyo, timu ya taifa ya Misri ilikua ikicheza dhidi ya taifa linalotoka Afrika Mashariki lakini limefanikiwa kupenyeza mizizi yake vizuri tu kwenye udongo mgumu wa soka la Afrika, nalo ni taifa la Uganda.

Siku hiyo kulikua na mwanamume mmoja tu ambaye kama kumwita shujaa, ungepaswa kumwita yeye na si mwingine, ni Mohamed Salah. Alifanya nini? Salah alifanya kadri ya uwezo wake kuhakikisha anaifungia bao muhimu timu yake ya taifa. Na kweli, kufanya kazi kwa kujituma hulipa zaidi ya uvivu.

Salah hakutaka tu kufunga kwenye mchezo huo, alicheza kama mpira unapaswa kuishi dakika zote. Alicheza kama yupo ndani ya jezi nyekundu za Liverpool na alifanya kazi yake yote siku ile. Huwa najiuliza, ni mazoezi ya aina gani ambayo humfanya Mohamed Salah kuwa pumzi kuanzia mwanzo wa mchezo hadi mwisho?

Hiki ni kitu cha ajabu sana kutoka kwenye mwili wake. Ni wazi, nidhamu ya upambanaji inaweza kuwa ndio mazoezi yanayoifanya damu yake kuwa yamoto muda wote uwanjani huku akijumlisha na mazoezi yenyewe. Hakika Misri inapaswa kujivunia kuwa na Messi wao anayeishi Uingereza.

Oktoba 8, 2017 jijini Cairo licha ya pilikapilika nyingi zilizolikumba jiji hilo zitokanazo na shughuli za kawaida za kibinaadamu, timu ya taifa ya Niger ilikua ikiwasili kwenye mchezo wake dhidi ya Misri.

Kama ilivyokawaida ndani ya jiji hilo, huwa si rahisi kuondoka na ushindi kama ambavyo Alexandria pia huwa. Niger ilijiandaa kwa ushindi lakini utashindaje mbele ya Misri yenye Salah wakati huo ambao alikua akihitaji kuchomoza kwenye ulimwengu wa soka la ushindani?

Ilikua ni bahati mbaya kwao, waliishia tu kubugizwa mabao 3-0 kisha Misri ya Salah ikajiweka vizuri kwenye mbio za kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, AFCON. Taifa la Misri limepata mtu ambaye anaweza kufanya shughuli ya Eden Hazard kule Ubelgiji.

Kwanini tusiamini kwamba huenda klabu ya Barcelona inayotajwa kumuwania ipo sahihi? Ofa kama hii ikimjia, Salah asiwe na papara, asitumie nguvu nyingi kama zile ambazo huzitumia akiwa uwanjani, afanye hivi.

Kwanza avute kiti, atulie na ashushe pumzi ndeefu kujipongeza kwani kazi ya miguu yake imewashitua wengi. Baada ya hapo ni kuagiza tu juisi taamu ya miwa yenye ubaridi wa kutosha na kuanza kuivuta kwa mrija kuelekea ndani ya kinywa chake akiwa na jibu moja tu, kwenda kucheza soka Barcelona kwenye mvua za masika na si Liverpool kwenye ukame mkubwa.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here