Home Kitaifa Banda anapeta tu Sauz

Banda anapeta tu Sauz

12071
0
SHARE

Beki wa kati wa zamani wa Simba Abdi Banda anaendelea kupeta kwenye klabu yake ya sasa Baroka FC ya Afrika Kusini inayoshiriki ligi kuu nchini humo (PSL). Banda amecheza mechi zote (12) hadi sasa katika msimu wake wa kwanza kwenye ligi hiyo ambapo zimesalia mechi tatu ili kumalizika kwa mzunguko wa kwanza.

Katika mechi hizo 12, Banda amefunga goli moja huku akiwa ameisaidia timu yake kukusanya pointi 19 na kukaa katika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi. Baroka imeshinda mechi nne, sare saba huku ikiwa imepoteza mchezo mmoja na kufanikiwa kukusanya alama 19, alama mmoja mbele ya wakongwe Orlando Pirates.

Banda amezungumza na shaffihdauda .co.tz na kusema lengo la timu ni kumaliza katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi ili kupata fursa ya kucheza mashindano ya Afrika.

“Bado mechi tatu tumalize raundi ya kwanza, Mungu anasaidia tunajitahidi tumalize katika nafasi nzuri. Jumanne (Dec. 5, 2017) tunakipiga na Mamelodi Sundowns.”

Banda ambaye anafanya vizuri pia akiwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ amesema, kuna tofauti kubwa ya kucheza nje ukilinganisha na nyumbani.

“Mpira unafaida sana ukicheza nje, unapata changamoto mpya uwanjani lakini hata upande wa maslahi si haba. Nimecheza nyumbani kwa miaka mitatu lakini huku nimecheza kwa miezi minne tu tayari nimeona tofauti.”

Jamaa bado anatafuta njia ya kutimiza malengo yake ya kucheza soka barani Ulaya ndoto ambayo ni ya kila mchezaji wa kisasa amekuwa akiiota.

“Sauz mimi napita tu, malengo yangu ni kucheza Ulaya na ninajiamini siku zote nitafanikiwa katika hilo, kama ikitokea mwakani sijanaenda, basi nitacheza timu kubwa hapa.”

Banda anasema, siku zote mwanzo huwa mgumu, lakini akasisitiza kwamba aliamua kujiunga na Baroka akiamini atapata nafasi ya kucheza bila presha kubwa kwa sababu si miongoni mwa timu kubwa zenye presha.

“Siku zote kuanza ndio kugumu, ndio maana niliamua kuanzia chini, tayari kwa sasa mambo sio mabaya nimeshaanza kujenga jina kwenye klabu yangu na hata kwenye ligi pia.”

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here