Home Kitaifa Mwambieni Ndemla saa 21 ni nyingi kuliko saa 172

Mwambieni Ndemla saa 21 ni nyingi kuliko saa 172

13349
0
SHARE

Na Priva Abiud

Usipende mafanikio ya ghafla. Kubali kufurahia kila sehemu ya maisha unayopitia. Said Hamis Ndemla yupo Sweden sasa hivi. Anapata selfie moja mbili tatu. Ndio hata ungekuwa wewe lazima ungepata kumbukumbu, Sweden siyo mbagala.

Alipo Ndemla ukitaka kwenda kama huna nauli ya ndege basi itabidi ukae kwenye gari saa 172 mpaka mji wa Eskilstuna. Huenda leo hii akina Ibrahim Ajibu nao wapo tayari hata kukaa kwenye basi saa 172 ili wafike alipo Ndemla, wasikate tamaa. Akili ya Ndemla kwa sasa huenda haipo Sweden tu. Anawaza na kwingine kama England. Kama hana mawazo hayo basi naye atarudi kama Haruna Moshi ‘Boban’ tu.

Ukipata baiskeli lazima utamani pikipiki. Usipowaza ya juu huwezi kusogea. Ndemla anapaswa kuwaza kusafiri umbali wa kilometa 2006, yaani kutoka Eskilstuna mpaka England. Ni umbali wa saa 21 kwa gari tu. Namshauri yafuatayo kwanza. Itabi apande treni kwanza atokee Sweden kupitia Malmö FC mpaka Copenhagen FC (Denmark). Halafu achanje mbuga mpaka Hamburg SV (Germany) au apitie Brussels (Belgium) na anaweza kutumia usafiri wa treni za Eurostar mpaka London.

Au ndemla apitie ferry barabara ya Hoek van Holland (Netherlands) aende mpaka Harwich (United Kingdom) pia anaweza kupiga zake misele tu mpaka Amsterdam (Netherlands) atokee Newcastle (United Kingdom).

Ukiweza kufungua mlango madirisha hayakusumbui. Twende taratibu utaelewa kwa nini nimetaja hizo safari zote. Ndemla yupo karibu kufika mbingu ya soka. Ndemla England ni kilometa 2006 kutoka hapo ulipo na hapo ulipo kurudi Tanzania ni kilometa 12,488.9. Lakini ni rahisi sana kurudi Tanzania kuliko kwenda London.

Ndemla hujatumia nguvu nyingi kwenda Sweden ukilinganisha na Mbwana Samatta kwenda Ubelgiji. Ndemla kufanikiwa Ulaya ni kazi sana kaka. Labda tu nikupe mfano wa mtu ambaye alikuwa palepale England lakini aliruka viunzi vingi.
Si unamjua Jarmie Vardy? Huyu jamaa alizaliwa Sheffield Uingereza. Alianzia soka pale Stocksbridge iliyokuwa ligi daraja la 8 mwaka 2007. Akiwa na Miaka 20 tu alikuwa mfungaji bora wa timu na aliisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa na kuipandisha daraja la 7.

Baadae alisafiri mpaka klabu ya Halifax Town inayocheza daraja la 7 mwaka 2010 wakati nyie mkisema ‘Ari mpya Nguvu mpya na Kasi’. Hapo pia alikuwa mfungaji bora na aliwapa kombe na timu hiyo kupanda daraja la 6, mwanaume hakukata tamaa akaenda Fleedtwon iliyokuwa daraja la 5 mwaka mmoja baadae. Hapa napo aliipeleka timu daraja la 4 kwenye Historia ya klabu hiyo akabeba kombe huku akaongoza ligi kwa magoli 31.

Ujue bado anazunguka pale pale England, anahangaika kuja ligi kuu. Najua huko kasulu kigoma wapo akina Ndemla wengi wanataka kuja Simba. Ila watafikaje Dar? Simba na Yanga wapo akina Ndemla kibao ila wanatoa wapi nauli kwenda Sweden?

Hatimaye Vardy alifika mjini Leicester. Huenda alifurahi kama wewe ulivyotua tu pale uwanja wa Tunavallen Eskilstuna Sweden baada ya mateso mengi ukiwa benchi na kisinglendi chako cha njano njano au cha blue ukimsubiri Niyonzima achoke uingie. Najua Ndemla mwingine yupo Kyela huko anatarajia kuuza mikungu ya ndizi kule Matola Mbeya mjini ili apate nauli ya Luwinzo aje Dar nae atoke kimaisha.

Jamie Vardy hakuwa na maisha mazuri sana Leicester licha ya kufunga magoli 16 yaliyoiwezesha kutwaa ubingwa na kuipandisha daraja la kwanza na kwenda ligi kuu. Alipofika ligi kuu hali haikuwa nzuri. Alitapatapa kama kijana wa Rombo aliyeuza mbege ili aje afungue duka mjini.

Mwaka 2014 alipambania kibanda chake cha Leicester kisipigwe ‘x’ kikashushwa daraja. Nafahamu unakumbuka alichokifanya 2015 alipotwaa ubingwa ambao ni mgumu kuliko yote duniani…akiwa mfungaji bora namba mbili nyuma ya Kane Harry.

Ndemla umeelewa maana ya hizo safari za Vardy? Basi hizo ndo safari zako za tren za Denmark, Uholanz, na Ubelgiji? Ukienda Ubelgiji sio lazima uende kwa Samatta, wewe nenda mpaka Brussels, ingia Jimbo la Mzee Eric Thomas meya Anderletch, utakutana na kiwanja kikubwa cha Constant Vanden Stock utamkuta Boss wa klabu hiyo Bwana Roger Vanden Stock ana pesa mingi na ni mtu mkubwa ukicheza pale ndio umetoka mzee baba.

Mimi sikumaanisha unapita tu kama msafiri. Nilimaanisha usije ukawa Haruna Moshi. Nasema hivi nenda kacheze soka maeneo hayo, zipo klabu nyingi kubwa kule. Pambana. Jikaze kama Vardy. Usikate tamaa. Usipokamuliwa kaka hutoi maziwa.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here